Na Mzee wa Atikali ✍️ ✍️✍️

"April 12, 1984 ilikuwa ni siku mbaya sana kwa Taifa la Tanzania. Ni siku ambayo hatutaisahau kwani siku hiyo tulimpoteza Kiongozi wetu tuliyempenda sana aliyekuwa Waziri Mkuu, Mh. Edward Sokoine. Mh. Sokoine alifariki kutokana  na ajali mbaya ya gari iliyotokea eneo la Wami- Dakawa".

ATILIO TAGALILE, April 11, 2011 (The Citizen, Tafsiri yangu.)

1. Usuli

Jumatatu ya leo, April 12, 2021, Taifa letu linatimiza miaka 37 toka marehemu EDWARD MORINGE SOKOINE, mmoja wa viongozi  bora kabisa kuwahi kutokea nchini, afariki kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984 eneo la Dakawa, wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

 Miaka 37, kwa umri wa mwanadamu, ni mingi sana. Hivyo, kuna baadhi ya "Bongolanderz" , hasa wa "Dot.com generation", ambao hawamjui kabisa na wengine wanamjua kijuujuu tu marehemu SOKOINE ndio maana mwandishi Bi HELLEN MATABA, alilibaini ombwe hili na kulielezea hapo Aprili 11, 2011-:

Today, 27 years after his tragic death, majority of Tanzanians aged below 27 years might not know who this man called Edward Sokoine was to Tanzania".

Hivyo basi, " MZEE WA ATIKALI" amewiwa kuziba ombwe hili kwa kumuelezea Mzalendo huyu wa kipekee kabisa toka siku anazaliwa hadi anafariki.

2. SOKOINE Azaliwa

Jumatatu ya Agosti 1, 1938, katika kitongoji cha Kilasho, kijiji cha Emairete, Monduli Juu, Arusha, huku mvua kubwa ikirindima, alizaliwa mtoto wa kiume. Mtoto huyo alikuja kuitwa EDWARD MORINGE SOKOINE ambapo baba yake aliitwa SOKOINE OLE SEVERE na mama yake aliitwa NAPELEL SINYATI NOOMAYAKI.

3. Elimu

3.1 Elimu ya Msingi

SOKOINE alisoma Shule ya Msingi Monduli kuanzia mwaka 1949 hadi 1953 na kisha akajiunga na "Monduli Middle School" toka mwaka 1953 hadi 1956.

3.2 Elimu ya Sekondari

 SOKOINE alifaulu mitihani yake hivyo mwaka 1956 alijiunga na shule ya sekondari ya Umbwe.

4. SOKOINE Ajiunga na TANU

Januari 1 1961,SOKOINE alijiunga na chama cha "Tanganyika African National Union" (TANU), ikiwa ni miezi michache kabla ya Tanganyika haijapata uhuru.

5. SOKOINE Aenda Masomoni

Mwaka 1962, SOKOINE alienda Ujerumani Magharibi kusomea mambo ya utawala na kurejea mwaka 1963.

6. SOKOINE Awa DEO

Baada ya kurejea toka Ulaya, SOKOINE alipangiwa kazi kama "District Executive Officer" (DEO) wa Maasai.

7. SOKOINE Agombea Ubunge

Septemba 30, 1965, SOKOINE, akiwa kijana mdogo tu wa miaka 27 lakini mwenye akili na ubunifu mkubwa, aligombea na kushinda ubunge jimbo la Masai. Mpinzani wake alikuwa Bw. EDWARD CARLO BONIFACE OLE MBARNOTE aliyekuwa Chifu wa Wamasai.

SOKOINE aliibuka mshindi baada ya kuhomola kura 6,977 wakati mpinzani wake, Chifu MBARNOTE aliduchua kwa kura 871.

8. Mh. SOKOINE Atema Cheche

Baada tu ya kuapishwa bungeni, Mh. SOKOINE alianza kutema cheche ambapo maswali yake ya kwanza yalikuwa-:

8.1 "Kwanini Wamasai wa Ngorongoro wanazuiwa kulima, wakati hawana mifugo ya kuwapatia chakula?"

