Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga akizungumza na Wadau wa Utalii wanaotoa huduma za malazi kwa Wageni katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro  kabla ya kuanza kutolewa kwa  mafunzo ya usajili wa Wageni kwenye  mfumo wa MNRT PORTAL yanayofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia leo  mkoani Arusha.
Baadhi ya Wadau wa Utalii  kati ya  250 wanaotoa huduma za malazi kwa Wageni walioshiki kutoka katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro  wakifuatilia  mafunzo ya usajili  Wageni kwenye  mfumo wa MNRT PORTAL yanayoendelea kufanyika kwa siku mbili kuanzia leo mkoani Arusha.

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewatoa hofu Wamiliki wa Huduma za Malazi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuwa usajili wa Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL utakaoanza kutumika nchini kote Oktoba 1, 2020 umelenga kupata takwimu sahihi za Wageni zitakazosaidia katika  kuboresha sekta ya Utalii nchini na si vingunevyo.

Pia, Imesema Usajili huo  utalinda siri za Wageni  na  zitatumika kwa ajili ya matumizi ya Serikali pekee na sio  kwa maslahi binafsi.

Hayo yamesemwa leo Jijini Arusha na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga alipokuwa akihitimisha mafunzo yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili ya usajili   Wageni kwenye Mfumo wa  MNRT PORTAL  kwa Watoa Huduma za Malazi zaidi ya 250 wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

Amesema Usajili wa Wageni katika Mfumo huo utahusisha Wageni wa ndani pamoja na Wageni kutoka nje ya nchi ambapo lengo kuu ni kupata takwimu zitakazosaidia kuboresha sera, mikakati na mbinu za kukuza utalii nchini.

Amesema Usajili huo mbali ya kusaidia kujua idadi ya Watalii wa ndani bali utawasaidia hata Wamiliki wa malazi hayo kuweka rekodi ya  Wageni waliolala katika malazi yao kwa kipindi chote ambacho anafanya biashara hiyo ya malazi.

Chitaunga amesema katika sekta ya utalii mfumo huo umekuwa ukitumika sehemu nyingi Duniani kama vile Uingereza, Marekani na Kanada  na si kitu kipya kilichoanzishwa hapa nchini.

Pia amesema mfumo huo utasaidia kurahisisha kazi kwa Wamiliki wa malazi ambapo badala ya kubeba karatasi na kwenda katika ofisi za Wizara ya Maliasili na utalii kwa ajili ya kulipia leseni ataweza kutumia  kompyuta yake akiwa ofisini kwake  kufanya usajili huo.

Mkurugenzi huyo amesema mfumo huo utakaonza kutumiwa na Watoa Huduma za malazi nchini kote mwezi Oktoba 1, 2020 utahusisha hoteli, loji, nyumba za Wageni pamoja na mahema ya watalii.

Ametaja vitambulisho vitakavyotumika katika usajili huo kuwa ni Kitambulisho cha Taifa kwa wageni ambao ni Watanzania na Pasi ya kusafiria kwa Wageni wa kutoka nchi za nje.

Katika hatua nyingine, Chitaunga amesema kuanza kutumika kwa Mfumo huo ni utekelezaji wa takwa la kisheria linalomtaka kila Mmiliki wa Malazi kuanza kusajili Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL.

Mbali na hiyo, Chitaunga amesema matumizi ya mfumo huo utaifanya sekta ya Utalii kwenda katika  uchumi wa bluu utakaoiweka Tanzania katika mazigira bora ya kibiashara.

Naye Anne Sosteness ambaye ni miongoni mwa Wamiliki wa Malazi katika mkoa wa Arusha aliyeshiriki mafunzo hayo, Amesema mafunzo ni mazuri na ni salama kwa mteja na mtoa huduma kwa ssbabu Mteja anatakiwa kuonesha kitambulisho chaTaifa au pasi ya kusafiria ili aweze kusajiliwa.

Aidha, Amesema mfumo huo unapunguza matumizi ya karatasi ambayo ni rahisi kupotea na kuchanika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...