Kombo Kessy Mhanga wa ajali picha ya kwanza kabla hajapata ajali,picha inayomuonyesha akiwa amepata ajali na amekatwa miguu yote miwili,picha ya tatu Kombo Kessy akiwa katika picha ya pamoja ma mkewe.

Na Veronica Ignatus.
"Hivi ninavyozungumza nawe nina Barua inayonipa siku 14 nilipe kodi ya Nyumba Tsh. 170, 000/ au niondoke kwenye nyumba niliyopanga, Nina Mke na watoto watano,Nimechanganyikiwa sijui nifanyaje .. Ajali kutokana na mwendo kasi imeharibu  kabisa Maisha yangu." Anasema Kombo Kessy almaarufu Kessy, mkazi wa Dodoma.

Kilio hiki cha Kessy kinaturejesha miaka 6 nyuma, usiku wa Agosti 16, 2014 ambapo ajali ya kusababishiwa, iliyotokana na mwendo kasi, imemsababishia Ulemavu wa kupoteza Miguu yake yote miwili na kuyabadili kabisa Maisha yake yaliyojitegemea kiuchumi, Maisha yaliyotosha kumlisha mkewe na wanae watano.

Kombo Kessy anasimulia kuwa, akiwa kwenye harakati zake za kusaka riziki kutokana na kazi yake ya kupiga picha za mnato na jongefu (video), alipata tenda kutoka kwa mwimbaji mashuhuri wa Taarabu, Bibi Shakira (sasa Marehemu) aliyekuwa na onesho jijini Mwanza.

Baada ya kumaliza zoezi na mizunguko yake, wakati anarejea nyumbani kwake Buzuruga, akakumbuka kuwa Bi Shakira alimwachia Mkoba amhifadhie. Ikamlazimu kuelekea Nyegezi ili kumpelekea mkoba huo.

Alipofika maeneo ya Igogo Tanesco, eneo ambalo maji hupita barabarani na mchanga kujaa pale Mvua inaponyesha alikuta ajali imetokea.

"Nakumbuka  ilikuwa Ijumaa usiku, Mvua kubwa sana ilinyesha. Maji yalikuwa yanapita barabarani. Nikiwa kwenye gari langu, niliona Gari mbele yangu linakuja kwa mwendo kasi sana. Mara likapiga kwny tuta, ule Mchanga na maji yaliyokuwepo likaangukia upande wa Pili. Ikabidi nipaki gari langu kitu cha Igogo Tanesco niende kuwasaidia." Anasema Kessy huku akiishika miguuu yake iliyosalia kuanzia kwenye ugoko pekee.

Eneo hilo, Kessy anasema huwa na utelezi sana na mchanga mvua inapoonyesha. Hivyo uendeshaji Gari kwa mwendo mkali huonesha wazi agano na Kifo.

"Wakati nikiendelea kusaidia kuokoa, mara Gari jingine ambalo baada ya ajali nililitambua kuwa ni Toyota Verona, liliikuja kwa kasi upande tulipokuwa. Kwa kutumia medani zangu za karate nikaruka ili kukwepa lakini nilikuwa  nimeshachelewa. Nikajikuta nimekaa chini. Wakati nataka kusimama ili nisaidie wengine nikaona Miguu mizito. Nikachukua simu mfukoni na kumulika, mguu wa kulia nikaona umekatika usawa wa ugoko na Mguu wa kushoto zimesalia nyama kuanzia gotini kwa chini kidogo. Nikamshukuru Mungu"

Kombo Kessy, mwenyeji wa Tanga, anayesema awali alifahamika sana jijini Mwanza kwa upigaji picha,akimiliki ofisi yake, alijikuta kitandani kwa takribani miaka miwili mpaka kupona kabisa. Maisha yakampiga na kumfilisi kila kitu hivyo ikamlazimu kuhamia Dodoma ili ajaribu Maisha katika Mkoa mwingine.

Kessy ambaye alilazimika kuuza baadhi ya mali zake ikiwemo Gari ili kumudu Maisha mapya,licha ya mihangaiko yake ya kila siku Mkoani Dodoma, bado haingizi Fedha za kukidhi kuhudumia familia yake ikiwemo kuwasomesha wanae. Matokeo yake sasa amepewa notice ya kuondoka kwenye chumba alichopanga, ndani ya siku 14 vinginevyo atatolewa kinguvu na Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa na Askari Jamii.

Hili linamtesa zaidi akikumbuka alivyoweza kuihudumia familia yake kikamilifu akisafiri mikoa karibu yote kufanya shughuli zake za upigaji picha.

"Hivi ninavyozungumza nawe nina Barua inayonipa siku 14 nilipe kodi ya Nyumba Tsh. 170, 000/- au niondoke kwenye nyumba niliyopanga,Kuna muda huwa nawaza mpaka nakufuru. Madereva wasio makini kwa mwendo kasi wanaharibia sana Maisha wengine. Gari ni kama Bunduki lisipokuua litakujeruhi. Lazima madereva walijue hilo." Anasema Kessy kwa uchungu.

Natazama katika Mitandao ya Kijamii na kukutana na kisa cha Dereva Mwanamke wa Mabasi ya mikoani ambaye amenukuliwa akisimulia, "Madereva wengi hawako makini kabisa barabarani hasa nyakati za usiku. Mtu eneo la spidi 50 anakwenda 80. Nafikiri Sheria kali ziongezwe kuwabana madereva wazembe wasiojali Maisha ya wengine."

