Viongozi wa Kamati ya Amani Mkoani Rukwa Wameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa utaratibu mzuri waliouweka katika vituo vya kupigia kura hali iliyopelekea kuondoa msongamano na wapiga kura kutimiza haki yao ya kikatiba bila ya bugudha wala kupoteza muda kwa kusimama kwenye foleni muda mrefu katika vituo hivyo.

Aidha, viongozi hao wametanguliza Shukrani zao kwa Mwenyezi  Mungu kwa kujalia hali ya utulivu na amani wakati wote wa kupiga kura na kuwashukuru Watanzania kwa kuzingatia maelekezo ya Tume katika muda wote wa zoezi hilo.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika alisema, “Tumeshuhudia katika vituo vyetu vya kupigia kura hali ikiwa shwari kabisa, na wapiga kura katika maeneo mengi nchini wameshuhudia kuwa kulikuwa na utengamano na utulivu mkubwa san ana tunawashukuru watanzania kwa kuzingatia maelekezo ya Tume mathalan, mara baada ya kupiga kura rudi nyumbani ili kupisha msongamano na karibu wote walifanya hivyo.”

Halikadhalika, Askofu Mwaipopo amewaomba watanzania kuendeleza utulivu wakati huu ambapo matokeo ya kura katika majimbo bado yanaendelea kutangazwa hadi pale wateule kwa nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani watakapokula nyapo zao.

“kikubwa ni kwamba baada ya haya matokeo kutangazwa, tuvunje makambi yetu ya kisiasa na kutoa ushirikiano kwa wale wote walioshinda na ikumbukwe kwamba, kwa nafasi ya Urais, iwe ama ulimchagua au la, ni Rais wako, vivyo hivyo kwa Wabunge na Madiwani, Ni uungwana na Uzalendo kwa Taifa letu kushikamana na kuwa wamoja kwaajili ya maslahi mapana ya nchi yetu,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa waanchi wa mkoa wa Rukwa kuendeleza utulivu akiamini kuwa wanarukwa hawawezi kudanganywa na watu ambao wanadhamira ya kuanzisha vurugu baada ya kushindwa na kuwasihi kujikita kwenye masuala ya kilimo baada ya kumaliza zoezi la kuwachagua viongozi wawapendao.

“Kuna watu ambao kula yao ipo huko, akichochea ndio anaenda kula lakini wewe usipokwenda kulima hutakula, kwahiyo wanachi wawapuuze, hasa vijana, wawapuuze watu wote ambao wanataka kutuletea vurugu, lakini pili niwaonye wale wote wanaotaka kujaribu kutuvuruga ndani ya Rukwa wasijaribu, vyombo vya ulinzi na usalama viko macho sana, tuko vizuri mno tumejipanga, yeyote atakayeleta vurugu tutamshughulikia ipasavyo, tena kwa ukamilifu,” Alisisitiza.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akimsalimia Mwenyekiti wa Kamati ya Amani  Mkoa wa Rukwa Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika. 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...