TAMKO LA MHE. MUSSA AZZAN ZUNGU (MB.),
WAZIRI WA NCHI - OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA KWA UMMA KUHUSU
MAADHIMISHO YA KIMATAIFA YA SIKU YA KUPAMBANA NA KUENEA KWA HALI YA JANGWA NA
UKAME DUNIANI, TAREHE 17 JUNI, 2020
Ndugu Wananchi,
Kila mwaka tarehe 17 Juni, nchi yetu huungana na nchi
nyingine duniani kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali
ya Jangwa na Ukame. Kimataifa Maadhimisho ya Siku hii yanafanyika Jijini Seoul
nchini Korea Kusini. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Tudhibiti Kuongezeka kwa Uzalishaji wa
Chakula na Malighafi; Tukabiliane na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame” (Food.
Feed. Fibre). Kaulimbiu hii inaelimisha jamii kuzalisha chakula na
malighafi kwa njia endelevu ili kunusuru ardhi kutokana na hali ya Jangwa na
Ukame. Aidha, Jamii inaelimishwa juu ya uhusiano wa Uzalishaji, Ulaji na Matumizi
ya Ardhi.
Ndugu Wananchi,
Maadhimisho ya siku hii yalitangazwa na Mkutano Mkuu wa Umoja
wa Mataifa uliofanyika mwezi Januari, mwaka 1995 kwenye Azimio namba 115. Azma
ya maadhimisho haya ni Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani kama
njia mojawapo ya utekelezaji wa shughuli za Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa
Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (United Nations Convention to
Combat Desertification) uliopitishwa mwaka 1992 ambapo nchi yetu ni
mwananchama.
Ndugu Wananchi,
Kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ni moja ya changamoto za
hifadhi ya Mazingira inayotishia uzalishaji wa chakula, ustawi wa jamii na
maendeleo ya kiuchumi duniani kote. Hivyo, maadhimisho haya yanahimiza kuwepo
kwa uwiano mzuri wa njia za uzalishaji, aina ya mazao yanayozalishwa na tabia
ya ulaji ili kuepuka uharibifu wa ardhi na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame. Aidha, Kauli mbiu hii inalenga kukuza uelewa
na kuhamasisha jamii kubadili mazoea ya kufanya shughuli za uzalishaji na
matumizi ya rasilimali yasiyo endelevu kama vile, kufyeka misitu na kuchoma
moto hovyo maeneo makubwa kwa ajili ya kupata ardhi ya kilimo na hivyo kuchangia
uharibifu wa ardhi na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.
Ndugu Wananchi,
Umuhimu wa kuadhimisha siku hii pamoja na mambo mengine
umezingatia matokeo ya taarifa za tafiti mbalimbali duniani. Tafiti hizi
zinaonyesha kuwa asilimia ishirini na tatu (23%) ya ardhi yote duniani haina
uwezo wa kuzalisha. Aidha, asilimia sabini na tano (75%) ya ardhi yote duniani
imebadilishwa kutoka kwenye hali yake ya asili na kuwa kwenye matumizi mengine
ya ardhi hasa kilimo. Tathmini iliyofanywa na Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja
wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame imebaini kuwa
ifikapo mwaka 2030, uzalishaji wa chakula cha kukidhi ongezeko la idadi ya watu
duniani utahitaji hekta milioni mia tatu (300Ha) zaidi. Tathmini hii,
inaonyesha kuwa mahitaji ya malighafi za kuzalisha nguo na viatu yanachangia
asilimia nane (8%) ya uzalishaji wa gesijoto duniani ambapo yanatarajiwa
kuongezeka kwa takribani asilimia hamsini (50%) ifikapo mwaka 2030.
Ndugu Wananchi,
Tangu mwaka 1994 nchi zilizoridhia Mkataba huu, Mashirika ya
Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa yasiyokuwa ya Kiserikali pamoja na
wadau wengine, huadhimisha siku hii kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazohusu
kupambana na tatizo la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame. Maadhimisho ya siku
hii yameendelea kuwa fursa muhimu katika kuhamasisha jamii kuchukua hatua
katika ngazi zote ili kujenga ushawishi wa kupambana na kuenea kwa hali ya
jangwa na ukame kwa nchi wanachama na Dunia nzima.
Ndugu Wananchi,
Ili kukuza uelewa wa jamii na kuhamasisha ubunifu kwa
wanafunzi na vijana katika masuala ya hifadhi ya mazingira hususan kupambana na
kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali wameandaa shindano la kuandika Insha kuhusu hifadhi ya
mazingira kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vijana wa vyuo vya
elimu ya juu. Lengo la shindano hili ni kuelimisha kizazi cha sasa kuhusu Mazingira
hususan Kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, Mabadiliko ya
tabianchi, pamoja na Hifadhi ya Bioanuai, hapa nchini.
