*Awataka wasifanye makosa kuchagua wapinzani, wamechelewa kimaendeleo

*Wenyewe wamwambia wamekosea ,wanamuomba msamaha...awajibu hana kinyongo 

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Hai

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amepokekelewa na maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambapo wamemhakikishia katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu hawatafanya makosa tena kwa kuchagua wapinzani kwa nafasi ya ubunge na madiwani.

Wananchi hao wamesema wanajuta kwa kumchagua Freeman Mbowe kuwa Mbunge wao kwani pamoja na changamoto nyingi ambazo zinawakabili ameshindwa kuwasemea na hivy kujikuta wakiwa katika wakati katika kupata utatuzi wa kero zinazowakabili.Wilaya hiyo ndiyo anayotoka Mbowe ambaye amekuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa muda mrefu.

Akizungumza na wananchi hao, Dk.Magufuli ambaye amefika kuwaomba kura  ili wamchague tena kwa ajili ya kuongoza nchini na kuendelea kuleta maendeleo , amesema amefurahi kwa makaribisho furahishwa makubwa ambayoa ameyapata Hai.

"Ndugu zangu wananchi wa Hai na Watanzania wengine wanaonisikiliza haya makaribisho kwangu ni Special.Sijawaji , sijawahi kukuta mkutano mkubwa na namna hii , sikutegemea kama nitakuta watu wengi hapa hivi nimebaki na deni kwenu.

"Nakumbuka nimekuwa nikija Hai , siku moja nilikuja kwenye barabara ya kwenda Sanya wakati huo nikiwa Waziri wa Ujenzi,, siku nyingine nikaja nikapita soko la Sadala, nikauliza hii halmashauri inaongozwa na Chama gani, nikaambiwa ni upinzani.Mliamua mliamua , hamjanikosea mimi ila mlizikosea nafsi zenu, sina kinyongo na ninyi, nawapenda kweli, na ndio maana na leo nimekuja tena kuomba kura zenu hapa.

" Lakini mahudhurio ya leo yamedhirisha wana Hai wana jambo lao Oktoba 28,  miaka mitano iliyopita nilikuja kuomba kura kwa unyenyekevu mkubwa kwasababu katika Ilani ninayoinadi ya kusara 303 inanifundisha ninapopea madaraka natakiwa  kuwatumikia watanzania wote na hicho ndicho nilichofanya,nilipoingia madarakani tulipanga kutoa elimu bure , hata kwa watoto wa hapa Hai waliendelea kusoma bure bila kulipa ada.

"Katika kudhihirisha hilo tumeendelea kutoa elimu bure kwa watanzania wote bila kubagua, mgombea mbunge wa CCM hapa Hai Saasisha Mafue amezungumza mengi mazuri yaliyofanyika kwa miaka mitano, tumeendelea kujenga vituo vya afya, kuimarisha hospitali, kuongeza bajeti ya afya kutoka Sh.bilioni 30 hadi Sh.bilioni 270.

Tumetoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, tumeendelea kupeleka umeme katika vijiji mbalimba na tayari vijiji 9700 nchini kote vikiwepo vya hapa vina umeme ingawa najua kuna baadhi ya vijiji hatujapeleka umeme na hapa vipo,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza ndio maana amefika kuomba kura ili akaendelee kupeleka umeme.

Dk.Magufuli amewakumbusha wananchi hao mwaka 2015 aliwaomba kura yeye walimpa lakini kwa nafasi ya ubunge na madiwani waliwapa upinzani."Mlinipa kura nyingi sana, kwenye ubunge mlichagua kutoka Chama kingine, mlinipa kazi kubwa, mlinebebesha mzigo mkubwa, mlinipa mtihani mkubwa, ilikuwa ni sawa ni kumfunga mtu miguu na mikono halafu unamwambia akachote maji, ilikuwa adhabu kwangu.

"Mbunge amliyemchagua kwa kuzingatia heshima ya Bunge letu alichaguliwa kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, akawa Msemaji wa kambi ya upinzani, Serikali ya CCM ikamtafutia gari ili ashiriki kwenye maendeleo ya kusaidia Bunge na nchi kwa ujumla.

"Ninyi watu wa Hai ni ninyi wa hai ni mashahidi, wakati naenda kufungua Bunge kwa mara ya kwanza mwaka 2015 mliona walichonifanyia,haikushia hapo hata tulipokuwa tunapanga bajeti za maendeleo mbunge wenu wa Hai na wabunge wengine wa upinzani wanatoka nje.Jiulize unahitaji dawa, vituo vya afya, barabara, kutatua kero, halafu mwakilishi wenu anatoka nje badala ya kuwasilisha kero,"amesema Dk.Magufuli.

