Naibu Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza
na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Simiyu, wakati wa
ziara yake mkoani humo, Februari 25, 2021.
Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) mkoani Simiyu, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen
Byabato (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake mkoani
humo, Februari 25, 2021.
Na
Zuena Msuya Simiyu
NAIBU Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato
ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufanya vikao vya mara kwa mara na
wafanyakazi wa shirika hilo kwa kila Kitengo na Idara husika ili kusikiliza changamoto
zinazowakabili watumishi hao.
Wakili Byabato alisema hayo, wakati akizungumza na
wafanyakazi wa shirika hilo mkoani Simiyu Februari 25, 2021, wakati wa ziara
yake mkoani humo.
Alisema vikao hivyo vihusishe wafanyakazi wote bila
kujali viwango vya elimu na ngazi za madaraja walizonazo, ili kila mtumishi
aweze kueleza yanayomsibu sehemu za kazi pamoja na kueleza namna bora ya
kuboresha utendaji kazi wao.
Aliwaeleza kwamba vikao hivyo ndivyo vinavyowafanya
wafanyakazi kujiona wao ni sehemu ya familia ya shirika kwa kuwa wanapata muda
wa kukaa pamoja na kuzungumza na viongozi wao.
Aidha alitaka watumishi hao kupewa nafasi ya kutoa
maoni au mapendekezo yao ya nini kifanyike ili kuboresha utendaji kazi wao
pamoja na shirika kwa jumla na maoni hayo yasikilizwe na kufanyiwa kazi.
“Mfanyakazi hutumia muda mwingi wa maisha yake
sehemu ya kazi, eneo hili ni muhimu sana kwa kuwa wote hujiona ni familia moja
licha ya kila mmoja kutekeleza majukumu yake, hivyo ni muhimu viongozi wa eneo
husika kuweka utaratibu kuwa na vikao vya pamoja ili waweze kueleza changamoto
zao, na zifanyiwe kazi kwa wakati sahihi, hii inaongeza morali ya kufanya kazi
muda wote kwa kasi, ubunifu na usahihi, na katika vikao hivyo mara nyingi hupatikana
mawazo chanya ya kujenga na kuimarisha zaidi ubora wa shirika”, alisema Wakili
Byabato.
Katika hatua nyingine aliwaonya watumishi hao kufika
kazini wakiwa wamelewa ama kunya pombe muda wa kazi, na atakayebainika kuwa na tabia
hiyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria za kazi.
Hata hivyo alipongeza wafanyakazi wa shirika hilo
mkoani humo kuwa wamekuwa wakifanya kazi zao kwa umakini na kutoa huduma nzuri
kwa wateja licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili za kukatika umeme mara
kwa mara mkoani humo.
Aidha aliwaeleza kuwa waendelee kuwa wavumilivu kwakuwa muda si mrefu changamoto hiyo
itatuliwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Imalilo.
Kituo hicho kitakuwa na uwezo kuzalisha umeme wa Megawati
90 itakayokuwa ikitumika katika mkoa huo na mikoa jirani, mahitaji ya umeme kwa
Simiyu kwa sasa ni Megawati 10 tu.
Mkoa wa Simiyu unapokea umeme kutoka mkoani
shinyanga na hivyo kuufanya umeme huo kuwa na nguvu ndogo kuhimili matumizi
halisi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...