Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kondoa

RAIS John Magufuli amesema Tanzania imetengeneza historia nyingine baada ya kusaini mkataba kati yake na Kampuni ya Total ya nchini Ufaransa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta linaloanzia Hoima nchini Uganda kuja mkoani Tanga.

Dk.Magufuli ambaye pia ni Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) amesema hayo leo Oktoba 26,2020 alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa kampeni zake za urais akiwa mbele ya wananchi wa Kondoa na Chemba akitokea Babati mkoani Manyara.

Amewaambia wananchi hao kuwa bomba hilo ambalo litajengwa katika nchi hizo za Uganda na Tanzania litakuwa na umbali wa kilometa 1445 ambalo litakuwa likisafirisha mafuta ya moto na limepita mikoa mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Dodoma.

"Mkataba wa makubaliano hayo utasainiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadhi ya watendaji wa Serikali ili mradi uanze kufanya kazi.Wawekezaji wa nje sasa wameanza kuielewa Tanzania na kuanza kuja kuwekeza na Tanzania,"na kuongeza nchi imejipanga vizuri katika kutunza rasilimari za Watanzania pamoja na kuendelea kushirikiana na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema kuingiwa kwa makubaliano hayo kati ya Tanzania na Kampuni ya Total ya Ufaransa kunaonesha katika masuala ya kukubaliana na wawekezaji nchi yetu iko vizuri, hivyo ameomba wawekezaji wengine kuja kuwekeza na kwamba nchi inahitaji wawekezaji wa aina hiyo kwani fedha zinazokuja zinaenda katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya,elimu, maji, umeme, barabara, nakuboresha huduma za jamii.

Aidha amesema mitano inayokuja watafanya makubwa zaidi ya hayo huku akiwaomba wananchi hao wamchague awe Rais na wagombea wengine wa Chama chake kwani walichokifanya miaka mitano iliyopita ni cha mtoto na miaka mitano ijayo makubwa yanakwenda kufanyika.

Kuhusu changamoto ya maji katika maeeo ya Kondoa na Chemba na maeneo mengine nchini,Dk.Magufuli amesema atahakikisha anamteua Waziri wa Maji, Naibu Waziri wa Maji na watendaji wengine wa wizara hiyo watakaokuwa na uwezo mkubwa wa kutatua changamoto hiyo.

"Nitakapochaguliwa kuwa Rais ,nitahakikisha Waziri wa Maji anafanya kazi ya uhakika ya kuondoa shida ya maji, nataka Waziri ambaye atakuwa anafikiria nje ya boksi,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza "Kwa barabara ya Kondoa  imejaa madaraja kila mahali na madaraja hayo yanapitisha maji,tutayatumia kupata maji,"amesema.

Amefafanua mahali palipojengwa madaraja ya kutosha ili kupitisha maji kwanini pakose maji,hivyo anahitajika Waziri wa Maji ambaye atakuwa anaweza kufikiria zaidi kutafuta ufumbuzi wa shida hiyo ya maji."Pia tutatengeneza matuta makubwa ya kukinga maji wakati wa mvua na kisha yatavunwa ili kupunguza adha ya shida ya maji."

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...