Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS)limewashauri wananchi na wafanyabiashara wote nchini kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini wazalishaji wa bidhaa za umeme hususani nyaya, zisizo na viwango ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa upimaji na ugezi wa Bidhaa kutoka TBS Johanes Maganga alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kuibuka kwa malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara kuhusu uwepo wa baadhi ya viwanda hapa nchini vinavyozalisha nyaya hizo zisizo na ubora na hivyo kutishia usalama wa wananchi pamoja na mali zao.

Kutokana na malakamiko hayo, Maganga amefafanua kuwa milango ya TBS ipo wazi wakati wote hivyo ni muda muafaka kwa wananchi, wafanyabiashara kwenda na kutoa taarifa juu ya uwepo wa viwanda vinavyozalisha nyaya hizo ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi yao

“Tunawakaribisha muda wote na kutoka mahali popote waje hapa ofisini kwetu kutupa taarifa ya watu hao ili tuweze kujiridhisha na kisha tuchukue hatua kali dhidi yao kwa kuwa sheria ipo wazi kwa yeyote anayeikuka taratibu zilizowekwa kisheria na mamlaka husika” amesema Maganga.

Ameongeza kwamba TBS imekuwa na utaratibu wa kutoa leseni za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za umeme kwa kuweka utaratibu wa viwango vinavyotakiwa hivyo kama kuna kiwanda chochote kinazalisha chini ya ubora hilo litakuwa ni kosa ambalo mhusika anapaswa kuwajibishwa jambo alilotaka litolewe taarifa pale linapojitokeza.

Aidha Maganga amesema pamoja na malalamiko hayo kutolewa, TBS haitakaa kimya na badala yake itaendelea na utaratibu wake wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara viwandani na kwenye maduka ili kuona kama viwango stahiki vinafuatwa ikiwa ni utaratibu wa usimamizi wa sheria zilizopo.

Siku za karibuni kulijitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wa vifaa mbalimbali vya umeme jijini Dar es Salaam wakidai juu ya uwepo wa biashara ya nyaya zisizo na ubora zinazozalishwa na baadhi ya viwanda hapa nchini na kuiomba Serikali kupitia Shirika la viwango Tanzania (TBS) kufanya msako viwandani na madukani ili kuwabaini wahusika

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kariakoo, baadhi ya wafanyabiashara hao pamoja na wanunuzi wa bidhaa hizo wamedai kumekuwepo na wimbi la uzalishaji wa bidhaa hizo hususani nyaya za umeme za majumbani ‘wiring’ zisizo na viwango unaohitajika.

Wafanyabiashara hayo waliojitambulisha kwa majina ya Rashid Salum pamoja na Frank Mtonga waliopo eneo hilo, walisema kumekuwepo na bidhaa hizo katika baadhi ya maduka ya kariakoo na hivyo kusababisha maduka yanayouza bidhaa zenye viwango bora kukosa wateja kutokana na wananchi wengi kukimbia kwa kigezo cha bei na kuzifuata nyaya zisizo na ubora kutokana na unafuu wa bei bila kujua athari zake.

“Kuna maduka mengi hasa maeneo ya mitaa ya Narungombe na maeneo mengine yanye maduka yanayouza bidhaa hiyo, wanauza nyaya ambazo hata ukizitamaza kwa macho utabaini kuwa hazina ubora, kigezo kikubwa kinachofanya wananchi wazikimbile ni unafuu wa bei” ameeleza Salum

Kwa upande wake Mtonga amesema yeye kama mfanyabiashara aliwahi kupokea lawama kutoka kwa baadhi ya wateja wake, waliomtuhumu kuwauzia nyaya zisizo na ubora, suala alilodai kuwa hakulifahamu kwa kuwa hakuwa na uelewa wa kutosha juu ya nyaya hizo na viwango vyake.

Akitolea mfano katika suala hilo, Mtonga amesema kwa nyaya zenye ubora wa viwango ambazo zinauzwa kwa wastani wa Sh 100,000, huuzwa kwa wastani wa hadi 70,000 kwa nyaya zisizokuwa na ubora wa viwango na hivyo kuathiri ushindani wa bei katika sokoo huku pia zikileta madhara kwa wananchi yakiwemo ya nyumba kuungua.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...