Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV


MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya siasa nchini John Shibuda ametoa mwito kwa wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwenye mikutano ya kampeni za wagombea wa vyama vyote vya siasa ili kusikiliza hoja na kisha kufanya maamuzi sahihi itakapofika Oktoba 28 mwaka huu ambayo ndio siku ya kupiga kura.

Shibuda ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akielezea hali ya kampeni za uchaguzi mkuu ambao unatarajia kufanyika siku hiyo ya Oktoba 28, ambapo ametumia nafasi hiyo kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.

Akifafanua zaidi kuhusu siku ya kupiga kura, Shibuda amesema ni vema wananchi wakaenda kusikiliza sera na hoja za wagombea wa vyama vyote na kisha watakuwa na maamuzi sahihi ya kutambua nani ana sifa za kuongoza nchi yetu.

"Siku ya kupiga kura mkapate nguvu ya kufanya uamuzi sahihi, wagombea wapo 15, nani ana sifa bora, nani ana weledi,nani ana elimu ya uraia kutekeleza yale ambayo Baba wa Taifa aliyaanzisha,"amesema Shibuda na kuongeza siku ya kupiga kura ni muhimu sana.

"Taifa letu lina majibu ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Watanzania tukumbuke historia inafundisha, uchaguzi mwaka 2015 tulidai mabadiliko, tulidai mageuzi hatukujua yana ladha chungu lakini kuna mafanikio ambayo yametendeka.

"Serikali ya Awamu ya Tano tunajua kuna mafanikio ambayo yamefanyika lakini CCM imejikosesha yenyewe kwa kutokuwa na mikutano ya hadhara.Hivyo nashauri baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu, kuwepo na utaratibu wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara,"amesema Shibuda.

Amefafanua wananchi kutopiga kura ni makosa, hivyo amewaomba wajitokeze kwani wasipojitokeza ni janga la Taifa."Uchaguzi ni ufunuo wa kuwatambua wanaopenda maslahi ya Taifa. Nendeni mkapige kura muamue nani anafaa kuwa kiongozi katika nchi yetu".

Amefafanua kama wapiga kura watapenda porojo na wakaogopa ladha chungu, watakwenda kupata wachumia tumbo na wasije kulalamika mirija ikirejea ya kunyonywa kwa Taifa letu na kwamba wakumbuke ukweli huchelewa kukomaa masikioni.

Amewataka wanasiasa wa vyama vyote na hasa wanaogombea kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais kuhakikisha wanakuwa na lugha ambazo zinaunganisha Taifa badala ya kusababisha uvunjifu wa amani iliyopo nchini pamoja na kujenga chuki miongoni wa jamii ya Watanzania.

"Wanasiasa na wagombea tengenezeni mashindano ya hoja kujenga ambazo zina maslahi kwa Taifa letu badala ya kuwa na siasa za uongo na uzushi ambazo madhara yake ni makubwa.

"Hizo ndio nasaha zangu kwa wagombea kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge na Urais ,ikumbwe uongo wa siasa huanda dhuluma dhidi ya vizazi na vizazi.Kwa hiyo wagombea wote wakumbuke ukweli una thawabu kwa Mwenyezi Mungu, ukweli huzaa haki dhidi ya dhuluma,"amesema Shibuda.

Amesisitiza kila chama cha siasa, kila mwanachama ajifanyie ukaguzi na kujitathimini ili kujitambua na kujiongeza na kujisahihisha kwa lengo la kufanya siasa safi.

"Wagombea upukeni kugeuza michakato ya kunadi sera kuwa mipango mikakati ya makusudi ya kutoleana lugha za kugombanisha na kuvuruga umoja wa jamii yetu ya watanzania."

Pia Shibuda amevitaka vyombo vya ulinzi nchini katika kipindi hiki cha kampeni na kuelekea uchaguzi mkuu kufanya kazi yao kwa weledi ili kuhakikisha nchi ibaki salama kabla na baada ya uchaguzi huo.

"Vyombo vya dola viwe na wajibu wa matendo kinga ya kulinda urithi wa tunu za taifa kwa ajili ya vizazi na vizazi.Nampongeza IGP Simon Sirro kwa kuhimiza kila mtu atimize wajibu wake ili kutekeleza ahadi ya Rais Dk.John Magufuli ya kufanyika kwa uchaguzi wa amani na haki,"amesema Shibuda.

 MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya siasa nchini John Shibuda akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar ,wakati akitoa mwito kwa wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwenye mikutano ya kampeni za wagombea wa vyama vyote vya siasa ili kusikiliza hoja na kisha kufanya maamuzi sahihi itakapofika Oktoba 28 mwaka huu ambayo ndio siku ya kupiga kura.

  MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya siasa nchini John Shibuda akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari leo jijini Dar alipokuwa akielezea hali ya kampeni za uchaguzi mkuu ambao unatarajia kufanyika siku hiyo ya Oktoba 28,Mwaka huu na ambapo ametumia nafasi hiyo kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoendelea nchini. Baadhi ya Wanahabari walioshiriki mkutano huo wakifuatilia yaliyokuwa yakielezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa nchini, John Shibuda.Picha na Michuzi JR-MMG.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...