Aina mbalimbali za uyoga unaopatikana katika kijiji cha Amanimakoro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma

Diwani wa Kata ya Amanimakoro wilayani Mbinga Ambrosi Nchimbi akielezea namna wanawake katika kata yake wanavyofaidika na program ya kuongeza thamani mazao ya misitu
Mama Hilda Joseph mkazi wa kijiji cha Amanimakoro wilayani Mbinga akionesha aina mbalimbali za uyoga wa porini ambazo wanauza na kuongeza kipato

 

Baadhi ya wanawake katika kijiji cha Amanimakoro wilayani Mbinga wakiwa kwenye msitu wanafanyakazi ya kuokota uyoga kwa ajili ya lishe na kuongeza kipato.

 

PROGRAM ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu (FORVAC katika Mkoa  wa Ruvuma inafanyakazi kwenye wilaya tano ambazo ni Songea,Mbinga,Nyasa,Namtumbo na Tunduru.

Moja ya maeneo ambayo FORVAC inatekeleza miradi yake ni katika Kata ya Amanimakoro Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambapo  FORVAC inawezesha mwananchi mmoja mmoja na vikundi kuongeza thamani mazao ya misitu.

Mratibu wa FORVAC Mkoa wa Ruvuma Marcel Mtunda anasema  katika mwaka huu wa fedha wanatarajia kutoa shilingi milioni 100 kwenye  vikundi vya vijiji saba vilivyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

Anasema fedha hizo zitaviwezesha vikundi hivyo kutengeneza mizinga ya nyuki,vifaa vya kulinia asali,vifaa vya kutengenezea vikapu na kuwawezesha akinamama wanaookota uyoga kuwa na mitambo ya kuchakata uyoga ili uweze kupatikana hata baada ya kipindi cha mvua.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Amanimakoro Ambrosi Nchimbi anasema kata yake imebahatika kuwa miongoni mwa kata ambazo zipo kwenye mradi wa kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu(FORVAC).

Anasema katika kata yake kuna vijiji viwili  vya Amanimakoro na Kiwumbi ambavyo vinashiriki kwenye mradi huo ambapo vijiji vyote vinatekeleza mradi huo kwa kutumia mlima wa Liyuni.

“Mipango ya matumizi bora ya ardhi imeshafanyika katika vijiji husika,mafunzo ya Kamati za Maliasili yamefanyika,lakini pia biashara ya mazao ya misitu imefanyika ambapo kuna akina mama wameandaliwa kwa ajili ya mradi wa kukusanya uyoga kwenye misitu”anasema Nchimbi.

Hata hivyo anasema  kabla ya mradi huo uyoga ukiwa porini ulikuwa unaoza na kutotumika ipasavyo hivyo kupitia mradi huo wananchi watanufaika na uyoga kwa kupata lishe na kuongeza kipato baada ya kuuza uyoga.

Nchimbi anasema FORVAC imekusudia kusaidia mradi wa mashine za kukaushia uyoga ambao utawezesha uyoga ukiwa mbichi uweze kukaushwa na kuhifadhiwa hatimaye kutumika wakati wa kiangazi ambapo uyoga unakuwa haupatikani.

Kwa mujibu wa Diwani huyo,katika kata yake kuna vikundi vya wafugaji wa nyuki ambavyo vimeanza kuchonga mizinga na kuhifadhi kwenye misitu ili kufuga nyuki na kupata asali hivyo kuinua uchumi wao.

Mmoja wa wanufaika wa mradi wa uyoga katika kijiji cha Amanimakoro Grace Hyera anasema mradi wa kuokota uyoga unamwezesha kupata lishe na kuuza uyoga hivyo kupata mahitaji mbalimbali ya familia.

Hata hivyo anasema upatikanaji wa uyoga unategemea na eneo ambalo unakwenda kutafuta kwenye msitu ambapo anasema kuna baadhi ya maeneo huota aina mbalimbali za uyoga.