Kauli hii inafanya nipekue kujisomea Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, Kifungu cha 51 (8) kinazungumzia maeneo machache tu yanayozuiliwa mwendo kasi kama vile maeneo ya makazi ya watu na yale ya mijini. Licha ya maeneo hayo machache bado hayatiliwi mkazo hasa ufuatiliaji kama kweli mwendo kasi unazingatiwa na adhabu
zinatekelezwa pale unapokiukwa.

Rozan Emmanuel, mwanafunzi wa Kidato cha nne kutoka Ruvu Sekondari anabainisha wazi kuwa mwendo kasi ni mwendo ambao umezidi kiwango kile kilichowekwa na alama za usalama barabarani kama vile Vibao vya Mwendo wa Kilomita 50 kwa saa. Mwanafunzi huyo ambaye ni mmoja wa wanafunzi walio Klabu za Usalama Barabarani anasema
ameshuhudia ajali mbalimbali ambazo mazingira yalionesha wazi dereva kushindwa kulimudu gari kutokana na mwendo kasi."Mara nyingi hutokea pale madereva kwa madereva wanaowahi abiria katika kituo kinachofuata.

Pia sisi abiria huwa tunachangia kutokana na kutaka tuwahi katika shughuli
mbalimbali kama vile wanafunzi kuwahi shuleni, wafanyakazi kuwahi ofisini. Abiria hufanya hivi pasi na kujua kuwa mwendo kasi unaweza kuleta vifo, ulemavu na hivyo kupoteza nguvu kazi ya taifa na kuyumbisha uchumi." Anasema Rozan huku akitoa wito kwa madereva kutofuata kile wanachotaka abiria badala yake kufuata sheria inachosema.

Boniface John,mfanyabiashara ndogo ndogo anasema kuwa kutokana na biashara yake hutumia vyombo vya usafiri kwa kiasi kikubwa. Anasema mwendo kasi umesababisha ulemavu na kifo kwa rafiki zake ambao waliparamiwa na gari lililotoka nje ya barabara
baada ya dereva kushindwa kulimudu.

"Nilishangaa tu wenzangu wako chini, kwenda tukakuta gari dogo limewavamia baada ya dereva kushindwa kulimudu kutokana na mwendo kasi ... Fikiria kutafuta kwetu riziki  ndio kama hivi barabarani, sasa ukipata ulemavu au madhara ndio basi tena."

Inaelezwa kuwa licha ya uwepo wa mwendo kasi, suala la kufunga mikanda linaweza kupunguza madhara makubwa kwa abiria kwa kati ya asilimia 50 mpaka 70. Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini LATRA zimesisitiza wazi ufungaji wa mikanda kwa magari yote ya abiria, mizigo na binafsi. Hata hivyo jambo hili ambalo  lilipaswa kupewa nguvu zaidi na sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, halimo. Hii ikimaanisha halina nguvu ya kisheria.

Jambo hili linanirejesha kwenye tafiti za Shirika la Afya Duniani (WHO) ambazo zinaonesha kuwa takribani watu milioni 1.25 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali za barabarani huku zaidi ya watu milioni 20 wakipata ulemavu kila mwaka. Ajali hizi kwa kiasi kikubwa husababishwa na mwendo kasi na madereva kutoheshimu alama za usalama barabarani. Hii ni nguvu kazi ambayo inapotea kutokana na ajali.

Nchini Tanzania, Takwimu za ajali za Barabarani zinaonesha kuwa 76% ya ajali zinazotokea husababishwa na uzembe wa madereva huku mwendo kasi ukiwa mmojawapo na ni 8% pekee ya ajali husababishwa na ubovu wa barabara. Hii ikimaanisha kuwa endapo mwendo kasi utadhibitiwa kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza ajali za barabarani kama sio kutokomeza kabisa na hivyo kutopoteza nguvu kazi ya taifa.

Nguvu kazi hii ni akina Kombo Kessy ambao wanajikuta wamebadilishiwa mfumo wao wa maisha kwa ulemavu wa kusababishiwa kutokana na mwendo kasi wa madereva wengine. Wakati mwingine wao wenyewe. Hii ni nguvu kazi inayotegemewa na familia, ndugu, jamaa,
marafiki na serikali katika mapato ya ndani.

Nini kifanyike?

Kessy anaamini fika madereva wanapaswa kukagua magari yao kwa utimamu na kuendesha magari kwa mwendo ambao wana uhakika kuwa lolote likitokea wanaweza kulimudu gari

"Nimeshawahi kupatwa na ajali zaidi ya tano wakati naendesha gari ikiwemo mbili ambazo tairi la mbele lilipasuka. Kwakuwa nilikuwa kwenye mwendo mdogo ilikuwa rahisi kulimudu gari na kutosababisha madhara makubwa. Madereva wawe makini, sijawahi kuona dereva ambaye aliua au alisababishia madhara wengine halafu maisha yake yakarejea
kwenye hali ya kawaida tu. Lazima ataishi maisha ya hovyo baada ya ajali
hiyo."

Rozan Emmanuel licha ya kusisitiza madereva waache tabia ya kuwasikiliza abiria wanachotaka, anaiomba serikali kutowafumbua macho maredeva wanaoendesha magari kwa mwendo kasi kwani wanalitia hasara taifa ikiwemo kuharibu barabara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...