Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha UDOM, Dk Ombeni Msuya (kushoto) akikabidhi Mashine za kunawia kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwa Mchungaji Anituja Msuya (kulia) wa kanisa la Usharika wa Ndanda, Usangi Mwanga kama mchango wake dhidi ya mapambano ya Corona.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha UDOM, Dk Ombeni Msuya (kushoto) akikabidhi Mashine za kunawia kwa Mchungaji wa Kanisa la KKKT usharika wa Msambeni, Ugweno Mwanga ukiwa ni mchango wake kwa makanisa ya Wilaya hiyo kwa ajili ya kujikinga na Corona.
Waumini wa Kanisa la Msambeni, Ugweno wilayani Mwanga wakimsikiliza Dk Ombeni Msuya wakati alipofika kutoa msaada wa mashine za kunawia kwa ajili ya kujikinga na Corona.

Charles James, Michuzi TV
KATIKA kuendelea na uungaji mkono serikali dhidi ya mapambano ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Corona, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Ombeni Msuya leo amekabidhi mashine 10 za kunawia kwa Taasisi za Dini wilayani Mwanga, Kilimanjaro.

Dk Msuya kupitia Taasisi yake ya Dk Msuya amekabidhi mashine hizo zenye ndoo na sabuni zake kwa makanisa yaliyopo katika Tarafa za Ugweno na Usangi Wilayani Mwanga ambazo zote kwa pamoja zina thamani ya Sh Milioni 2.5.

Akizungumza wakati akikabidhi mashine hizo Dk Msuya amesema ameguswa kuchangia mashine hizo baada ya kuona nia njema ya serikali katika mapambano ya ugonjwa huo.

Dk Msuya amesema serikali chini ya Rais Dk John Magufuli imeonesha jambo la kiimani kwa kuruhusu nyumba za ibada ikiwemo Makanisa na Misikiti kuendelea na shughuli zake kama kawaida kwa watu kuabudu tofauti na Nchi zingine ambazo zimepiga marufuku.

" Ndugu zangu kama kijana wenu ambaye mmenilea hapa nimeguswa na kushawishika kuleta vifaa hivi ambazo naamini vitakua msaada mkubwa kwenye makanisa yaliyopo kwenye Wilaya yetu. Ni wajibu wangu kama mtanzania pia kushirikiana na serikali katika mapambano haya.

Nafahamu tunapaswa kumtegemea Mwenyezi Mungu lakini kupitia vifaa hivi pia tunajilinda na maambukizi ya ugonjwa huu. Tuendelee kuhamasishana kwa pamoja katika kufuata ushauri wa kitaalamu ambao serikali yetu kupitia wataalamu wake imekua ikiutoa kwetu juu ya ugonjwa huu," Amesema Dk Msuya.

Aidha ameahidi kuchangia Mabati 50 kwa ajili ya kumaliza Ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Msambeni lililopo Tarafa ya Ugweno huku akiwaomba waumini wengine kuungana nae katika kufanikisha Ujenzi huo.

Pia Dk Msuya ameahidi kununua Kompyuta na Mashine ya Printer ambayo ameombwa na Kanisa la KKKT Tarafa ya Usangi ambapo vyote hivyo ameahidi kuvitoa kabla ya mwezi Juni.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo Mchungaji Eliewaha amemshukuru Dk Msuya kwa kuguswa kwake na kuwaletea mashine hizo ambazo amesema zitakua msaada tosha kwa wananchi ambao wanaenda makanisani sehemu ambayo ina mkusanyiko wa watu mbalimbali.

" Hakika tumefarijika kuona kijana wetu ambaye tumekulea ukiwambuka wazazi wako na kutuletea mashine hizi. Ungeweza kuwa mbinafsi na kugawa kwa kanisa lako tu lakini umegawa kwa makanisa tofauti yaliyopo wilayani kwetu, Tukusihi uendelee na moyo huo huo," Amesema Mchungaji Eliehawa.

Dk Msuya jana pia aligawa vifaa hivyo kwenye Soko la Kikweni na Zahanati ya Mamba ambapo pia amewaomba watanzania wengine wenye uwezo kushirikiana na serikali katika mapambano haya ya kujikinga na maambukizi ya Corona.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...