Ndugu Wananchi,
Suala
la matumizi bora na endelevu ya ardhi ni muhimu katika kupambana na kukabiliana
na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, kwani kasi ya uharibifu wa mazingira ya
ardhi na vyanzo vya maji inaongezeka kutokana na ukataji wa miti hovyo, ufugaji
holela, kilimo cha kuhamahama, uchimbaji madini holela, uendelezaji wa makazi
holela na kutokuzingatia maelekezo
ya wataalam kunazidisha ukubwa wa tatizo hili. Kutokana na changamoto hizo, pamekuwepo na ongezeko la ukame, upungufu
wa mazao ya chakula na biashara pamoja na kuongezeka kwa hali ya umaskini
miongoni mwa jamii za watanzania.
Ndugu Wananchi,
Mnatambua kwamba nchi yetu ina uhitaji
mkubwa wa ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kuzalisha chakula na uendelezaji wa
shughuli za ufugaji kutokana na ongezeko la idadi ya watu. Tafiti zinaonyesha
kwamba asilimia sitini na moja (61%) ya ardhi ipo katika hatari ya kugeuka
jangwa na asilimia kumi na sita (16%) ya nchi nzima imekwisha onyesha dalili za
wazi za kuwa jangwa. Aidha, utegemezi mkubwa wa rasilimali kama misitu
umechangia kwa kiasi kikubwa katika tatizo. Tafiti zinaonyesha kuwa, asilimia
themanini na tano (85%) ya watanzania wanategemea kuni na mkaa kwa ajili ya
kupikia. Utegemezi huu husababisha upotevu wa hekta mia tatu sabini na mbili
elfu (372,000Ha) za misitu kila mwaka.
Ndugu Wananchi,
Juhudi nyingi zimefanyika ili kupambana na kuenea kwa hali ya
jangwa na ukame hapa nchini. Juhudi hizo ni pamoja na, programu maalumu ya
Mpango wa Kudhibiti Ukame (2018) ambapo utafiti wa kubainisha
maeneo kame umeanza kufanyika nchi nzima; Sheria, Kanuni, Miongozo, Programu na
Matamko mbalimbali kwa kuzingatia sekta ambazo zina utegemezi wa moja kwa moja na
ardhi.
Mipango na Mikakati mingine ni kama Mkakati wa Kuhifadhi
Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji, 2006, ambao unatekelezwa katika mikoa
yote Tanzania bara. Moja ya maelekezo ya
mkakati huu ni kupanda miti milioni moja na nusu(1,500,000) kila mwaka kwa kila
halmashauri; Programu ya Pili ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II 2017/18 -
2028/29) ambayo inatekelezwa nchi nzima; Uanzishwaji wa Mashamba mapya ya Miti ambapo
jumla ya hekta elfu moja mia saba na thelathini na nne (1,734) zimepandwa
katika mashamba mapya ya miti ya Wino (Songea), Iyondo Msimwa (Ileje),
Biharamulo (Chato), Mpepo (Mbinga), Buhigwe (Kigoma) na Mtibwa/Pagale
(Mvomero). Aidha, shamba jipya kwa ajili ya uzalishaji wa gundi inayotokana na
miti ya migunga lenye ukubwa wa hekta 50,000 limeanzishwa katika Wilaya ya
Iramba (Singida).
Juhudi nyingine ni kuwepo kwa Mpango wa Mfumo wa Taifa wa
Matumizi ya Ardhi (2013 – 2033) ambao unatekelezwa katika mikoa yote Tanzania
bara; uhamasishaji wa matumizi ya Nishati Mbadala wa Mkaa na Kuni ambapo majeshi,
shule, vyuo, hospitali, na baadhi ya hoteli za kitalii hapa nchini zinatumia nishati mbadala wa mkaa; uhamasishaji
wa usimamizi Shirikishi wa Misitu ambapo jamii zinashiriki kulinda na kuhifadhi
misitu na hivyo kunufaika na misitu hiyo.
