WALIOONGOZA KITAIFA MATOKEO KIDATO CHA NNE WATAMANI UHANDISI (ENGEENERING)

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

WAHITIMU wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2020, matokeo yao yametangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) mwaka huu wa 2021 huku wengine wakiongoza kwa nafasi nzuri na kuingia kwenye Kumi Bora wakati huo baadhi ya Shule zikitangazwa kuongoza katika 10 Bora Kitaifa katika matokeo hayo.

Moja ya Habari kubwa kwa sasa ni yule Kijana aliyeshika nafasi ya kwanza Kitaifa ambaye ni Paul Cosmas Luziga aliyehitimu Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Panda Hill iliyopo Mbeya, sambamba na Binti Justina Gerald aliyeshika nafasi ya Pili na kuwa Mwanafunzi wa kwanza wa Kike Kitaifa katika Matokeo hayo aliyehitimu Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Canossa iliyopo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Media Group kupitia Michuzi Blog na Michuzi TV zilipata nafasi kuzungumza na Wahitimu hao wawili kwa nyakati tofauti, yaani Paul Cosmas aliyeshika nafasi ya kwanza na Justina Gerald aliyeshika nafasi ya Pili Kitaifa katika mazungumzo yao walieleza malengo yao makubwa kuwa Wahandisi (Engeeners).


Licha ya kuwepo kwa Taaluma nyingi za Udaktari, Ualimu, Sheria, Uhasibu, Ufamasia, Uandishi wa Habari na nyingine nyingi, Vijana hao wenye talanta za kipekee vichwani mwao, wote walichagua Taaluma ya Uhandisi.


PAUL LUZIGA NA MALENGO YA KUWA MHANDISI MAWASILIANO

Kupitia mahojiano hayo nyumbani kwao Goba jijini Dar es Salaam, Paul Lubiza amesema malengo yake kuwa Mhandisi Mawasiliano (Telecommunications Engeenering), Paul amesema anatamani kuwa Mhandisi kutokana na upendo wake wa Taaluma hiyo na upendo wa Masomo yanayotokana na Taaluma husika yaani (Physics, Chemistry, Mathematics).


Katika Mitihani yake ya mwisho ya Kidato cha Nne, Paul ameeleza kuwa hakutegemea kuongoza Kitaifa bali alitegemea kufaulu vizuri Mitihani hiyo iliyofanyika mwaka 2020.

Paul ameshauri Wanafunzi wa Kitanzania ili kufika malengo katika masomo yao watumie muda vizuri, kuzingatia Mtihani, akieleza kufanya hivyo ni kujiwekea mazingira mazuri ya kufanya vizuri katika masomo.

“Mimi kuwa wa kwanza Kitaifa ni jambo kubwa sana sikuwahi kutegemea kabisa, lakini nimeweza kama Binadamu wa kawaida, nawashauri Wanafunzi watunze muda vizuri wasipuuze Mitihani haswa Mitihani ya Taifa”, amesema Paul Luziga.

Paul ameeleza anaamini kufanya vizuri na kuwa na kiwango bora cha ufaulu tangu kuanza Kidato cha Kwanza hadi kufanya vizuri Mitihani ya mwisho ya Kidato cha nne mwaka 2020. “Naamini nilikuwa nafanya vizuri katika Mithani yangu ya Kidato cha Kwanza, Pili, Tatu hadi Mtihani wangu wa mwisho wa Kidato cha Nne.


JUSTINA NA MALENGO YA KUWA MHANDISI WA MAFUTA NA GESI.

Justina yeye katika Mahojiano yake na Michuzi TV nyumbani kwao Bunju jijini Dar es Salaam amesema anataka kuwa Mhandisi wa Mafuta na Gesi, amesema Taaluma hiyo ina jukwaa kubwa la maarifa kwa upande wake, amesema kwa nchi zinazoendelea (Developing Countries) Sekta ya Mafuta na Gesi ni tegemeo kubwa katika ukuaji wa Uchumi.


“Mitahani yangu ya mwisho niliomba sana Mungu nifanye vizuri, lakini sikufikiria sana kuwa wa Pili Kitaifa na kuongoza kundi la Wasichana waliohitimu Kidato cha Nne 2020”, ameeleza Justina.

“Nashukuru matokeo yangu ya Kidato cha Kwanza, Pili na Tatu sikuwahi kushuka ‘Top Five’ naamini nilifanya vizuri kila mtihani niliokutana nao”, amesema.

Katika matokeo yake ya Kidato cha Nne, Justina amesema amepata matokeo mazuri kutokana na ushirikiano mzuri baina ya Wanafunzi aliokuwa anasoma nao Shuleni hapo sambamba na kuwa na nia ya kufaulu mitihani hiyo ya mwisho.

Justina amewashauri Wanafunzi wengine kumtegemea Mungu na kumtanguliza katika kila kitu, pia kusikiliza ushauri na kuwa mwepesi kuchukua ushauri huo.

 Mwanfunzi Bora Kitaifa katika Matokeo ya Kidato cha Nne, Paul Cosmas Luziga akizungumza katika Mahojiano na Michuzi TV nyumbani kwao Goba jijini Dar es Salaam wakati akieleza siri ya mafanikio ya kuwa wa kwanza Kitaifa.

Mwanafunzi Bora wa Kike na aliyeshika nafasi ya Pili Kitaifa, Justina Gerald akizungumza katika mahojiano yake na Michuzi TV nyumbani kwao Bunju jijini Dar es Salaam.
Justina alimaliza Shule ya Sekondari ya Canossa iliyopo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...