KATIKA  kile alichoeleza kuwa ni kuimarisha sekta ya misitu ili iweze kutoa mchango unaostahili kwa jamii na taifa kwa ujumla, Kamishna Mhifadhi wa Misitu, Profesa Dos Santos Silayo amesema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)umeingia  makubaliano ya miaka mitatu ya upatikanaji wa malighafi ya miti, kutoa mitaji na kuwatafutia masoko ya mbao wafanyabiashara wanaovuna misitu katika mashamba ya miti ya serikali.

Prof. Silayo amesema hayo jana mjini Dodoma katika mkutano na wadau wa sekta ya misitu ambao ulilenga kutoa mrejesho wa hatua zilizochukuliwa na TFS baada ya kukusanya maoni, kero na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo muhimu nchini kwa ajili ya kuzitafutia utatuzi wa haraka katika kikao kilichofanyika Juni 17, 2020.

“Ili tuweze kujenga nchi na hasa kupitia sekta ya Misitu ni vyema kujadiliana na kukubaliana mambo kwa misingi ya uhifadhi ambapo sisi tumeamua leo tuje na rasimu ya mkataba itakayokwenda kuwahakikishia upatikanaji wa malighafi kutoka kwenye mashamba ya miti ya Serikali kwa miaka mitatu badala ya mwaka mmoja (mwaka wa fedha) kama tulivyokuwa tunawapa.

“Hatutaishia kuwapa malighafi tu, tunaenda mbali zaidi kuhakikisha mnakuwa na mitaji itakayowawezesha kuwekeza kwenye viwanda vya kisasa vya misitu, tumewaleta wenzetu wa NMB ili waweze kuwaeleza kwa upana juu ya fursa za mitaji katika biashara ya mazao ya misitu.

“Katika ukuajiaji wa viwanda, masoko ya ndani na nje ni muhimu kwa juhudi binafsi au za serikali kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade). Hivyo leo tumewalea watalamu wa masuala ya biashara kutoka TanTrade kutupatia uzooefu juu ya masoko. Hii yote ni kutaka kuhakikisha sekta ya viwanda vya misitu nchini inakuwa,” alisema Prof. Silayo.

Alisema utaratibu huo utaanza kutumika rasmi mara baada ya pande zote mbili kuafikiana kwenye mambo ya msingi ambapo kupitia kikao hicho waliafikiana.

Aidha, Prof. Silayo aliwaongezea muda wavunaji waliolipia mgao wa miti kwenye mashamba ya miti ya serikali na kushindwa kumaliza zoezi la uvunaji ndani ya mwaka huu wa fedha kama mkataba unavyowataka kutokana na janga la Covid- 19.

“Tunatambua shughuli nyingi za uchumi ziliathirika na kusimama kutokana na janga hili la Covid -19 na hivyo ninawaongeza miezi michache wavunaji wote waliomaliza kulipia gharama za mgao wa miti katika mwaka huu wa fedha unaoisha Juni 30, 2020 ili waweze kumaliza zoezi la uvunaji.

Kwa upande wake Mtafiti na Mchambuzi wa masuala ya biashara ya kilimo na chakula kutoka NMB Ability Kakama anasema benki yao imeona fursa iliyopo kwa wafanyabishara wa mazao ya misitu na hivyo wameamua kuwapatia mikopo na huduma nyingine za kifedha kutokana na umuhimu wa sekta ya misitu katika ukuwaji wa uchumi wa nchi.

“Mdau Mkubwa wa NMB ni Rabo benki ya Uholanzi inayojishughulisha na wakulima na hivyo tunapoamua kuwekeza kwa wafanyabishara wa mazao ya misitu tunaangalia mnyororo mzima wa sekta ya misitu, niwashukuru TFS kwa kutukutanisha na wadau hawa ambao sasa tunakwenda kuwapa huduma za kifedha zitakazosaidia kukuza viwanda na hatimaye kuongeza ajira nchini,” alisema Kakama.

Wakati huo huo Ofisa Biashara wa TanTrade, Gilbert Waigama alisema mazao ya misitu hayana tatizo la masoko isipokuwa tu ni namna ya wadau wanaofanya bishara hiyo kushindwa kuyafikia.

“Kikao hiki cha leo kimekuwa na tija kwani kwa pamoja tumekubariana kuanzisha Exporters Association ambapo kitawaongezea tija katika kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakwenda kuyafikia masoko mbalimbali,’ alisema Waigama.

Katibu wa Umoja wa Wavunaji Magogo SaoHill (UWASA), Dk.Basil Tweve anasema kupitia mkataba huo mpya wa upatikanaji malighafi sasa wanakwenda kukuza biashara ya sekta ya misitu nchini kutokana na kuwa na sifa za kukopa kiwango kikubwa cha fedha tofauti na awali walipokuwa hawana uhakika wa upatikanaji malighafi na hivyo kukosa sifa za kukopa mkopo mkubwa kwenye taasisi za fedha.

Katika mkutano huo wadau wa misitu walipata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo ushauri na kero mbalimbali wanazokumbana nazo katika sekta hiyo ambazo ziliahidiwa kufanyiwa kazi kwa haraka na TFS.  Miongoni mwa hoja hizo ilikuwa Magorofani wa uvunaji uzingatie vipindi vya mwaka na kalenda ya mwaka wa fedha wa Serikali.

Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya Wavunaji wa Miti katika Mashamba ya Miti ya Serikali.

 Kamishna wa Mhifadhi wa Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) Profesa Dos Santos Silayo akizungumza kuhusu makubaliano yaliyoingiwa ya upatikanaji wa malighafi ya miti,kutoa na kuwatafutia masoko ya mbao wafanyabiashara wanaovuna misitu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...