Anthony Ishengoma

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amekabidhi Pikipiki 14 kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wao na kuonya kuwa hatarajii kuona pikipiki hizo zikitumika nje ya shughuli za Serikali.

Kiongozi huyo wa Mkoa wa Shinyanga amekabidhi pikipiki hizo kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli na kuwataka maafisa tarafa hao kuhakikisha pikipiki hizo zinatunzwa vizuri ili wengine waweze kuzitumia na kuwaonya watendaji hao kutotumia pikipiki hizo kubeba abiria kama ilivyo kwa madereva bodaboda.

Aidha Bi. Telack amewataka Maafisa Tarafa hao pamoja na kupewa pikipiki mpya pia wahakikishe wanatunza Ofisi walizojengewa pamoja na vifaa walivyopewa kwa lengo kuwezesha mazingira mazuri ya utendaji kazi zinatunzwa vizuri akionya kuwa baadhi yao tayari washaanza matumizi mabaya ya vifaa hivyo.

‘’Wapo watu wanafanya vizuri na tumeanza kuona mnavyofanya kazi vizuri, yapo matatizo mengine mmeanza kuyashughulikia endeleeni lakini niwahusie kuwa zile kompyuta ni kwa ajili ya matumizi ya kazi za Serikali zisitoke kwenda sehemu yoyote fanyeni kazi kwani nasi tunafarijika kuona mnafanya kazi na kutupunguzia mzigo.’’Aliendelea kusema Bi. Zainab Telack Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa pia aliwataka Maafisa Tarafa hao kuwasimamia watendaji wa kata ili waeze kutatua migogoro inayowakabili wananchi akiongeza kuwa lengo la Serikali ni kuona wananchi wa Shinyanga wakiishi kwa furaha na amani na kutambua uwepo wa viongozi wao.

Bi. Telack amewataka Maafisa Tarafa kutunza pikipiki hizo kutokana na uwepo wa mahitaji makubwa ya pikipiki katika jamii nakuwazuia wasisimame nazo katika mabaa na kuonya kuwa Afisa yoyote atakayesema kuwa Pikipiki yake imeibiwa hataeleweka.

Wakati huo huo Afisa Tarafa Bw. Cleophasi Mdui amempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia vitendea kazi maafisa hao baada ya kuwaita Ikulu Juni 4, mwaka jana na kuhaidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kulipa fadhila kwa kiongozi Mkuu wa Nchi.

Naye Afisa Tarafa kutoka Old Shinyanga Bi. Neema Mkandala amesema usafiri huo utawawezesha Mafisa Tarafa hao kutatua kero za wananch kwa haraka ikiwemo kufika maeneo yenye shida na kutoa maelekezo kwa wananchi kwa lengo la kuboresha ufanisi.

Pikipiki hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais John Pombe Magufuli kama kutimiza ahadi yake kwa Maafisa hao aliyoitoa tarehe 4 Juni mwaka jana Ikulu jijini Dar es Salaam. 
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akikabidhi Pikipiki 14 kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Shinyanga mapema leo Ofisini kwake Mjini Shinyanga.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akiongea na vyombo vya habari pamoja na  Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Shinyanga mapema leo Ofisini kwake Mjini Shinyanga wakati wakuwakabidhi pikipiki 14 maafisa hao zilizotolewa na Rais John Pombe Magufuli kwa lengo la kuboresha utendaji wao.
 Bw. Cleophasi Mdui Afisa Tarafa –Kahama akijaribu kuwasha moja ya  pikipiki iliyokabidhiwa kwake na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack mapema leo Ofisini kwake Mjini Shinyanga.
.Neema Mkandala  Afisa Tarafa –Old Shinyanga akijaribu kuwasha moja ya  pikipiki iliyokabidhiwa kwake na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack mapema leo Ofisini kwake Mjini Shinyanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...