8.2 "Kwakuwa tangu kuanza kwa Taifa hili, kuna makabila yamepata maendeleo sana na mengine yapo nyuma sana, je serikali ina mpango gani wa kuwaelimisha walioko nyuma kimaendeleo ili wawe sawa na wenzao?"

9. Mh. SOKOINE Aukwaa Uwaziri Mdogo

Mwaka 1967, Mh.SOKOINE aliteuliwa na Rais NYERERE kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano, Usafirishaji na Kazi.

10. Mh. SOKOINE Awa Waziri wa Nchi

Mwaka 1970, Rais NYERERE Alimteua Mh. SOKOINE kuwa Waziri wa Nchi. 

11. Mh. SOKOINE Akonga Nyoyo

Mh. SOKOINE alijulikana kwa uchapakazi wake toka akiwa Naibu Waziri. Hivyobasi, haikushangaza katika kikao nyeti cha NEC ya TANU, 1971, Mh. SOKOINE alipokonga nyoyo za wajumbe kwa hotuba kuntu kuhusu nchi kujilinda.

12. KINGUNGE "Amfagilia" Mh. SOKOINE

Baada ya hotuba hiyo mujarab, Rais NYERERE alimwita chemba, Mh. KINGUNGE NGOMBARE MWIRU na kumtaka maoni yake amwonavyo Mh. SOKOINE. Mh. KINGUNGE akamsifia sana, kama Prof ISSA SHIVJI aelezevyo katika kitabu cha "A Biography of Julius Nyerere" Mh. KINGUNGE alivyojibu-:

"Sokoine's speech was brilliant".

13. Rais NYERERE Amteua Mh SOKOINE Kuwa Waziri

Mwaka 1972, Rais NYERERE akamteua Mh. SOKOINE kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

14. Mh. SOKOINE Awa Mjumbe wa CC

Baada ya CCM kuzaliwa kutokana na TANU na ASP kuungana Februari 5, 1977, Mh. SOKOINE akawa mjumbe  wa Kamati Kuu ya CCM.

15. Mh. SOKOINE Ateuliwa kuwa "PM"

Februari 13, 1977, kutokana na utendaji kazi wake makini, Rais NYERERE alimteua Mh. SOKOINE kuwa Waziri Mkuu.

16. Mh. SOKOINE na Vita ya Kagera

Mh. SOKOINE alikuwa kiungo muhimu kwenye vita ya Kagera 1979. Kabla ya vita kuanza, SOKOINE aliwaagiza RCs wote wakusanye nyenzo zote tayari kwa kumtandika Nduli. Januari 23, 1979, alitembelea Mutukura.  Hatimaye, TZ ikashinda vita hiyo. Mh. SOKOINE alikuwa halali usingizi wakati wa vita, hali iliyopelekea afya yake kutetereka; kama "Wikipedia" inavyoeleza-:

"Sokoine had gone many days without sleep during the conflict and was left in ill health by its end."

17. Mh. SOKOINE Aomba Kujiuzulu

Novemba, 1980, Mh. SOKOINE aliomba na kukubaliwa kujiuzulu u-Waziri Mkuu na akaenda Yugoslavia kwenye matibabu na nafasi yake ikashikwa na Mh. CLEOPA DAVID MSUYA. Prof ISSA SHIVJI anatanabaisha-:

"Sokoine requested Nyerere to be relieved of his post because of his illlness; he suffered from severe diabetes. Sokoine went to Yugoslavia for treatment"

Mh. PIUS MSEKWA alieleza  kuwa Mh. CD MSUYA alikuwa "anamshikia tu" Mh. SOKOINE  cheo hicho-:

"Sokoine returned from Yugoslavia in 1983 having fully recovered from the disease that was troubling him. That was the time when President Nyerere reappointed him Prime Minister  to replace Msuya who, apparently, had been "housewarming" that position in Sokoine's absence".