Amesisitiza ndio maana anaeleza alikuwa anapata shida katika uongozi wake, alipata shida ya kuwahudumia kwani hakukua na kiunganishi kati ya wanannchi na Seriakli na kwamba ukiwa mbunge asiyehudhuria bungeni maana yake hawezi kuwalisha shida za wananchi.

"Mbowe ni rafiki yangu, nampenda sana, katika hili siungani naye, nimekuwa Mbunge kwa miaka 20 katika jimbo langu, kazi ya Mbunge ni kujenga mahusiano na Waziri ili kueleza shida zako, ikifika wakati wa bajeti unaomba kwa ajili ya watu wako, sasa bajeti ikija unapinga. Poleni sana wana Hai.

"Jimbo la Hai ni jimbo lenye kero nyingi, tulikuwa na kiwanda cha Kilimanjaro Mashine Tools, pale  hata wananchi kupata mashamba hadi wakodishiwe, kuna tatizo la maji hapa, tumefanikiwa kutoa maji Ziwa Victoria yamekwenda hadi Tabora.Arusha kuna mradi wa maji uliogharimu wa Sh.bilioni 620, Hai mbunge wenu hajawahi kuomba , nasema haya kwa uchungu,"amesema.

Dk.Magufuli amesema hata wakati wa janga la Corona dunia nzima ilikuwa katika hofu kubwa na watu wengi walipoteza maisha.Kama nilikuwa na wakati mgumu basi nikipindi kile, ndio ulikuwa wakati wa kuzungumzia bajeti ya nchi nzima."Ilikuwa ni jukumu la wabunge wetu wapitishe muswada wa kusaidia kukabiliana na Corona, kilichofuata mheshimiwa sana wa jimbo lenu na wenzake wakatoka nje, kwao maisha yao ni muhimu zaidi.

"Lengo ilikuwa ni kushawishi Bunge, kuishawishi Serikali kuwe na lockdown kwa maana ya kwamba watu wasifanye shughuli zao, tulikuwa tunaingia kwenye mtego na wakasema Bunge lazima lifungwe na wakasema wanatoka nje, badala ya kutoa ushauri wanatoka nje.Sina uhakika kama walivyotoka bungeni alikuja huku Hai,"amesema Dk.Magufuli.

Amesisitiza ndio maana aliamua  kumtanguliza Mungu na amewashukuru viongozi wa  dini, watanzania na wana Hai kwa kushiriki katika maombi ya kumuomba Mungu atuepushe na Corona na leo hakuna Corona."Mungu ametubeba, mataifa mengine yanahangaika na Corona.

"Pamoja na Corona haikuwepo nchini hawa hawa watu wakazunguka duniani kwenye vyombo vya dunia wanasema Tanzania watu wanakufa sana, wabunge wa CCM wakakaa bungeni wakapitisha na bajeti ya Uchaguzi Mkuu Sh.bilioni 330, baada ya muda nao wamekuja kuomba kura

"Ninachotaka kuwaeleza Hai, mjue mlikotoka, mlipo na mnakoelekea, maendeleo hayana Chama lakini lazima mchague viongozi wanatokana na CCM, kwa imani yangu mnaye kijana mzuri Saasisha, nawaambia wana Hai mkiniletea huyu Saasisha akasifishe matatizo ya wana Hai, safari hii Hai msiniangushe, wana Hai msiniangushe,makaribisho haya ya leo ni makubwa sana,"amesema Dk.Magufuli.

Hata hivyo amesema pamoja na kutochagua mbunge na madiwani wa CCM , waliendelea kuwahudumia licha ya kuwa na wakati mgumu kwani ilikuwa ngumu kujua wananchi wanahitaji nini na wana changamoto gani.

Amewaahidi wananchi hao kuwa ataendelea kushughulikia kero mbalimbali ambazo zinawakabili na kwamba anafahamu kuna changamoto ya uhaba wa maji kutokana na ubovu wa miundombinu, kuna mgogoro wa ardhi kati ya Kiwanja cha Kimataifa cha Kilimanjaro(KIA) na wananchi.

Anafahamu kuna ombi la ujenzi wa barabara za lami na yote hayo kwake yanawezekana kwani hakuna kinachoshindakana kwake,hivyo kazi ya wananchi ni kuchagua wagombea wa CCM walete maendeleo na kutatua kero zilizopo.

Dk.Magufuli amesema wamejipanga kutatua shida zao za muda mrefu, ndio maana wanaomba mwaka huu wasifanye makosa."Kwa mfano nafahamu pale kwa Sadala mnajitaji soko la kisasa kwa ajili ya ndizi, nileeteni Saasisha Mafue pamoja na madiwani, nitawaletea hilo soko, mnahitaji umeme wa REA nileta.Boma Ng'ombe kuna changamoto ya maji tutashughulikia".

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...