Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (katikati) pamoja na ujumbe aliyoambatana nao wakiwa katika kikao cha ndani katika ofisi za kampuni ya umeme ya TEXPOL iliyopo wilayani Uyole Mkoani Mbeya, walipofanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji wa umeme iliyofanywa na kampuni hiyo katika vijiji sita vya wilaya hiyo, Julai 4,2020. Miongoni mwa nyumba zilizounganishiwa umeme na kampuni ya umeme ya TEXPOL iliyopo wilayani Uyole Mkoani Mbeya, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati pamoja na ujumbe wake walifanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji wa umeme iliyofanywa na kampuni hiyo katika vijiji sita vya wilaya hiyo, Julai 4,2020.

Muonekano wa miundombunu ya umeme iliyosimikwa na kampuni ya umeme ya TEXPOL kwa ajili ya kusambaza umeme kwa wananchi wa Wilaya ya Uyole Mkoani Mbeya, Naibu Katibu Mkuu Wiraza ya Nishati pamoja na ujumbe wake walipofanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji wa umeme iliyofanywa na kampuni hiyo katika vijiji sita vya wilaya hiyo, Julai 4,2020.

Kibao kinachoeleza jukumu na dhumuni halisi la kampuni ya umeme ya TEXPOL iliyopo wilayani Uyole Mkoani Mbeya, Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Nishati pamoja na ujumbe wake walifanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji wa umeme iliyofanywa na kampuni hiyo katika vijiji sita vya wilaya hiyo, Julai 4, 2020. Kampuni hiyo ilifanya kazi ya kusambaza umeme kwa wananchi badala ya lengo mama.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, (mwenye suti nyeusi katikati) akipata maelezo ya mashineumba iliyofungwa na kampuni ya umeme ya TEXPOL iliyobainika kuwa na kasoro katika ufungaji wake, kutoka kwa Kaimu Kamishna Msaidizi wa umeme wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (wapili kulia), kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Ufundi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu, na Kushoto ni Meneja Uzalishaji Umeme na Masoko wa Mamlaka ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Nda’nzi Kiboko, walipofanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji wa umeme iliyofanywa na kampuni hiyo katika vijiji sita vya Wilaya ya Uyole mkoani Mbeya, Julai 4,2020.

**********************************

Na Zuena Msuya, Mbeya

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja amesema kazi ya kusambaza umeme iliyotekelezwa na Kampuni ya TEXPOL katika Kaya zaidi ya mia tatu za Vijiji sita vilivyopo katika Kata ya Ilungu, Wilaya ya Uyole mkoani Mbeya haridhishi.

Mhandisi Masanja alisema hayo baada ya kufanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme iliyofanywa na kampuni hiyo kwa lengo la kuona, kujiridhisha na kutathmini ubora wa kazi na miundombinu iliyotumika katika kutekeleza kazi ya usambazaji umeme katika eneo husika.



Awali, Kampuni hiyo ilitakiwa kujenga kituo kidogo cha kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji katika wilaya hiyo na baadaye kuwauzia wananchi umeme huo kwa bei elekezi ya serikali, jambo ambalo halikuweza kutekelezwa hadi sasa. Badala yake kampuni hiyo ilifanya kazi ya kusambaza umeme kama zinavyofanya kampuni zingine katika mradi wa usambazaji umeme vijijini katika maeneo mbalimbali nchi.



Ziara hiyo ilifanyika, Julai 4, 2020, ambapo Naibu Katibu Mkuu huyo aliambatana na Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Viongozi wengine kutoka Taasisi zilizochini ya wizara hiyo ikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Huduma za Nishati na Maji, (EWURA) ili kila mmoja aweze kuona namna ambavyo kampuni hiyo imetekeleza kazi zake kwa kiwango na kwa kuzingatia vigezo na ubora unayotakiwa.

Baada ya ziara hiyo, changamoto na dosari mbalimbali zilionekana katika kutekeleza mradi huo, hivyo Mhandisi Masanja aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO), kuwasilisha taarifa inayoeleza mchakato mzima wa utendaji kazi wa kampuni hiyo na namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana katika kazi.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, uongozi wa juu wa kampuni hiyo haukuweza kushiriki ziara hiyo licha ya kupewa taarifa juu ya ziara hiyo katika eneo lao la kazi, kutokana na sababu mbalimbali, hata hivyo walimuagiza mmoja wa wahandisi aliyejulikana kwa Jina la Chakuja ili kushiriki ziara hiyo, ambaye pia hakuweza kujibu baadhi ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa kwakuwa hakuwa na majibu.

“Hii ziara inafahamika na uongozi wa kampuni ya TEXPOL unafahamu na wamekuwa wakiwasiliana na Kamishna msaidizi, cha ajabu hawapo eneo la tukio ili tuweze kuwauliza maswali yetu na kupata majibu stahiki, badala yake wamemuagiza huyu kijana mhandisi ambaye hawezi kutupatia majawabu stahiki na hafahamu, TANESCO mtaleta taarifa ya maandishi Wizarani kwakuwa ninyi ndiyo mnawasimamia na mnawafahamu vyema,”alisema Mhandisi Masanja.

Vijiji vilivyounganishiwa umeme na kampuni hiyo katika kata hiyo ya Ilungu iliyopo Wilaya hiyo ya Uyole ni Mwela, Ifupa, Mashese, Nyalwela, Ngole pamoja na Shango, ambavyo vina Kaya zaidi ya mia tano, mia tatu kati ya hizo tayari zimeunganishiwa umeme, zikiwemo baadhi ya shule na vituo vya afya.

Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni ya TEXPOL, aliueleza ujumbe wa ziara hiyo kuwa bado kampuni hiyo ipo katika mchakato wa kujenga kituo kidogo cha kufua umeme kama ilivyoelezwa hapo awali, kinachosubiriwa sasa ni fedha walizoziomba kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambazo wanategemea kuzipata.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa REA, Mhandisi Jones Olotu, alimueleza mwakilishi huyo kuwa, kampuni hivyo haiwezi kupata fedha hizo kwa sababu haikuweza kukidhi vigezo vinavyotakiwa, vilivyoweka katika ushindani wa kuomba fedha hizo ikiwa pamoja na kushindwa kukamilisha kazi za awali.

Vilevile tayari kampuni hiyo imeandikiwa barua ya kufahamishwa juu ya kilichotokea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...