Prof ISSA SHIVJI nae alieleza vivyo hivyo-:

"In hindsight, it appears as if Msuya's premiership was a holding operation:

Baada ya kurejea, Rais NYERERE alimteua tena Mh. SOKOINE kuwa Waziri Mkuu  Februari 24, 1983. Aidha, mwaka huo wa 1983, Mh. SOKOINE alianza kusomea shahada ya "Political Science".

18. Mh. SOKOINE: Muasisi wa Daladala

Mh. SOKOINE alikuwa ni mtu wa kutafuta majawabu ya matatizo ya wananchi. Alipoona UDA "inambwelambwela" akaasisi utaratibu wa daladala.

Prof. ISSA SHIVJI anafafanua-:

"Sokoine allowed private mini-bus operators to provide transport in Dar es Salaam under licence from the state bus company, UDA. Mini-buses came to be called "Daladala" because the newly minted five-shilling coin was the fare, and it happened to be the exchange rate of a US dollar. "Daladala" is one of Sokoine's lasting legacies".

19. SOKOINE & Uhujumu Uchumi

Aprili 5, 1983, Rais NYERERE alizindua kampeni kabambe ya kupambana na wahujumu uchumi baada ya kupitishwa kwa Sheria ya "The Economic Sabotage Act No. 9 of 1983" . Kampeni hii iliendeshwa na kusimamiwa na SOKOINE.

Sheria hii ilimtaka mtu aeleze mali aliyokutwa nayo aliipata wapi. Zilianzishwa Mahakamani Maalum na Mawakili hawakuruhusiwa kuingia, watu walitakiwa wajitetee wenyewe (Rais NYERERE aliona wahalifu wangeweza kutumia ujuzi wa mawakili kuachiwa). Katika zoezi hili, watu walimuogopa sana SOKOINE kwani sehemu nyingi nchini hasa Dsm mf Oysterbay & Upanga walitupa barabarani na mitaroni vitu vya thamani vilivyokuwa vimeingizwa nchini kinyemela mf TVs, na pia walitupa mabunda ya fedha na wapita njia  waliogopa kuviokota vitu na fedha hizo kwa kumuogopa SOKOINE hivyo polisi walikuwa wakiziokota fedha hizo na kuzipeleka BOT!. Vita hii ilimjenga sana SOKOINE kisiasa na akapendwa nchini kote.

Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kutokana na jinsi zoezi hilo lilivyoendeshwa yaliyopelekea Mh. SALIMN AMOUR, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, aombe radhi-:

"Mistakes were made during the campaign but it was not the intention of the government to victimise anybody. Those who were unfortunately involved should forgive the nation as the move was aimed at improving the situation".

Baada ya kifo cha SOKOINE, Sheria hii ilifutwa na ikatungwa "The Economic & Organized Crimes Control Act, 1984" ambapo mambo mbalimbali, mf uwepo wa mawakili, yalirekebishwa.

20. Mh. SOKOINE Ahudhuria Bunge

Mh. SOKOINE alihudhuria kikao cha bunge jijini Idodomia mwezi April 1984. 

Jumatatu ya tarehe April 9, 1984, Mh. SOKOINE alikwenda kusali kanisa la Mtakatifu PAUL, Idodomia. Usiku wa Jumanne, tarehe April 10, 1984, Mh. SOKIONE aliandaa karamu ya chakula cha jioni kwa Mawaziri na Wakuu wa Mikoa ambapo alionekana kuongea na kila Waziri na kila Mkuu wa Mkoa. Jumatano, tarehe  April 11, 1984, aliandaa chakula cha jioni kwa Wabunge wote wa mkoani kwake Arusha ambapo aliwasihi wafanye jitihada kuwaondoa wananchi wao kwenye lindi kubwa la ufukara.

