MKURUGENZI
wa Taasisi ya Munanta Med Company Ltd na wataalamu wa afya wametembea
jamii za pembezoni ikiwemo wafugaji wa Tarafa ya Engaranaibo Wilayani
Longido Mkoani Arusha kwa kuwapatia vifaa na elimu ya kujikinga na
maambukizi ya virusi vya corona ili kuhakikisha nao wanaepuka kupata
tatizo hilo.
Munanta Med
pamoja na kutoa elimu hiyo kwenye masoko na minada pia, maofisa
watendaji na wenyeviti wa vijiji, viongozi wa kimila, waganga wa jadi na
wakunga wamepatiwa mafunzo ya kupambana na corona.
Mkurugenzi
wa taasisi hiyo, Dk Juma Muna akizungumza jana wakati akitoa mafunzo
hayo alisema lengo ni kuongeza uelewa hasa kwa jamii zilizopo pembezoni
ambapo elimu haijawafikia zaidi.
Dk
Muna alisema eneo la tarafa ya Engaranaibo lipo vijijini mpakani mwa
nchi ya Kenya na wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na Namanga mkoani
Arusha hivyo elimu hiyo inatakiwa kutolewa kwa ukubwa zaidi.
Alisema
jamii hizo za wafugaji hukutana kwenye mnada uliopo Engaranaibo, bila
kuwapa elimu ya kujikinga na corona wengi wao wataathirika ndiyo sababu
wakafika kuwaelimisha.
Alisema
ikiwa ni miezi kadhaa tangu corona iingie nchini ni wajibu wa wadau
kutoa elimu ya afya katika kujikinga na janga hilo ikiwemo kunawa mikono
kwa maji tiririka na sabuni na kuvaa barakoa na kutokaribiana.
"Ukishawapa
elimu hii viongozi wa kimila, wakunga wa jadi na waganga, tegemea jamii
ya wafugaji kwa ujumla itanufaika kwani huwa wanawasikiliza mno
viongozi wao tofauti tungewaeleza sisi wenyewe," alisema Dk Muna.
Alisema
pamoja na elimu hiyo pia walitoa baadhi ya vifaa vya kujikinga na
corona ikiwemo sabuni za kunawia mikono lita 65, ndoo 13 za kuweka maji
tiririka na barakoa 100.
"Pia
tumewaeleza kuwa maji yanapaswa kuosha mikono walau kwa sekunde 20
kukaa umbali wa mita moja na kufuata miongozo yote inayotolewa na
serikali wa idara ya afya," alisema Dk Muna.
Mkazi
wa eneo hilo, Yamati Ole Motika alishukuru taasisi ya Munanta Med kwa
kuwapa elimu ya namna ya kuepuka maambukizi na pia vifaa vya kujikinga
na corona.
Motika
alisema jamii za pembezoni huwa zinasahauliwa kwenye masuala mbalimbali
kutokana na jiografia yao ila wanashukuru kwa wao kukumbukwa.
Alitoa
ombi kwa wadau mbalimbali wajitokeze kuwasaidia kwani jamii ya wafugaji
waliopo pembezoni nao wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma hasa
kipindi hiki cha kupambana na corona.
Mkurugenzi wa taasisi ya Munanta Med, Dk Juma Muna (kushoto)
akiwakabidhi viongozi wa Kata ya Engaranaibo Wilayani Longido Mkoani
Arusha, Ally Hussein, sabuni za kunawia mikono lita 65, ndoo 13 na
barakoa 100 kwa ajili ya wananchi wa eneo hilo kujikinga na maambukizi
ya virusi vya corona jana.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...