Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin P. Mhede (mwenye tai nyekundu) akiongea na Wajumbe wa Bodi, Menejimenti ya TRA pamoja na Waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kuwasilisha ritani za Kodi (e-filing) leo Jijini Arusha.

Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (kushoto) akielezea namna Mfumo wa Kuwasilisha Ritani za Kodi unavyofanya kazi mbele ya Wajumbe wa Bodi, Menejimenti ya TRA pamoja na Waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kuwasilisha ritani za Kodi (e-filing) leo Jijini Arusha.



Wajumbe wa Bodi, Menejimenti ya TRA pamoja na Waandishi wa habari wakifuatilia uzinduzi wa Mfumo wa Kuwasilisha ritani za Kodi (e-filing) leo Jijini Arusha.

………………………………………………………………..

Na Rachel Mkundai, Arusha

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzisha mfumo wa uwasilishaji wa ritani za kodi kwa njia ya kielektroniki (e-Filing System) ukiwa na lengo kurahisisha uwasilishaji wa ritani za kodi na kupunguza gharama kwa upande wa mlipakodi.

Akizindua mfumo huo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha Kamishna Mkuu wa TRA Dr. Edwin Mhede amesema mfumo huu mpya utaongeza tija katika usimamizi wa kodi na kuboresha uwasilishaji wa ritani ambapo mlipakodi ataweza kuwasilisha ritani za kodi na kupata hati ya madai kwa ajili ya kufanya malipo bila kutembelea ofisi za TRA.

“Hii itapelekea kuondoa adha ya upotevu wa muda na rasilimali, kwa kuwa mfumo unamuwezesha mlipakodi kuwasilisha ritani za kodi wakati wowote hata siku za jumamosi, jumapili au sikukuu,” amesema Kamishna Mkuu wa TRA Dr. Mhede.

Aidha, Kamishna Mkuu ameongeza kuwa mfumo huu pia unamwezesha mlipakodi kujua taarifa za ritani za kodi zinazotakiwa kuwasilishwa kwa kipindi husika na hivyo kuziwasilisha ndani ya muda stahiki na kuepuka faini ya kuchelewa kuwasilisha ritani hizo.

Kamishna Mkuu Dr. Mhede amesema mfumo huu umetengenezwa katika namna ambayo unakumbusha mlipakodi tarehe ya mwisho ya kuwasilisha ritani na kulipa kodi zake stahiki na hivyo kupunguza uwezekano wa kutozwa riba na adhabu zinazotokana na kuchelewa kuwasilisha ritani na kulipa kodi stahiki kwa wakati.

Hali kadhalika kwa mujibu wa Kmaishna Dr. Mhede mfumo ni kiungo cha kurahisisha mawasiliano baina ya mlipakodi, mkaguzi wa mahesabu na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika majukumu ya kisheria ya kuidhinisha ritani za kodi pamoja na kuomba muda wa ziada wa uwasilishaji wa ritani endapo itabidi kufanya hivyo jambo ambalo litapunguza vitendo vya udanganyifu wa kughushi mihuri ya wakaguzi wa mahesabu katika kuidhinisha ritani za walipakodi.

Akiongea kwa niaba ya washauri wa masuala ya kodi Mwakilishi wa kampuni ya ushauri wa kodi ya PWC Bi. Pamela Saleh amesema, kuzinduliwa kwa mfumo huu utasaidia kupunguza misongo ya mawazo kwa wawasilishaji wa ritani za kodi kwa kuwa utawawezesha kuwasilisha kwa wakati.

“Mfumo huu wa uwasilishaji ritani za kodi utakuwa mfumo mzuri kwa kuwa utatuondolea ‘stress’’yaani msongo wa mawazo kwa kuwa tutawasilisha ritani za kodi wakati wowote na kutuepusha na fani za kuchelewa,” amesema Bi. Saleh.

Pamoja na mfumo wa sasa wa uwasilishaji wa ritani za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa njia ya kielektroniki, mfumo huu mpya (e-Filing System) utahusisha ritani zifuatazo:- Ritani ya makadirio ya Kodi ya Mapato kwa watu binafsi; Ritani ya makadirio ya Kodi ya Mapato kwa Taasisi; Ritani ya Kodi ya Mapato kwa watu binafsi; Ritani ya Kodi ya Mapato kwa Taasisi; Ritani ya tozo ya Mafunzo na Maendeleo ya Ufundi Stadi (Skills Development Levy – SDL); na Ritani ya Kodi ya Zuio katika mapato ya waajiriwa (PAYE).

Hata hivyo, wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya uchimbaji wa madini, mafuta na gesi wataendelea kuwasilisha ritani zao za kodi ya mapato kwa njia ya kawaida (manual). Vilevile, ritani nyingine ambazo hazijatajwa hapo juu, zitaendelea kuwasilishwa kwa njia ya kawaida katika ofisi za TRA.

Mfumo huu wa uwasilishaji wa ritani za kodi kwa njia ya kielektroniki unaambatana na miongozo na mafunzo kwa walipakodi na wadau mbalimbali ili kujenga uwezo wa namna sahihi ya kutumia mfumo huu.

Mamlaka inawasihi walipakodi na wadau wengine kufuatilia kwa karibu miongozo itakayotolewa kwa njia mbalimbali za mawasiliano pamoja na kushiriki mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huu.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin P. Mhede (mwenye tai nyekundu) akiongea na Wajumbe wa Bodi, Menejimenti ya TRA pamoja na Waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kuwasilisha ritani za Kodi (e-filing) leo Jijini Arusha.

Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (kushoto) akielezea namna Mfumo wa Kuwasilisha Ritani za Kodi unavyofanya kazi mbele ya Wajumbe wa Bodi, Menejimenti ya TRA pamoja na Waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kuwasilisha ritani za Kodi (e-filing) leo Jijini Arusha.

Wajumbe wa Bodi, Menejimenti ya TRA pamoja na Waandishi wa habari wakifuatilia uzinduzi wa Mfumo wa Kuwasilisha ritani za Kodi (e-filing) leo Jijini Arusha. ​

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...