21. Mh. SOKOINE Aliasa Bunge

Mh. SOKOINE, siku ya Jumatano ya tarehe April 11, 1984, akilivunja Bunge, aliasa kwa uchungu:

"Ndugu Spika, ningependa kumalizia kwa kukubaliana na wabunge wote waliosema na ambao hawakusema lakini wana mawazo haya kwamba jambo hili la kutumia fedha bila idhini ya bunge lazima tutafute kila njia ya kulikomesha".

22. SOKOINE Apangiwa Ndege, Agoma

Mh. SOKOINE alipangiwa kusafiri kwa ndege lakini akaamua kusafiri kwa njia ya barabara na sababu ya kufanya hivyo aliiainisha bungeni-:

".... Mungu akipenda tutakutana tena kwenye kikao kijacho cha  bunge. Mimi nasafiri kwa njia ya barabara ili nijionee hali ya mazao ya wakulima...".

23. Mh. SOKOINE Aanza Safari

Mapema Alhamis, tarehe  April 12, 1984, Mh.  SOKOINE aliondoka na msafara wake Idodomia saa 4.30 asubuhi akiwa ndani ya Mercedes Benz ambapo msafara huo uliongozwa na msafara wa polisi. Magari yote yaliyokuwa yakikutana na msafara huo yalikuwa yakipaki pembeni kuupisha msafara huo.

24. Gari la Mh. SOKOINE Lilikuwa Kwenye Mwendo wa Kasi!

Msafara wa SOKOINE ulikuwa na mwendo wa kasi; kama "Minutes" za CC ya CCM ya April 17, 1984 zinavyoeleza-:

"... Msafara wa Sokoine uliondoka Dodoma majira ya saa nne na nusu asubuhi na ulikuwa ukienda kwa spidi  ya kilomita 154 kwa saa".

Baada ya gari hilo kufika eneo la Dakawa, ghafla kilisikika kishindo kikubwa. Gari la Mh. SOKOINE lilikuwa limegongana na gari aina ya Toyota Land cruiser lililokuwa likiendeshwa na Bw. DUMISAN DUBE (23), mpigania uhuru wa chama cha ANC, aliyekuwa akiishi Mazimbu, Morogoro. 

Bw. DUBE, licha ya kusimamishwa na polisi, hakusimama kwani nae alikuwa kwenye mwendo wa kasi. Bw. DUBE, katika msafara huo, alikuwa na abiria wawili ambao ni Bw. BOYCE MOYE & Bw. PERCE GEORGE. 

Mh. SOKOINE, ambaye alikuwa ni mtu wa miraba minne, alikuwa amekaa kiti cha nyuma huku akiwa hajafunga mkanda. Katika ajali hiyo, Mh. SOKOINE alirushwa toka nyuma hadi akagonga kioo cha mbele na hivyo kupelekea aumie sana. Mh. SOKOINE alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitali ya mkoa wa Morogoro ambako madaktari walithibitisha kifo chake.

25. SOKOINE Alipata Majeraha Makubwa

Marehemu SOKOINE alipata majeraha makubwa na kwa mujibu wa "Postmortem Report" yake iliyowasilishwa mbele ya CC ya CCM, mbavu na mifupa ya mikononi na miguuni vilivunjika. Mbavu zilizovunjika zilipelekea kuchoma mapafu yake!.

26. Mabodigadi wa Mh. SOKOINE Hawakuumia Sana

Ajali hiyo ilichukua maisha ya Mh. SOKOINE tu kwani wengine wote walisalimika na kupata majeraha ya wastani.

Bw. YUSTO CHUMA, aliyekuwa bodigadi wake ambaye alikaa kiti cha mbele kulia, na Bw. ALLY ABDALLAH aliyekuwa dereva wake, walijeruhiwa kiasi. Prof. ISSA SHIVJI anatanabaisha-:

"Neither Sokoine's bodyguards in the car nor anyone else in the other vehicles, including Dube, were seriously injured".

27. Rais NYERERE Atangaza Kifo

Alasiri ya siku hiyo, RTD ilisitisha ghafla matangazo yake na ukapiga wimbo wa Taifa. 

