Na.Catherine Sungura, Dar es Salaam

Serikali ipo tayari kuweka mazingira sahihi na ya kisera ili kuhakikisha watoto wenye magonjwa adimu wanapata haki sawa na kutoachwa nyuma katika kuwahudumia.

Hayo yamesemwa leo na
Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  wakati wa maadhimisho ya siku ya Magonjwa Adimu duniani yaliyofanyika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mama Samia amesema Serikali haijawaacha nyuma watoto hao na kwamba ina nia, dhamira na sababu ya kufanya mazingira wezeshi ya kuwahudumia kwani magonjwa hayo ni kama magonjwa mengine.

Ametoa wito kwa wazazi wenye watoto hao kutowaficha na hivyo kuongeza sauti ili kuweza kuwaamsha wengine kujitokeza, hiyo itaisaidia Serikali kubaini haja iliyopo na kuweza kutoa matibabu sawa.


Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima ameahidi Wizara hiyo ipo tayari kupokea maoni na mawazo kutoka kwa wadau na wazazi wenye uzoefu wa kuwahudumia watoto wenye magonjwa adimu na kuyaingiza kwenye mapitio ya Sera mpya ili iwe na sura inayotambua mapambano yanayotakiwa kufanywa Kwenye eneo hilo.

Dkt. Gwajima amesema wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau pamoja kutengeneza mpango kazi wa namna wa kuongeza kasi ya kuimarisha huduma za magonjwa adimu nchini ili kuleta usawa na usawia katika makundi yanayoathirika na magonjwa hayo ili wajisikie na wenyewe ni sehemu halali kabisa ya jamii na wanayopambana nayo kwamba yanawahusu wote.

Vilevile Dkt.Gwajima amesema wizara inakamilisha mpango mkakati wa huduma shufaa na utengamao utakaoongeza kasi na ubora wa huduma hizo kwani muelekeo wa sekta ya afya ni kuyapa malengo ya kipaumbele.

Hata hivyo wizara ya afya imepitia mpango mkakati wa sekta ya afya  wa kuzuia na kudhibiti Magonjwa yasiyo ambukiza ambapo magonjwa adimu yamewekewa malengo ya kipaumbele .

Naye, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amewapa pole na kuwapongeza wazazi wote nchini wenye watoto wanaougua magonjwa adimu.

Prof.Makubi amesema Serikali imefanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa hao na kuweka miundombinu na utayari wa nchi upo kwa kuyaweka kwenye mpango mkakati wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza Kama kipaumbele hata kama ni  machache ila haijalishi kwani changamoto wanazopitia wazazi ni kubwa na nyingi.Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni "Usawa wa Waishio na Magonjwa Adimu".

 

 Makamu wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ,Mama Samia Suluhu Hassan,



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...