Na Mercy Kaanaeli
Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania, Jumamosi ya Mei 23 liliendesha ibada ya shukrani ikiwa ni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kumshukuru Mungu kwa kusikia maombi ya Tanzania na kuiepusha nchi na Janga la ugonjwa wa COVID-19.
Ibada hiyo ya shukrani iliendeshwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania, Mchungaji Mark Walwa Malekana, katika kanisa la Ushindi lililopo Mikocheni B jijini Dar es Salaam, mahali ambapo pia ni makao makuu ya Taasisi ya Vyombo vya Habari vya Kanisa la Tanzania TAMC, na kuhudhuriwa na washiriki mbalimbali pamoja na waandishi wa Habari.
Akizungumza katika Ibada hiyo, Mchungaji Malekana alieleza mambo 4 yanayoonesha Shukrani halisi kwa Mungu wa Mbinguni.
“Jambo la kwanza ni kujitoa kuwa Dhabihu kama inavyoelekezwa katika Warumi 12:1, jambo la pili ni kutoa Sadaka ya Shukrani, jambo la tatu ni kuwasaidia maskini na jambo la nne ni kujitoa katika kazi na kutimiza majukumu ya kijamii kikamilifu”, alisema Mchungaji Malekana.
Askofu Malekana, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Vyombo vya Habari vya Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania, alisisitiza kuwa mtu hawezi kusema anamshukuru Mungu kwa kwenda katika kumbi za starehe, kulewa vileo na kufanya anasa kwa madai ya kufurahia, bali shukrani ya dhati sharti itoke moyoni na idhihirishwe kwa matendo safi.
“kumshukuru Mungu, sio kujishukuru sisi, sio kujipongeza sisi, sio kula na kunywa na kuvaa, lakini ni kutoa kwanza sadaka ya roho zetu, na pili kutoa sadaka kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kwahiyo watanzania na waumini wote wa kanisa hili, popote wanaposali, nawaomba watoe sadaka maalum kwa Mungu wetu Shukrani. 
Lakini pia tunamshukuru Mungu kwa kuwasaidia wahitaji, hilo ni jambo la muhimu sana. Katika nchi yetu kuna jamii kubwa imepoteza makazi kwa ajili ya mafuriko kutokana na mvua zilizonyesha nchini, kuna jamii inayoishi katika hali ya ufukara zaidi, kwahiyo katika suala la kumshukuru Mungu, niwakumbushe watanzania kuwasaidia wahitaji hawa”, alisisitiza Mchungaji Malekana.
Ibada hii ya shukrani iliambatana na maombi maalum ya kumuombea Rais Magufuli na Serikali yake ili Mungu azidi kuwaongoza katika kazi kubwa waliyonayo ya kuiongoza Tanzania.
Baadhi ya waumini waliozungumza na Sauti Kuu baada ya Ibada hiyo, walionyesha kufurahishwa kwao na ibada iliyoendeshwa.
“nimefurahi sana kupata fursa ya kuja kanisani kumshukuru Mungu, hasa ukizingatia tunaendelea na siku 100 za maombi, napenda kumshukuru Rais wetu kwa kutuongoza kushukuru kwani wengi wetu hatujapata ugonjwa wa COVID-19 hivyo tuendelee kumshukuru Mungu, na tuendelee kuchukua tahadhari zote zinazoelekezwa”, alisema Lucy Selemani.
“Leo imekuwa Sabato ya pekee sana kwani tumekuwa na viongozi wetu wa kanisa mchungaji Malekana, na ametuongoza katika ibada hii ya maombi ya shukrani, tukiungana na Rais wetu Dkt. Magufuli ambaye alituelekeza kufanya maombi ya Shukrani, kwahiyo leo hapa kanisani tumebarikiwa sana na tumefurahi sana na tunamshukuru Mungu kuwa kama Tanzania ameendelea kutulinda dhidi ya ugonjwa huu wa COVID-19. Tuendelee kuchukua tahadhari zote, lakini tunaamini kwamba Mungu wetu anatupenda na ameendelea kutulinda na watanzania wote tumekuwa mashahidi juu ya hilo”, alisema Magessa Wandwe, Mzee wa Kanisa Ushindi.
“Napenda kumshukuru sana Mungu kwa ibada ya leo kwani ukilinganisha na Ibada zilizopita, ya leo imekuwa tofauti kwani imekuwa na watu wengi zaidi na hii ni kutokana na ukweli kwamba Mungu ametutendea miujiza na hii corona imekuwa ni adui anayeenda kufa sasa. 
Tuko katika siku 100 za maombi ambazo zinaisha mwezi Julai, na ningependa kusisitiza tuendelee kumuomba sana Mungu kwani bado kuna mambo mengi yanaendelea, tumuombe Mungu aingilie kati, atuongoze, atusaidie, na tusikate tamaa, tusiache kuomba, Biblia inasema ‘ombeni bila kukoma’, tusiache kuomba na Mungu atatusaidia. Napenda kuwakaribisha wale ambao walikuwa na hofu hata ya kuja kanisani kuwa sasa mambo yanaenda kufunguka na Mungu anazidi kutubariki. Tuendelee kuchukua tahadhari kila inapobidi”, alisema Mathias Mavanza, Mzee wa Kanisa Ushindi.
Jumapili ya Mei 17, Rais Magufuli alipozungumza na watanzania mara baada ya ibada aliyohudhuria katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Chato aliwaomba viongozi wa dini kuiongoza tena Tanzania katika siku nyingine 3 za maombi za Maombi ya kumshukuru Mungu kuanzia ijumaa Mei 22 hadi jumapili Mei 24, na wakati huu ni maombi ya kumshukuru Mungu kwa kutupigania.
Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni kote linaendelea na ibada ya maombi ya siku 100 yaliyoanza Aprili 4 na yatahitimishwa Julai 27 2020. Mambo makuu yanayoombewa katika siku hizi 100 ni Kujazwa Roho Mtakatifu, Uamsho wa mtu Binafsi na janga la COVID-19, ambapo masomo mbalimbali hutolewa kila juma na waumini huyasoma na kufanya maombi kila siku. Ni Imani ya Kanisa kuwa siku hizi 100 za maombi zitakapohitimishwa, Mungu atakuwa ametutendea makuu sana, kama ambavyo tayari taarifa za sifa zimeanza kutangazwa Tanzania na maeneo mengine ya Ulimwengu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...