Rais NYERERE, baada tu ya wimbo huo na kwa uchungu mkubwa, akalitangazia Taifa msiba huo wa kihistoria kama ifuatavyo-:

"Ndugu wananchi, leo hii ndugu yetu, kijana wetu, Edward Moringe Sokoine, Waziri Mkuu wa Tanzania, alipokuwa akirejea Dar es Salaam toka Dodoma, gari lake lilipata ajali na amefariki. Ndugu Watanzania naomba muamini Edward amefariki kwa ajali na si kitu kingine".

28. Rais NYERERE Aangua Kilio

Baada tu ya Rais NYERERE kutoa taarifa hiyo alibubujikwa na machozi kutokana na uchungu mkubwa. Mwandishi nguli, Bw. ATILIO TAGALILE, aliyekuwa "Daily News" kipindi hicho, alieleza April 15, 2015 kuwa Mwalimu NYERERE, baada tu ya kutangaza, akatokwa machozi!.

29. Vilio Vyatamalaki Nchini

Baada tu ya taarifa hiyo, vilio na simanzi kubwa vilitamalaki nchi nzima. Kwenye maofisi, vyuoni, mashuleni, kwenye mabaa, mabarabarani, kote huko wananchi walionekana dhahiri wamevurugwa!.

Kikao cha UWT kilichokuwa kikifanyika Lumumba, kilisambaratika ghafla bila hata Mwenyekiti wake, mama SOPHIA KAWAWA, kukiahirisha kwani mara tu baada ya taarifa hiyo iliyoleta huzuni, jakamoyo na jitimai kubwa, wakinamama waliangua vilio kwa sauti za juu sana!.

30. Serikali Yatangaza Wiki Mbili za Maombolezo

Serikali ilitangaza wiki mbili za maombolezo na kuamuru bendera nchi nzima kupeperushwa nusu mlingoti.

31. Rais NYERERE Aangua Kilio Baada ya Kuuona Mwili wa Mh. SOKOINE

Mwili wa marehemu SOKOINE uliwasili Ikulu, Dsm toka Morogoro saa 11 jioni siku hiyohiyo ukiwa umefunikwa kwa bendera ya Taifa. 

Rais NYERERE, akiongozana na Mama MARIA, waliujongelea mwili huo na kisha Rais NYERERE akaifunua bendera na kuweka mikono yake miwili kwenye paji la uso wa SOKOINE.

Rais NYERERE na Mama MARIA, aliyekuwa na kitambaa cheupe, walilia kwa uchungu sana hadi kuondolewa na walinzi wao. Bw. ATILIO TAGALILE, mwandishi wa "Daily News" wakati huo aliyekuwepo Ikulu, aliandika-:

"Mwalimu Nyerere burst into tears and was whisked away by his bodyguards".

32. JOSEPH NYERERE Azua Kimuhemuhe Ikulu!

JOSEPH NYERERE, mdogo wa Rais NYERERE, ambaye alijulikana kwa kutomung'unya maneno, alikwenda kwa kasi ulipokuwepo mwili huku akiwa na huzuni kubwa na akasema-:

"Mwalimu huna ulinzi. Waziri Mkuu anafia barabarani?!!!" .

Prof. ISSA SHIVJI anafafanua jinsi JOSEPH NYERERE alivyoondolewa-:

"Security guards quickly whisked Joseph Nyerere away from the casket and he was driven away from the State house".

 Mwili wa marehemu SOKOINE ukapelekwa hospital ya Lugalo kwaajili ya kuhifadhiwa.

33. Jeneza la SOKOINE Latengenezwa Usiku wa Manani

Shughuli ya kutengeneza jeneza la SOKOINE alipewa Bw. GEORGE CHRISTOS, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari TZ. Huyu alikuwa ni chotara kwani baba yake alikuwa ni Mgiriki na mama yake Msukuma akiitwa MARIA, aliyekuwa mmoja wa mabinti wa Chifu KIDAHA.

