Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imesema itaendelea kuweka mazingira mazuri kwenye sekta ya Kilimo ili kuwavutia vijana wengi nchini kujikita kwenye kilimo na kuondoa fikra za kuajiriwa pekee.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde alipotembelea maonesho ya Nanenane na kuwakabidhi vyeti vijana waliomaliza mafunzo ya vitalu nyumba.

Naibu Waziri Mavunde amesema tayari serikali ilishafanya mazungumzo na wafanyabiashara wakubwa nchini ili waweze kununua mazao ya bidhaa zao kwa wakulima wa ndani na hasa vijana.

" Niwapongeze kwa kumaliza mafunzo haya na kutunukiwa vyeti, ni imani yangu kwamba mtayatumia mafunzo haya katika kujiendeleza nyie wenyewe na kubadilisha fikra zenu juu ya sekta ya kilimo.

Kupitia kilimo tu naamini tunaweza kupunguza tatizo la ajira mtaani kwani ndio sekta pekee ambayo inaweza kuchukua kundi kubwa la vijana na wote wakaendesha maisha yao kupitia kilimo," Amesema Mavunde.

Amesema serikali inaamini kilimo ndio uti wa mgongo katika kukuza uchumi wa Nchi na kuwataka vijana kukimbilia fursa ya kilimo hasa kile cha Zabibu jijini Dodoma ili kuweza kunufaika na soko la zao hilo.

" Mkoa wa Dodoma unalima zao la zabibu ambalo kwa hakika Zabibu inayopatikana Dodoma ni ya kipekee na haipatikani sehemu nyingine zaidi ya hapa, hivyo niwatake wataalamu wetu wa Halmashauri kubuni mbinu mbalimbali za kuhakikisha tunalinyanyua zao hili na kuteka soko lake," Amesema Mavunde.
 Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde akimkabidhi Cheti cha kumaliza mafunzo ya vitalu nyumba mmoja wa vijana waliohudhuria mafunzo hayo jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde akizungumza na vijana waliomaliza mafunzo ya vitalu nyumba ambao amewakabidhi vyeti leo kwenye maonesho ya Nanenane jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...