Ofisa Mipango wa Taasisi ya Haki Fursa Kwagilwa Reuben (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi habari leo Mei 27 , 2020 jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa Rais Dk.John Magufuli kupewa tuzo maalumu ya kutambua na kuthamini mchango wake katika kupambana na janga la Corona nchini.Kushoto ni Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo Ntimi Charles na kulia ni Ofisa Ustawi wa Jamii wa taasisi hiyo Lwitiko Mwakikuti.
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Haki Fursa Ntimi Charles (katikati) akisikiliza kwa makini swali kutoka kwa moja ya waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa mkutano uliotishwa na taasisi hiyo kwa ajili ya kutoa pongezi zao kwa Rais Dk.John Magufuli kwa jinsi alivyofanikiwa kupambana na vita dhidi ya Corona.Wengine ni Ofisa Mipango wa taasisi hiyo Kwagilwa Reuben(kushoto) na Ofisa Ustawi wa jamii Lwitiko Mwakikuti(kulia).
Ofisa Mipango wa Taasisi ya Haki Fursa Kwagilwa Reuben(katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 27 mwaka 20202 jijini Dar es Salaam.Kulia ni Ofisa Ustawi wa jamii Lwitiko Mwakikuti na kushoto Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Haki Fursa Ntimi Charles.
Kwagilwa Reuben ambaye ni Ofisa Mipango wa Taasisi ya Haki Fursa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.Kulia ni Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Haki Fursa Ntimi Charles.
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Haki Fursa Ntimi Charles(kushoto) akiwa makini kusikiliza maswali ya waandishi wa habari.Kulia ni Ofisa Ustawi wa jamii Lwitiko Mwakikuti.
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Haki Fursa Ntimi Charles(wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wengine wa taasisi hiyo baada ya kumaliza kwa mkutano kati yao na waandishi wa habari uliofanyika leo Mei 27 mwaka 2020 jijini Dar es Salaam.


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

TAASISI isiyo ya kiserikali ya Haki Fursa imemshauri Spika wa Bunge Job Ndugai kuandaa tuzo maalum kwa ajili ya kumtunuku Rais Dk.John Magufuli ikiwa ni ishara ya heshima ya kutambua mchango wake mkubwa ambao ameutoa katika mapambano dhidi janga la Corona kwani kupitia uimara, weledi, uzalendo na hulka yake ya kujali imetuwezesha Watanzania kushinda vita hiyo.

Pia imesema wakati Spika wakimuomba kuandaa tuzo hiyo ambayo wanatamani kuona Rais Magufuli anakabidhiwa siku ambayo atakwenda kuvunja Bunge, taasisi hiyo imepedekeza kila watu, kila taasisi wampongeze Rais na ikiwezekana kwa kufanya maandamano , watu kubeba picha ya JPM na kuendesha mijadala kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kumpongeza.

Wakizungumza leo Mei 27 mwaka 2020 jijini Dar es Salaam, viongozi wa taasisi hiyo wamefafanua kwa kina namna amavyo Rais Magufuli amewaongoza kwenye mapambano ya vita ya Corona na ukweli kuna kila sababu ya kutoa shukrani na pongezi nyingi kwa Rais na kwa kuwa Muhimili wa Bunge ndio wenye kuwakilisha wanannchi, basi Spika wa Bunge Job Ndugai ni vema akaandaa tuzo maalumu na kisha kumkabidhi Rais kama ishara ya kutambua kazi kubwa ambayo ameifanya kukabiliana na janga la Corona.

Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Haki Fursa Ntimi Charles amesema kuwa wameamua kukutana leo na waandishi wa habari kwa ajili ya kumpongeza Rais Magufuli kwa namna alivyojitoa kikamilifu na kwa ujasiri kutuvusha kwenye janga hili la corona.Rais Magufuli ni zaidi ya shujaa wa nchi kwa hili ambalo amelifanya kwa ajili ya Watanzania.

"Katika hili tunamuomba Spika wa Bunge Job Ndugai kuandaa tuzo maalum ya kumpongeza Rais na tunatamani kuona tuzo hiyo akikabidhiwa siku ya kufunga Bunge na iwe tuzo ya karne. Tunaamini na kutambua kuwa bila sisi Watanzania kujitoa na kumthamini Rais wetu hakuna mtu anayeweza kumpongeza.

"Hivyo sisi kama taasisi binafsi tunachukua jukumu hili kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa ya kishujaa aliyoifanya.Hatua kadhaa ambazo amechukua kukabiliana na janga hilo mataifa mengine duniani nayo yameamua kufuata mbinu za Rais katika kukabiliana na Corona.Ameruhusu watu kwenda kwenye nyumba za ibada wakati wengine wameshindwa , hili ni jambo la kumpongeza Rais ,Watanzania katika mapambano ya Corona tulianza na Mungu na tumemaliza na Mungu,"amesema Charles.