Saa 12 jioni ya siku hiyo, Bw. CHRISTOS na mkewe, Bi. ELIZABETH WALKER & Bw. PAUL MKANGA, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, walienda hospitali kuchukua vipimo vya mwili wa SOKOINE. Kisha wakaelekea Chang'ombe kilipo kiwanda cha HEM-SINGH ambako bahati nzuri mwenye kiwanda alikuwa hajafunga.

Kazi ya kutengeneza jeneza ikaanza mara moja na kumalizika usiku wa manane. Kisha, Bi WALKER akalipamba jeneza hilo na likapelekwa hospitalini. 

34. SOKOINE Aagwa na Wakazi wa Dsm

Siku ya Ijumaa, Aprili 13, 1984, maelfu ya wakazi wa jiji la Dsm na mikoa ya jirani walifurika "Karimjee Hall" kumuaga mpendwa wao, marehemu SOKOINE. Kwa hakika, umati uliokuwepo uliweka rekodi iliyokuja kuvunjwa na umati uliojitokeza Octoba 21,1999 kufuatia kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu NYERERE.

35. Daladala Zapeleka Abiria Bure "Airport"

Jumamosi  ya Aprili 14, 1984, mwili wa marehemu SOKOINE ulipelekwa "airport" kwaajili ya kusafiridhwa kwenda  Arusha  kwenye mazishi. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Daladala zote jijini zilipeleka abiria bure uwanja wa ndege kumuaga mpendwa wao. Mwandishi Bi. HELLEN MATABA anajuza zaidi-:

"Sokoine was the brainchild of city commuter buses commonly known as "Daladala" and no wonder hundreds of thousands of Dar es Salaam residents were ferried on Daladala free of charge and then Sokoine's body  was flown to Monduli for burial".

36. SOKOINE Azikwa kwa Heshima Zote

Kaburi la aina yake lilijengwa huko Monduli na MJ JOHN BUTLER WARDEN "Black mamba", Mtanzania chotara, na aliifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na askari wa TPDF.

" Black Mamba" alifanya kazi nzuri kiasi cha kupewa "mchongo" wa kujenga kaburi la aliyekuwa Rais wa Nchumbiji, marehemu SAMORA MACHEL aliyefariki baada ya ndege yake aina ya "Tupulov Tu 135" kuanguka Octoba 19, 1986.

Mazishi ya marehemu SOKOINE yalipewa heshima zote na yaliyohudhuriwa na umati wa watu wakiongozwa na Baba wa Taifa .

Bw. OLIVER TAMBO, aliyekuwa Rais wa ANC na ALFRED NZO, aliyekuwa Katibu  Mkuu wa ANC, walihudhuria na kuelezea kusikitishwa sana na kifo hicho kilichosababishwa na raia mwenzao wa Afrika Kusini. 

37. SOKOINE Aacha Wake 2, Watoto 11

SOKOINE alikuwa na wake wawili ambao ni NAPONO na NAKITETO na watoto 11.

38. DUMISAN DUBE Afikishwa kwa Pilato

Mei 17, 1984, Bw. DUMISAN DUBE alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro ambako kesi yake iliahirishwa.

Juni 12, 1984, upande wa mashaka ukiongozwa na Bw. JOHNSON MWANYIKA (SSA) ulitinga mahakamani na mashahidi 21. Hata hivyo, Bw. DUBE aliposomewa mashtaka 7 alikiri hivyo Mh. SIMON KAJI (PRM) akampa kifungo cha miaka mitatu. 

39. Kwanini SOKOINE Alipendwa Sana?

Nukuu zake kuntu zinajibu swali hilo-:

39.1 SOKOINE alichukia sana wazembe:

"Ole wake kiongozi asiye na nidhamu na mzembe ntakaemkuta. Viongozi wazembe na wabadhilifu wahesabu siku zao"

39.2 SOKOINE alitaka Wazazi Wawajibike kwa Watoto Wao:

"Vijana wengi siku hizi wana mali kuliko wazazi wao waliofanya kazi kwa miaka zaidi ya 40 lakini wazee hao wanataka Serikali ndio iwaulize watoto hao wamepata wapi mali hizo. Mzazi unashindwa nini kumuuliza mwanao?"

