Na Abdullatif  Yunus Michuzi TV.

Wananchi na Wakazi wa Miji ya Kyaka, Bunazi na maeneo ya jirani, Wilayani Missenyi Mkoani Kagera huenda wakaondokana na changamoto ya upatikanaji wa Huduma ya Maji inayowakabili kwa sasa, kufuatia kuanza Kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa Maji ikiwa ni ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa kwa wakazi hao, akiwa ziarani Mkoani Kagera Mwaka Jana.

Mradi huo mkubwa unaotarajiwa kukamilika Juni 2021, umezinduliwa rasmi na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo wakati alipofika Wilayani Missenyi na kujionea hali halisi, huku shughuli za awali zikiwa tayari zimeanza tangu Mei 11,2020 na huku mradi huo ukitarajia kugharimu jumla kiasi cha shilingi Bilioni 15.1, wakati ambapo kwa sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya Maji safi na salama ni asilimia 72 sawa na Wananchi 179,555 kati ya Wananchi 202,632.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika Ukumbi wa Halmashauri Wilayani Missenyi, Profesa Kitila, amesema kuwa Mradi huo mkubwa ni wa kwanza Mkoani Kagera na Kanda ya Ziwa ambao Serikali itapeleka Maji kwa Wananchi kutoka Mto Kagera, jambo ambalo halikuwahi kufanyika kwa miaka yote, kwani Mara nyingi Wananchi wamekuwa wakitegemea Maji ya Visima.

Aidha Profesa Kitila ameongeza Serikali ya awamu ya Tano imeendelea kutatua kero ya maji maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi 792, huku miradi 633 ikiendelea kujengwa, huku asilimia kubwa ya Miradi hiyo inatekelezwa kupitia Fedha za Ndani, isipokuwa miradi 41 ambayo inategemea fedha za Wahisani, na kwa  Kanda ya Ziwa Serikali kupitia Ziwa Victoria inatekeleza miradi kumi mikubwa, katika Miji kumi na Tatu ambayo itagharimu Tirioni 1.2.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ambao pia ni wasimamizi wa mradi Ndg. Leonard Msenyele amesema kuwa MWAUWASA, RUWASA na BUWASA tayari wamekamilisha mchakato wa kumpata Mkandarasi ambae ni China Civil Engineering & Construction Corporation (CCECC) na tayari wameingia nae mkataba wa shughuli za awali ambazo zitagharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni Tisa ikiwa ni loti ya kwanza, huku loti ya pili ikitarajiwa kufanyika kwa njia ya "Force Account" ambayo itagharimu Shilingi Bilioni 5.7.
 Pichani ni wanaonekana Vijana ambao wamekuwa wakifanya shughuli za kuuza Maji ya Mto Kagera kwa wakazi wa Mji wa Kyaka wakati ambapo Dumu moja huuzwa kati ya Shilingi 500 hadi 700.
 Pichani ni Profesa Kitila Mkumbo Katibu Mkuu Wizara ya Maji wakati akizungumza na Wananchi wa Kata Kyaka, akiwa katika eneo ambapo shughuli za Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mto Kagera zitafanyika.
 Pichani Wanonekana Wakazi wa Mji wa Kyaka Wilayani Missenyi wakiteka Maji ya Mto Kagera ambayo yamekuwa msaada mkubwa kwao licha ya Maji hayo yamekuwa yakitumika bila kutibiwa.

 Pichani ni Mkandarasi wa Ujenzi wa Mradi wa Maji Kyaka Bunazi Mr. Lee kutoka Kampuni CCECC, Akiwa anaendelea kumsikiliza Profesa Mkubo (hayupo pichani) wakati wa kikao na Wananchi wa Kyaka
 Pichani ni Ndg. Leonard Msenyele Kaimu Mkurugenzi Mtendaji MWAUWASA akitoa Taarifa ya kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi, katika Ukumbi wa Halmashauri Missenyi.

Pichani wanaonekana watoto wakazi wa Kyaka wakitokea kuteka Maji, ambapo hutembea zaidi ya kilomita 7 kufuata Maji hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...