Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akisisitiza jambo wakati akizungumza na Uongozi wa Bodi ya Kahawa Ofisini kwake Mjini Bukoba, leo tarehe 4 Juni 2020.
 (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akisisitiza jambo wakati akizungumza na Uongozi wa Bodi ya Kahawa Ofisini kwake Mjini Bukoba, leo tarehe 4 Juni 2020. 
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam akiteta jambo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg Emmanuel Sherembi wakati wa ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Richard Ruyango akisisitiza umuhimu wa elimu kutolewa kwa vyama vya Ushirika kuhusu kuimarisha ubora wa kahawa wakati wa kikao kazi na watendaji wakuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania pamoja na vyama vya Ushirika vya Wilaya hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi na wanunuzi binafsi wa Kahawa katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba leo tarehe 4 Juni 2020. Wengine pichani ni Afisa Biashara wa Mkoa wa Kagera Ndg Isaya Tendega akimuwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa (Kushoto), Meneja wa Bodi ya Kahawa kanda ya Kagera Ndg Melkiad Masawe (Wa pili kutoka Kulia) na Kaimu Mwonjaji wa kahawa na Dalali Mkuu Bodi ya Kahawa Tanzania, Rogatus Meela (Wa kwanza kulia) 
Sehemu ya wanunuzi binafsi wa Kahawa wakifatilia maelekezo ya serikali yaliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam kuhusu ununuzi wa Kahawa katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba leo tarehe 4 Juni 2020. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kagera
MKUU wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema kuwa serikali inaunga mkono wanunuzi binafsi kwenye zao la Kahawa japo wamechelewa sana kuingia sokoni kuanza kununua kahawa za wakulima.

Gaguti ameyasema hayo leo tarehe 4 Juni 2020 wakati akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam ofisini kwake Mkoani mjini Bukoba na kuwataka wanunuzi hao kuingia sokoni.

"Serikali haitaki maneno inataka wakulima wapate fedha kwa wakati, wanunuzi binafsi wamechelewa sana kuingia sokoni tulitegemea waingie sokoni tangu mwezi wa pili waanze kuingia makubaliano na Vyama vya Ushirika, lakini hawajachelewa sana waje ofisini kwangu waeleze wazi wanataka kahawa kiasi gani kisha tuingie makubaliano ya awali" Alikaririwa Rc Gaguti

Ameongeza kuwa Wanunuzi binafsi wanapaswa kujitokeza hadharani watoe ofa yao ikieleza kuwa wanataka kununua kiasi gani cha kahawa ili kuhuisha maneno yao kwa matendo.

Awali katika mkutano uliofanyika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkuu wa Wilaya hiyo, Richard Ruyango alisisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia mipango yake katika zao la Kahawa hususani kuimarisha usimamizi madhubuti ili kuwa na kahawa Bora kwa kuongeza tija na Uzalishaji.

Kuhusu wanunuzi binafsi amesema kuwa wanapaswa kutekeleza sheria, na taratibu za ununuzi wa zao hilo ikiwa ni pamoja na kuwa na kibali cha ununuzi kinachotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halamshauri husika pamoja na kuwa na leseni ya Biashara inayotolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof. Jamal Adam akizungumza na wanunuzi wa Kahawa katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba ameweka bayana utaratibu wa ununuzi wa kahawa ya wakulima katika Mkoa wa Kagera ambapo Wanunuzi watakaoruhusiwa kununua kahawa ni wale waliopata leseni za kununua kahawa kwa mujibu wa kanuni ya 26 ya Kanuni za Kahawa 2013. 

Ameongeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri watapaswa kutoa vibali kwa haraka kwa wanunuzi wenye sifa ili kuiwezesha Bodi kutoa leseni kwa wakati. 

Kadhalika, Prof Jamal amesisitiza kuwa Wakurugenzi wanapaswa kuwajulisha kwa maandishi waombaji watakaonyimwa vibali wakiweka bayana sababu za kutowapatia vibali na nakala ya barua hiyo iwasilishwe Bodi ya Kahawa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kwa upande wao wanunuzi wa kahawa wamepongeza uamuzi huo wa serikali kuwaruhusu kununua kahawa kwenye vyama vya Ushirika huku wakiahidi kutekeleza taratibu na sheria za ununuzi wa Kahawa.

Akizungumza kwa niaba ya wanunuzi hao Afisa Masoko wa Kampuni ya Karagwe Estate Ltd Ndg Kamanzi Mombeki amesema kuwa Kampuni hiyo imejipanga kurejea tena katika ununuzi wa kahawa baada ya kusimamia kwa zaidi ya miaka miwili kufanya Biashara hiyo.

"Sisi kama Kampuni tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa kurejesha wanunuzi binafsi kununua kahawa hivyo nasi tumerejea kwa nguvu na Ari kubwa katika ununuzi wa kahawa" Alisema Mombeki.

Amesema kuwa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kuhusu wanunuzi binafsi wakati akizungumza na wananchi wa Kyaka, Rwamisheye, Kemondo Muleba, Nyakabango na Kyamyorwa mkoani Kagera tarehe 11 Julai 2019 yalilenga kuongeza ushindani wa kibishara jambo ambalo linamnufaisha zaidi mkulima mwenyewe.

Mombeki ameonyesha kuwashangaa watu wanaopinga maelekezo ya Dkt Magufuli yenye lengo la kumkomboa mkulima.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...