Charles James, Michuzi TV

SIKU moja baada ya pazia la uchukuaji fomu za Urais kufunguliwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) leo mgombea Urais was Chama cha Mapinduzi, Rais Dk John Magufuli amechukua fomu hiyo katika ofisi za tume hiyo Njedengwa jijini Dodoma.

Baada ya kuchukua fomu hiyo, Dk Magufuli alienda katika ofisi za Makao Makuu ya CCM White House na kuzungumza na viongozi, wanachama na wapenzi wa chama hicho ambao walijitokeza kumlaki.

Dk Magufuli ameongozana na mgombea mwenza wake ambaye ni Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai na viongozi wengine wa sekretarieti na Jumuiya za chama hicho.

Akizungumza na wanachama waliojitokeza kumlaki Dk Magufuli amesema amechukua fomu ya kugombea Urais kwa mara ya pili ili aweze kumalizia kazi ya kuwatumikia watanzania kwa miaka mingine mitano huku akisema kampeni za chama hicho zitazinduliwa jiji la Dodoma ambapo ndipo Makao Makuu ya Nchi.

Ameyataja mafanikio ambayo serikali yake imeyapata kuwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya zaidi ya 500, Shule za Msingi na Sekondari, umeme kila kijiji sambamba na ujenzi wa barabara za lami ambazo zimerahisisha huduma mbalimbali za kijamii.

Rais Magufuli amesema leo Tanzania imefikia uchumi wa kati baada ya kazi kubwa ambayo serikali yake imefanya kwa kuwabana mafisadi na kuzuia mali za Tanzania yakiwemo madini kusafirishwa kiholela kwenda nje ya nchi.

" Wakati tunashughulika na makinikia walisema hatutofanikiwa na tutashtakiwa lakini leo wote tumeona jinsi ambavyo tumefanikiwa na mabilionea wa kitanzania akina Laizer wanachimba na kupata madini tena makubwa ambayo yote yanakuza vipato vyao na uchumi wetu.

Ndugu zangu jinsi ambavyo mimi na Makamu wa Rais Mama Samia tulivyopambana kuboresha umeme vijijini ambapo vijiji 9,402 vimepata umeme ilihali wakati tunaingia mwaka 2015 ni vijiji 3,000 tu vilikua na umeme tukaona tuna kila sababu ya kuomba tena ridhaa ya kuwatumikia nyinyi watanzania," Amesema Dk Magufuli.

Amesema mafanikio yaliyopatikana nchini ni mengi na wala hayatoshi siku moja pekee huku akisema miaka mitano mingine itakua ni ya kazi zaidi bila kulala lengo likiwa kukuza zaidi uchumi wa Tanzania na kuwasogezea wananchi huduma zaidi.

" Wanasema nitapigiwa kura na Ndege, Madaraja na Vituo vya afya, mimi nasema asante sana maana wananipigia kampeni, tumenunua ndege 11 tena kwa hela  zetu cash hatujakopa na Leo tunaona matunda yake, tumejenga flyover ambazo tulizoea kuziona kwenye Runinga sasa zipo kwetu na tunazitumia.

Treni za Umeme siyo ndoto tena ujenzi wa Reli ya Kisasa unakaribia kukamilika ili treni hizo zipite, ndugu zangu kwa hayo yote nikasema mtu pekee wa kumalizia kazi iliyobaki ni mimi na Mama Samia na chama chetu cha Mapinduzi, " Amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amewataka wanachama wa chama hicho kutobweteka kujiona tayari CCM imeshashinda badala yake wazidi kupiga kazi ili kura walizonazo zisipungue.

Awali akimkaribisha Dk Magufuli, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema wako tayari kuwakabili wapinzania na kwamba wanaenda kwenye uchaguzi huu wakiwa wenye kujiamini kutokana na mafanikio ambayo yamepatikana kupitia kwake Rais Magufuli na serikali yake.

Amesema wao kama viongozi watafanya kampeni za kistarabu na kuwataka wanachama wa CCM kutolala badala yake wapige kampeni za Mtaa kwa Mtaa, Nyumba kwa Nyumba na kitanda kwa kitanda.

" Ndugu mgombea wetu utendaji wako mahiri wa kazi ndio unaotupa imani ya kwamba tutaibuka washindi katika uchaguzi huu, Jumuiya zetu tumeshazigaia majukumu na zitafanya kazi mchana na usiku kuhakikisha ushindi unapatikana wa kishindo," Amesema Dk Bashiru.
 Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais Dk John Magufuli akiwasilimia wanachama na wapenzi wa CCM waliojitokeza kumlaki leo Makao Makuu ya chama hicho White House jijini Dodoma baada ya kutoka kuchukua fomu ya Urais Katika ofisi za Tume ya Uchaguzi.
 Mgombea Urais wa CCM, Rais Dk John Magufuli akizungumza na viongozi, wanachama na wapenzi wa chama hicho katika makao makuu ya chama hicho jijini Dodoma baada ya kutoka kuchukua fomu ya Urais.
 Mgombea Urais wa CCM ambaye pia ni Rais Dk John Magufuli na Mgombea Mwenza ambaye ni Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan wakimkabidhi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma fomu za udhamini kwa ajili ya kuomba wadhamini wa kuwadhamini mkoani Dodoma.
 Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli akionesha kwa wanachama wa chama hicho fomu ya kugombea Urais ambayo ametoka kuichukua Tume ya Uchaguzi (NEC) leo jijini Dodoma.
 Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akizungumza wakati wa kumkaribisha mgombea wa Urais wa CCM, Dk John Magufuli leo alipotoka kuchukua fomu ya Urais leo jijini Dodoma.
 Spika wa Bunge, Job Ndugai akisimama kumshukuru Rais Magufuli ambaye amesema atashangaa kama Ndugai hatochaguliwa kuwa Spika tena kwa jinsi alivyofanya kazi kubwa ya kulisimamia Bunge.
 Wanachama wa CCM jijini Dodoma ambao wamejitokeza kwenye mapokezi ya mgombea wa Urais wa chama hicho kwenye ofisi za CCM Makao Makuu Dodoma.
 Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Mama Samia Suluhu Hassan akizungumza na wanachama wa chama hicho Makao makuu ya CCM Dodoma.
 Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, Mgombea Mwenza Mama Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally (wa kwanza kulia) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa kwanza kushoto) katika picha ya pamoja Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma.
  Baadhi ya viongozi kutoka Jumuiya za CCM wakiwa wenye furaha walipokua wakimsikiliza mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli Makao makuu ya chama hicho jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...