Anazitaja aina za uyoga unaopatikana katika eneo hilo kuwa ni ulelema, Ulundi, uinda, ngaukau, ungala, unodo, kisanga, ukufu,mndyelesa,lukolombi na aina nyingine nyingi za uyoga.

“Tangu mdogo  nilikuwa nakwenda na mama yangu porini ambaye alikuwa ananielekeza aina zote za uyoga unaofaa kuliwa  na uyoga ambao ni sumu’’,anasema Hyera.

Hata hivyo anasema kwa siku moja anaweza kuokota uyoga na kujaza vikapu vitatu na kwamba anapochemsha uyoga unapungua na anapoanika uyoga huo unapungua zaidi  na kupata kilo moja ambayo anauza shilingi 10,000.

Mary Kapinga ni mmoja wa akinamama wanaookota uyoga katika kijiji cha Amanimakoro,anazitaja baadhi ya  changamoto ambazo wanakutana nazo kuwa  ni kuharibika kwa uyoga inapotekea mvua nyingi hali inayosababisha kukosekana jua la kutosha kukaushia uyoga.

Anasema watakapopata mashine za kukaushia uyoga kama walivyoahidiwa na FORVAC utakuwa ni  msaada mkubwa katika kazi yao ya ujasirimali.

Kwa upande wake Hilda Joseph anasema awali alikuwa hafahamu faida za uyoga licha ya kutumia kama kitoweo hivyo anasema elimu waliopewa na FORAV kuhusu uchumaji uyoga endelevu imewasaidia sana ambapo hivi sasa wanauza na kupata kipato.

“Kupitia uyoga tunapata pesa ambazo zinawapeleka watoto shuleni,tunapata pesa za kukidhi mahitaji mbalimbali kama chakula na kununua pembejeo za kilimo’’,anasema.

Hata hivyo anatoa rai kwa FORVAC kuwapatia mbegu ambazo zitawawezesha kupanda uyoga majira ya kiangazi ili muda wote wawe na soko la uyoga.

Akizungumzia changamoto ya nyoka kwenye uyoga,Hilda anasema nyoka anapenda sana kula uyoga ambapo huwa anajiviriga kwenye uyoga mkubwa na kwamba wakati fulani inawalazimu kukimbia na kuacha uyoga kwa sababu nyoka chakula chake kikuu ni uyoga.

Anasema wanaanza kuchuma uyoga kuanzia Desemba hadi Aprili kila mwaka  ambapo anasema uyoga wa kuliwa unajulikana na uyoga wa sumu pia unajulikana.

Anazitaja sifa za  uyoga unaoliwa kuwa ni uwepo wa  wadudu,unanukia  na nyoka wanapenda uyoga wa aina hiyo ukilinganisha na uyoga wenye sumu.

Jackson Boimanda ni Mshauri wa Biashara wa FORVAC Halmashauri ya Mbinga anasema mafunzo ambayo hadi sasa wameyatoa kwa akinamama hao yamewasaidia kuwajengea uwezo katika biashara ya uyoga.

Anasema FORVAC tayari imeandaa bajeti ya kuwanunuliwa akinamama hao vitendeakazi ikiwemo mabuti,epuloni,mashine za kukausha uyoga na vifaa vingine walivyoviomba ili waweze kufanyakazi ya kuokota uyoga kwa ufanisi na tija.

“Moja ya majukumu yangu ni kuwaunganisha akinamama hawa na masoko,hivyo tunawatafutia masoko ili waweze kuuza kile wanachokizalisha,kuna Taasisi ambazo zipo tayari kutoa mafunzo na kununua uyoga wakiwemo WWF ambao wanahitaji tani nyingi za uyoga’’,anasema.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Amanimakoro Moses Nyoni anasema wananchi wanapata faida kubwa kutokana na mradi wa FORVAC ikiwemo kupata lishe na kipato.

Anaishauri FORVAC kuongeza bajeti katika program ya kuongeza thamani mazao ya misitu ili wananchi wengi waweze kunufaika kupitia mradi huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...