Ametumia nafasi hiyo kueleza Dunia imeshuhudia Rais Magufuli akitoa maono ya kugeukia tiba na mbinu za kiafrika kama vile dawa za Madagasca na zilzogunduliwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania(NIMR).Rais alituma timu ya maofisa waandamizi wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje kwenda Madagasca kufuata tiba ya asili na imeingia nchini.

Amesisitiza kuwa "Hapo Rais anadhihirisha kuwa ana maono ya Afrika ianze kujitegemea kwenye masuala ya msingi kama tiba za jadi kunapokuwa na changamoto kama hizo na tayari mataifa mengi yamefuata dawa hiyo ya Madagasca ambayo taarifa zinaonesha imewatibu wagonjwa wengi.Dhana ya utegemezi kwa waafrika si jambo ambalo mabeberu wanalipenda hata kidogo lakini Rais Magufuli amelisisitiza na matokeo yake wagonjwa wengi wamepona,"amesema.

Kwa upande wake Ofisa Mipango wa Taasisi ya Haki Fursa ameeleza katika mapambano dhidi ya Corona, Rais Magufuli amekuwa mwangalifu kwa miongozo ya Shirika la Afya Duniani(WHO) pamoja na Shirika la Usimamizi wa Fedha Duiani(IFM)."Pia Rais amefunga shule, akasitisha michezo , akapunguza mikusanyiko isiyo ya lazima huku akisisitiza watu wafanye kazi wakichukua tahadhari za watalaamu wa afya.

"Tunaona watu wana barakoa , kunawa maji yanayotiririka kwa sababu.Tunaona watu wakiitikia maagizo ya kutokaribiana sana lakini wakiruhusiwa kusali kwa Mungu wao kwani kwa nchi yetu kusali ni haki ya kiraia. Kwa ajili ya Covid-19 Rais Magufuli kaajiri madaktari zaidi ya 300 na kaongeza bajeti ya vifaa na usimamizi mzima wa janga hili.Kama haitoshi kaunda timu ya kitaifa kusimamia upimaji na utangazaji wa matokeo ya waliogua na waliokufa kila mara inapotokea.

"Hadi sasa kila mkoa una mpango mkakati wa kukabiliana na Corona kwa kuratibu na kutenga bajeti ya kutosha na kuweka miundombinu sahihi kwa mujibu wa muongozo wa Rais na watalaamu wa afya wakiongozwa na Wizara ya Afya.Rais Magufuli akaenda mbali zaidi ili ahakikishe anajua ukweli kuhusu vipimo na uhalisia wa tatizo la ugonjwa , akatuma kwa siri sampuli za oil za magari,papai, nanasi, mbuzi, njiwa na vitu mbalimbali ili kujua ukweli kinachopimwa ni kweli.

"Matokeo yakaja vyote vimeambukizwa!Hii ikamthibitishia Rais kuwa kuna hujma katika upimaji na utangazaji matokeo.Wananchi wanaposikia watu wanakufa tena wengi wanajaa hofu.Hofu ni hatari zaidi ya ugonjwa Covid-19, hali hiyo inapotanda katika nchi watu huishia kusita kuzalisha mali na ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji unapungua na hivyo kuathiri uchumi wa nchi.

Amesisitiza kwa jinsi Rais alivyosimama imara kwenye mapambano dhidi ya Corona kuna kila sababu ya kumpongeza na kufafanua mbali ya kuokoa maisha ya Watanzania ameokoa uchumi na kunusuru Taifa kuingia kwenye mkumbo wa mataifa mengine yaliyoiga mpango wa kuzuia watu kutoka nje(Lockdown) na kwamba hatua hiyo ingechochea uchumia wa Tanzania kuchechemea.

"Tunapaswa kufahamu sio kwamba Rais hakuwa na uwezo wa kuagiza nchi iwe Lock down lakini kwa upendo na kutambua Tanzania inategemewa na nchi karibu nane ambazo zinatuzunguka na mchango wa bandari ya Dar es Salaam kwa nchi hizo pamoja na maeneo mengine yote muhimu, aliamua kutofunga mipaka nchi wala kufungia watu wake ndani. Watanzania tunapaswa kupuuza watu wote wanaombeza Rais kwani tunafahamu kuwa hii ilikuwa vita ya tatu ya dunia.Hivyo tumuombe Spika aandae tuzo kwa ajili ya kumpongeza Rais wetu kwa niaba yetu Watanzania,"amesema.

Wakati huo huo Ofisa Ustawi wa Jamii wa taasisi hiyo, Lwitiko Mwakikuti, amesema Rais Magufuli kwa kinywa chake akimpongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa namna alivyoweza kufanyakazi nzuri kwenye janga hili la corona, hivyo kama yeye amempongeza Waziri yeye atapongezwa na nani kama siyo Watanzania wenyewe."Hivyo tunakila namna ya kujivunia na kumpongeza Rais wetu."

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...