39.4 SOKOINE Alihimiza Majeshi Yawe kwa Faida ya Wote:

"Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi kuwa chombo cha kulinda haki na maslahi ya wengi. Kamwe hayaruhusiwi kuwa chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao".

39.4 SOKOINE Alikuwa Mzalendo wa Kiwango cha Juu:

"Viongozi wanaoteuliwa lazma wawe wazalendo wa hali ya juu. Naskia huko mikoani kuna viongozi wanagombania magari na nyumba. Mambo hayo si muhimu. Viongozi wanatakiwa kugombania juu ya Maendeleo ya wanavijiji. Huu ni ugomvi mtakatifu".

39. 5 SOKOINE Alichukia Upuuzi

Mwezi Machi 1983, PM SOKOINE alifanya ziara Singida. Mmoja wa viongozi mkoani humo akamfuata Bw. ACCADOGA CHILEDI aliyekuwa "Press Secretary " wa PM SOKOINE na kumwambia- 

"Mzee tumeishamtayarishia blanketi chapa ya mtu" (akimaanisha kimada). Bw. CHILEDI akamuuliza kiongozi huyo- "Brother, Mh. Sokoine unamjua au unamsikia? Hilo blanketi lako ondoka nalo haraka na utoweke kabisa maana nikimjulisha ujue unapoteza kazi yako sasa hivi"

39. 6 SOKOINE Alikuwa Mchapakazi Hodari:

SOKOINE alikuwa mchapakazi hodari na alipenda sana kuwatumikia wananchi. Prof ISSA SHIVJI anadadavua-:

"Sokoine's personal integrity was beyond reproach. He worked hard and demanded an equal level of hard work and accountability from his subordinates"

SOKOINE daima alifanya kazi hadi usiku na mara nyingine hadi usiku wa manani. Mh. MARTENS LUMBANGA (Baba wa Bi HARRIETH ), aliyefanya kazi kwa karibu na SOKOINE, alitiririka April 7, 2021-:

"Mimi nilikuwa Kamishina wa Planning. Nilikuwa nafanya kazi na makamisha wengine na Sokoine mara nyingine hadi usiku wa manani kisha anatusindikiza ye anarudi kuendelea na kazi. Asubuhi tunakuta ameishatoa mafaili. Marehemu Sokoine alikuwa Mfanyakazi hodari, Mwaminifu na Muungwana sana".

39.7  SOKOINE Hakupenda Utajiri

Maisha ya SOKOINE yalielezewa kwa ufasaha na Mwalimu NYERERE kwenye msiba wake- 

"Edward hakuwa na mali yoyote ukiachilia ng'ombe wa urithi. Alikuwa na suti tatu na viatu pea mbili tu".

39.7 SOKOINE Alikuwa Mbunifu Sana

SOKOINE alianzisha "PRESIDENTIAL TRUST FUND" Ikulu ambapo alikuwa akiweka sehemu ya mshahara wake ili kuwasaidia akina mama kuweza kukopa. Mshahara wa PM wakati huo ulikuwa ni TZS 3, 000/= kama alivyobainisha Mh. CD MSUYA (PM 1980-1983) "Kwenye sherehe ya siku yangu ya kutimiza miaka 80 niliwaambia marafiki zangu kuwa nilipokuwa PM nilikuwa napokea mshahara wa TZS 3,000/= tu, hawakuamini."

39.8 SOKOINE Alikuwa Mcha Mungu Sana

SOKOINE alikuwa Mkristo Mkatoliki na aliipenda sana dini yake na alikuwa mwanachama wa utawa wa tatu wa Mt. Fransisca. SOKOINE alikuwa akisali kanisa la Mt. Joseph, Dsm ambako Jumatatu, Aprili 12, 2021 kutakuwa na misa maalum kumkumbuka iliyoandaliwa na familia yake.

