Charles James, Michuzi TV

KICHEKO! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana Rais Dk John Magufuli kusema kwamba atawaruhusu wateule wake ambao wataandika barua za kuomba ridhaa ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao hasa Ubunge.

Rais Magufuli ameitoa kauli hiyo jana Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya ambao amefanya teuzi zao hivi karibuni.

April 25 mwaka jana wakati akizungumza na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, Ikulu Chamwino, Rais Magufuli aliwaonya wateule wake wanaotaka kwenda kugombea kuwa hatowateua tena endapo watashindwa kwenye Ubunge.

Rais Magufuli alitumia mfano wa aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Monanzila ambaye aliacha u-RC na kwenda kugombea Ubunge na kukosa ambapo yeye aliamua kutomteua kwenye nafasi yoyote kwa sababu alionekana ni mtu mwenye tamaa.

Sasa kufuatia jana kutangaza kwamba atapokea ruhusa za wateule wake wanaotaka kwenda kugombea nafasi zingine, Michuzi Blog inafahamu kuwa wapo wateule kadhaa katika Mkoa wa Dodoma ambao wataachia nafasi zao na kwenda kugombea Ubunge maeneo mbalimbali nchini.

Wateule ambao mpaka sasa wanatajwa kwenda majimboni ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi ambaye anatajwa kwenda kugombea Jimbo la Chilonwa wilayani Chamwino, Dodoma.

DC Ndejembi aligombea katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2015 lakini alikosa nafasi Katika kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo Mbunge wa sasa, Joel Mwaka ndiye ambaye alipitishwa kugombea na chama hicho na kushinda.

Kwenye uchunguzi ambao Michuzi imeufanya unaonesha kuwa vita ya Ubunge kwenye Jimbo hilo ipo hasa kwa Ndejembi na Mwaka licha ya kwamba wapo wagombea wengine akiwemo mmoja wa watumishi Ofisi ya Rais-Tamisemi aliyejulikana kwa jina moja la Chaula.

" Kiukweli sisi tunafahamu Ndejembi ana nia ya kugombea Ubunge na anaweza kuja kuchukua fomu hapa kwetu, ni Kiongozi mzuri tunaona kazi zake wilaya jirani ya Kongwa, tunafahamu ana uwezo mzuri lakini nafikiri vikao vya chama ndio vitaamua nani ni nani," Kilisema chanzo chetu.

Ndejembi amekua Mkuu wa Wilaya ya Kongwa ambayo pia ni Jimbo la Spika Job Ndugai kwa miaka minne toka alipoteuliwa na Rais Magufuli Julai 7 mwaka 2016.

PATROBAS KATAMBI

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi ni mojawapo ya jina kubwa katika medani za siasa nchini hasa kwa vijana.

Wengi wanamkumbuka kwa harakati zake za kisiasa akiwa kama Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wana Chadema (BAVICHA) kabla ya kujiunga na CCM mwishoni mwaka 2017 na kisha kuteuliwa kuwa DC Dodoma Julai 2018.

Huyu ni miongoni mwa wateule wa Rais Magufuli ndani ya Mkoa wa Dodoma ambao wanatajwa pasipo na mashaka kwamba atarudi kugombea tena Ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini lakini safari hii akigombea kwa tiketi ya CCM tofauti na 2015 alipogombea akiwa Chadema na kushindwa na Mbunge wa sasa Steven Masele (CCM).

Inaelezwa kuwa DC Katambi amekua na nia ya kuwatumikia wananchi wa Shinyanga Mjini na kwamba dhamira yake ya kugombea Ubunge mwaka huu imezidi baada ya jana Rais Magufuli kuruhusu wateule wake wanaotaka kwenda majimboni.

" Bado Katambi ana nia ya kuja Shinyanga, kwa mwaka 2015 alikua na nguvu kubwa sana lakini sasa hii miaka mitano amekua akiwatumikia wananchi wa Dodoma kiasi kwamba haonani mara kwa mara na watu wa Shinyanga kwa sababu ya majukumu lakini hiyo haizuii yeye kushinda, Nafasi yake inaweza kuwepo kama wana-CCM wakimpa ridhaa ya kugombea," Kimetanabaisha chanzo chetu.

GODWIN KUNAMBI

Mmoja wa Wakurugenzi wa Halmashauri ambaye amekua maarufu nchini ni Godwin Kunambi ambaye ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma.

Kunambi amekua maarufu kutokana na namna ambavyo ameliongoza Jiji la Dodoma kwa muda mrefu sasa kuongoza kwa ukusanyaji wa mapato kulinganisha na majiji mengine makongwe.

Nia yake ya kugombea Ubunge inatajwa kuwepo pale pale na kitendo cha Rais kutoa ruhusa jana kinaweza kumuongezea ari zaidi ya kuelekea Jimboni.

Kunambi kama ilivyo kwa Ndejembi na Katambi nae aligombea ubunge katika Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro mwaka 2015 lakini alikosa nafasi hiyo mbele ya Mbunge wa sasa, Suzan Kiwanga kutoka Chadema.

Michuzi Blog inafahamu bado Kunambi amekua na nia ya kurudi tena kugombea Ubunge wa Jimbo la Mlimba na safari hii akijivunia zaidi mafanikio aliyoyapata ndani ya Jiji la Dodoma kama tiketi ya kuomba kuteuliwa na chama chake cha CCM kugombea Ubunge wa Jimbo hilo.

" Kwa kweli Kunambi ana dhamira ya kuwatumikia watu wa Mlimba bado, ushindani wake bado unaonekana ni nje ya Chama kwa maana ya Mbunge aliyepo, lakini kwa jinsi serikali ilivyofanya kazi kubwa kwa miaka mitano hii kama Kunambi atapitishwa na chama atakua mguu ndani kuwa Mbunge wa Mlimba," Kilisema chanzo chetu.

Kabla ya kauli ya Rais ya kuwaonya wateule wake mwaka jana idadi ya namba ya waliokua wanataka kugombea mkoani Dodoma ilikua ni kubwa ambapo hata Mkuu wa Mkoa, Dk Binilith Mahenge alikua akitajwa kurudi Jimboni Makete pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Chemba ambaye amekua akitajwa kugombea kati ya Jimbo la Rorya ama Bunda.

Kufuatia kauli ya Rais kuonesha yuko tayari kutoa kibali cha kugombea kwa wateule wake tutegemee kuwaona viongozi hao na wengine wakijichomoza kuanzia Julai 14-17 katika Ofisi za CCM kwenye maeneo yao kuchukua fomu za kugombea Ubunge.

Rais Dkt John Pombe Magufuli

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...