Wakulima waomba TARI kuanzisha vitalu vya miche ya korosho ngazi ya Wilaya, na Kata


Na Mwaandishi Wetu, Lindi


WAKULIMA wa korosho kutoka wilaya za Nachingwea, Liwale na Ruangwa wamekiomba kituo cha Utafiti wa Kilimo Nchini TARI Naliendele, kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche ya kisasa ya zao la korosho katika ngazi ya wilaya na kata ili kuwezesha wakulima kupata mbegu hizo kwa wakati mwafaka.


Wakizungumza katika kikao cha mafunzo ya ukuzaji bora wa zao la korosho kwa njia za kisasa yaliyoandaliwa na TARI Naliendele wakishirikiana na Bodi ya Korosho nchini (CBT), wakulima hao wamesema uwepo wa vitalu hivyo katika ngazi ya wilaya na kata utasaidia wakulima kupata miche ya kupanda kwa haraka na rahisi kutoka vitalu hivyo.


“Upatikanaji wa mbegu bora za korosho haswa kwa sisi wakulima wa vijiji vya ndani ndani huko sio rahisi, kuna urasimu sana katika kuzipata na tunatembea umbali mrefu mnoo kwenda kuzitafuta,” amesema mkulima wa korosho wilayani Nachingwea Rahisi Maula.


Amesema kuna haja ya serikali kupitia kituo cha TARI Naliendele kutengeneza mfumo huo uwe endelevu ambao utarahisisha upatikanaji wa mbegu kwa wakati kwa wakulima wa mikoa ya kusini na mikoa mingine ambao inajihusisha na kilimo cha zao la korosho nchini,” amesema na kuongeza


Amesema upatikanaji wa mbegu za korosho urashisishwe na kuwa kama upatikanaji wa mbegu zingine za mazao kama vile mahindi, ufuta , karanga na mazao mengine.


“Tunaomba serikali kupitia kituo chetu cha utafiti kulifikiria hilo na kutusaidia sisi wakulima si tu kupata mbegu za kupanda kwa haraka ila hata katika kujifunza kupitia vitalu hivyo mbinu za kisasa za kukuza zao na korosho ambazo zimebuniwa na kituo hicho,” amesema.


Afisa Kilimo Kata ya Ruangwa Mjini, Musa Maimula amesema kwamba hali ya upatikanaji wa mbegu za korosho sio nzuri huku akitaka serikali kulete mazingira wezeshe kwa kulete vitalu vya miche kwenye ngazi ya halmashauri ili kusaidia wakulima kupata mbegu bora kwa wakati.


“Hali ya upatikanaji wa mbegu za korosho kwa wakulima sio nzuri, sana, kuna urasimu katika upatikanaji, mkulima mpaka kuipata kuna uzito kwa maana ya kwamba umbalI, mpaka kufika Naliendele, mkulima anapata ugumu,” amesema.


Kwa Upande wake Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Ruangwa Idrisa Mkwawa amesema kila mwaka halmashauri huomba na kuletewa mbegu bora kutoka TARI Naliendele na kuzisambaza kwa wakulima vijijini na maeneo mengine wilayani humu.


“Kwa upande wa halmashauri yetu ya Ruangwa, kila mwaka huwa tuna ‘request’ mbegu na kuletewa, kwa mfano msimu uliopita tuli ‘order’ kilo 5000 nakuzipata  na kabla ya kuzisambaza kwa wakulima, tulizifanyia kazi na kupanda mbegu 400 kwenye shamba la halmashauri na zingine tukazisambaza kwa wakulima,” amesema na kuongeza kuwa kwa mwaka huu wameomba mbegu kilo 3000 ambazo watazisambaza kwa wakulima kwa msimu ujao.


Kituo Cha TARI Naliendele kimegundua na kusajili mbegu bora 54 za korosho kwa ajili ya matumizi kwa wakulima. Aina hizo zina uwezo mkubwa kuzaa korosho nyingi na bora na kuvumilia magonjwa na wadudu waharibifu.

 Mtafiti Upande wa wadudu waharibifu na Magonjwa ya mikorosho kutoka TARI Naliendele Dadili Majune (Mwenye shati ya Blue katikati) akitoa maelekezo kwa wakulima wa korosho kutoka Wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Liwale jinsi ya kudhibiti wadudu na magonjwa kwenye mikorosho.


 Mtafiti Msaidizi Mkuu daraja la Kwanza kutoka TARI Naliendele Stella Mafune akitoa maelekezo kuhusu matumizi sahihi ya mbegu Bora za korosho kwa wakulima kutoka Nachingwea, Liwale na Ruangwa Mkoani Lindi. 

Afisa Kilimo Msaidizi (Mwenye apron ya dark blue) kutoka TARI Naliendele Bashiru Libuburu akitoa maelezo kwa wakulima namna ya upandaji Bora wa miche kwa wakulima wa korosho Nachingwea, Liwale na Ruangwa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...