Wazazi nchini wameshauriwa kujenga utamaduni wa kuwakatia watoto wao  Bima ya elimu itakayo wahakikishia uhakika wa kupata elimu bora hata pale wazazi wanaposhindwa kutimiza wajibu huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ulemavu wa kudumu au kifo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa wateja wadogo na wa kati wa benki ya NBC Bw Mussa Mwinindaho alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya 16 ya Shule ya Msingi Tusiime  yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

“Bima ya Elimu itawawezesha wazazi kuwa na uhakika na elimu ya watoto wao kwa kuwa mtoto ataweza kusoma kwa kipindi chote cha masomo yake hadi atakapomaliza hata kama wazazi watapatwa na majanga yanayoweza kusababisha ulemavu wa kudumu au kifo.’’ Alisema.

Akitolea mfano wa bima ya elimu ya Educare inayotolewa na benki hiyo, Bw Mwinindaho alisema  kupitia huduma hiyo  mzazi humwekea akiba mtoto wake kidogo kidogo kwa ajili ya elimu kwa kiasi atakachopanga kwa mkataba wa muda kuanzia miaka saba hadi 18 ili kugharamia elimu ya mtoto wake.

“Bima hii ya elimu ni mpango ambao mzazi huweka akiba kila mwezi hivyo kuleta faraja moyoni kwamba endapo chochote kitatokea iwe ulemavu wa kudumu ama kifo kabla ya muda huo basi bima itagharamia elimu ya mtoto wake.’’ Alisema.

Aliongeza kuwa uwekezeji katika elimu ya mtoto ni jambo pekee katika kuhakikisha malengo ya kielimu ya mtoto yanatimia huku pia akitumia fursa hiyo  kuwahimiza wahitimu na wanafunzi kwa ujumla juu ya umuhimu wa elimu na nafasi ya elimu kwenye jamii.

“Elimu ni urithi pekee usio hamishika kwa mwanadamu. Na lengo kuu la elimu ni kuhakikisha kwamba mwanadamu anapata maendeleo endelevu maishani ili aweze kulinda na kudumisha utu wake na jamii inayomzunguka. Elimu huongeza upeo wa kufikiri kwa mwanadamu hivyo ni nyenzo  muhimu ya kutatua matatizo ya kijamii.” Alisema.

Alisema kwa kutambua  umuhimu wa elimu, mbali na bima ya Elimu pia benki hiyo inatoa mikopo binafsi kwa ajili ya kuwezesha wazazi kulipia ada za watoto wao kwa ajili ya maendeleo yao ya kielimu.

Aliupongeza uongozi wa shule hiyo kwa mchango wao katika ukuaji wa elimu nchini Tanzania.

Kwa upande wa Mkuu wa Shule hiyo Bw Laurent Gama aliipongeza benki ya NBC kuwa imekuwa kiungo muhimu katika utekelezaji wa azma ya serikali ya kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa elimu bora kwa ngazi zote za elimu nchini.

 

Alisema Benki hiyo imekuwa ikisaidia kukuza mitaji ya kiuwekezaji, kutoa elimu ya namna bora ya kupanga na kusimamia miradi ya maendeleo, na pia kutoa mikopo mbalimbali kwa wazazi ili kuwawezesha vyema kumudu gharama za elimu ya watoto wao.

"Kwetu sisi jumuiya ya Tusiime, tutauendeleza ushirikiano wetu na NBC ili kwa pamoja tuweze kuisaidia serikali yetu kutimiza azma yake ya kutoa elimu na malezi bora kwa vijana wa kitanzania katika mazingira yaliyo safi na salama.” Alisema.

 Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa wateja wadogo na wa kati wa benki ya NBC, Bw Mussa Mwindaho akipokea risala ya wanafunzi wanaohitimu darasa la Saba, Shule ya Msingi Tusiime katika mahafali ya 16 ya shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jiji Dar es Salaam.

 Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa wateja wadogo na wa kati wa benki ya NBC, Bw Mussa Mwindaho akisikiliza maelezo kutoka kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tusiime, alipotembelea banda lao kwenye mahafali ya 16 ya Shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.


 Mkurugenzi wa Shule za Tusiime Bw Albert Katagira akizungumza jambo kwenye Mahafali ya 16 ya Shule ya Msingi Tusiime yaliyofanyika mwishoni mwa wiki j jijini Dar es Salaam

 Wanafunzi wa Shule ya Msingi Tusiime wakitoa burudani kwa kucheza ngoma za asili wakati wa mahafali hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...