Ndugu Wananchi,
Pamoja na utekelezaji wa Sheria, Mipango na Mikakati
mbalimbali ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame hapa nchini,
Serikali imeelekeza jamii kuongeza juhudi katika utekelezaji wa mipango na
mikakati hiyo. Maelekezo haya ni pamoja na kuendeleza kampeni ya upandaji miti
milioni moja na nusu (1,500,000) kila mwaka kwa kila Halmashauri, kutekeleza Mpango
wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame ambapo kila sekta
imepewa jukumu la kuutekeleza na kuhuisha Mpango huu katika Mipango yao ya
Kisekta; kuendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusu kupambana na kuenea kwa Hali ya
Jangwa na Ukame pamoja na athari zake; kusimamia na kutekeleza Kanuni bora za
Matumizi endelevu ya Ardhi zilizoelekezwa kwenye Mpango wa Kitaifa wa Matumizi
ya Ardhi.
Ndugu Wananchi,
Katika kupunguza utegemezi wa nishati ya kuni na mkaa ambayo
husababisha ukame na kuenea kwa jangwa, Serikali, ipo katika ujenzi wa Bwawa la
kuzalisha Umeme la Julius Nyerere Hydropower Station lenye uwezo wa kuzalisha
megawati za umeme zaidi ya elfu mbili mia moja kumi na tano (2,115MW). Umeme
huu utapatikana kwa bei rahisi na hivyo kuwezesha wananchi wa kawaida na
taasisi kutumia umeme kama nishati ya kupikia. Sambamba na hilo serikali inaendelea
na ujenzi wa reli kwa ajili ya treni ya umeme (Tanzania Stardard Gauge Railway-SGR) kwa lengo la kupunguza
msongamano wa magari katika barabara zetu na hivyo, kupunguza uzalishaji wa
gesijoto unaosababisha mabadiliko ya tabianchi ambayo huchangia kuwepo kwa hali
ya jangwa na ukame.
Ndugu Wananchi,
Mtakumbuka kuwa mwaka 2018 Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania alizindua Kampeni ya kuifanya Dodoma iwe ya kijani na
kuelekeza Kampeni hii itekelezwe mikoa yote. Lengo la kampeni hii ni kupunguza
kasi ya uharibifu wa ardhi katika jiji la Dodoma kwa kupanda na kutunza miti. Katika
kampeni hii jumla ya miti milioni moja mia nne na mbili elfu mia nane kumi na
mbili (1,402,812) ilipandwa kati ya mwaka 2018 hadi 2020 katika ukubwa wa hekta
elfu tatu mia tano na saba nukta mbili (3,507.2Ha) katika maeneo mbalimbali ya
Mkoa wa Dodoma na kati ya miti hiyo asilimia themanini na moja nukta saba tatu
(81.73%) inafanya vizuri. Aidha, mafanikio ya Kampeni hii ni chachu ya
kuendeleza shughuli za upandaji miti katika mikoa mbalimbali hapa nchini na
hivyo kuchochea juhudi za Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame.
Ndugu Wananchi,
Ili kutekeleza kampeni ya Mhe. Makamu wa Rais, kwa kipindi
cha mwaka 2018/19 nchi yetu iliweka malengo ya kupanda miti milioni mia tatu
kumi na tatu mia moja tisini na sita elfu mia tano (313,196,500) katika mikoa
yote. Ili kufanikisha lengo hili, kiasi cha miti iliyopandwa ni milioni mia
mbili na tisa miasaba sitini na saba elfu mia nane kumi na tano ( 209,767,815)
ikiwa ni asilimia sabini na mbili nukta sita (72.6%) ya lengo zima. Kati ya
miti yote iliyopandwa, iliyopona ni miti milioni mia moja hamsini na tatu, mia
mbili themanini na nane elfu, mia nane arobaini na tano (153,288,845) sawa
asilimia sabini na tatu nukta moja (73.1%) ya miti yote iliyopandwa. Hali hii
inaonyesha kuwa wananchi wanafanya juhudi kubwa katika kukabiliana na hali ya
jangwa na ukame kwa njia ya kupanda na kutunza miti.
Ndugu Wananchi,
Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza
wadau wote wa Mazingira walioshirikiana na Serikali kuandaa na kusimamia
program mbalimbali za kupambana na hali ya ukame na kuenea kwa jangwa hapa
nchini. kwa madhumuni ya kudhibiti kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula na malighafi
ili tukabiliane na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.
Kwa namna ya pekee
navishukuru vyombo vya habari kwa kufanya jitihada za kuelimisha umma juu ya
kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame nchini.
Asanteni
kwa Kunisikiliza.
MUSSA
AZZAN ZUNGU (MB)
WAZIRI
WA NCHI – OFISI YA MAKAMU WA RAIS
MUUNGANO
NA MAZINGIRA
17 JUNI,
2020
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...