39.9 SOKOINE Alipambana Vikali na Wahujumu Uchumi

SOKOINE aliendesha mapambano makali na wahujumu uchumi yaliyopelekea hadi Mh. EDWARD BARONGO, RC Kilimanjaro "aliwe kichwa" na kuwekwa "detention" kwa miezi minne hadi alipoachiliwa na Rais NYERERE".

40. Rais Marehemu Dr. JPM Alimkubali Sana SOKOINE

Marehemu Dr. JPM alimkubali sana SOKOINE, kama alivyoeleza Aprili 12, 2018-:

"Aprili 12, 1984 Sokoine alipofariki ilikuwa ni huzuni kubwa sana. Mimi nilikuwa kwenye mafunzo ya lazima JKT Mpwapwa "Operesheni Nguvukazi". Sokoine kamwe hatasahaulika kwani alipiga vita rushwa, wizi na unyonyaji. Alikuwa Mzalendo wa kweli hivyo ni wito wangu kwa Watanzania tumuige na tumuishi."

41. Jeshi Lilimpenda Sana SOKOINE

SOKOINE alipendwa sana na Jeshi toka alipoongoza Wizara ya Ulinzi; kama Prof. ISSA SHIVJI anavyofafanua katika kitabu cha "A Biography of Julius Nyerere"

"Sokoine was the political leader whom the Army respected most after Nyerere because he earned their trust when he was the Minister of Defence for five years between 1972 and 1977"

42. Mwalimu NYERERE Ampa Mjukuu Wake Jina la MORINGE

Baba wa Taifa alikuwa na watoto 7 na wajukuu kedekede na alifanya kazi na Mawaziri Wakuu wengi. Hata hivyo, ni jina la MORINGE tu ndilo alilompa mmoja wa wajukuu zake. Prof. SAIDA YAHYA-OTHMAN anatujuza zaidi katika kitabu chake cha "A Biography of Julius Nyerere"-:

"Nyerere named one of Magige's sons Moringe, after Edward Sokoine, who was much beloved by Nyerere, and whose death in 1984 was absolutely devastating to him".


43. SOKOINE Alimchagua mwanae JOSEPH Kuwa Mkuu wa Familia


Kati ya watoto wake wote 11, SOKOINE alimpenda sana JOSEPH na alikuwa akimuamsha mara kwa mara usiku kuandika "notes" za masuala ya kitaifa. Jumamosi moja alimuamsha usiku wa manani na kumwambia amemteua yeye kuwa mkuu wa familia. JOSEPH akamwambia mbona kuna kaka zake wakubwa na pia kesho yake wanaenda kanisani asubuhi, si watachoka sana? SOKOINE akamjibu-:

"Nimezoea kufanya kazi hadi usiku mwingi ili kuwatumikia wananchi. Aidha, nina sababu zangu za kukuteua wewe kuwa Mkuu wa familia lakini usifikiri nakupa ufalme. La hasha. Nakupa utumwa na utumishi wa familia yangu".

Bw. JOSEPH alikuja kuwa Balozi na Naibu Katibu Mkuu. 

44. "LANDCRUISERS" Zapewa jina la DUBE!

"Bongolanderz" ni viumbe wasioishiwa maneno. Kutokana na kuwa Bw. DUBE ndiye aliyeendesha gari lililomuua SOKOINE lilikuwa aina ya "Toyota Landcruiser", basi toka wakati huo, aina hiyo ya magari ikawa inaitwa "DUBE"!.

45. TAMATI

Huyu ndiye marehemu EDWARD MORINGE SOKOINE, mmoja wa viongozi bora kabisa kuwahi kutokea nchini, ambaye alikuwa mzalendo wa kweli aliyewapenda wananchi wenzake kwa dhati kabisa ya moyo wake na aliyejitolea kwa hali na mali kuwasaidia na alichukia na kupambana vilivyo na wezi wa mali za umma, wala rushwa na walanguzi.

SOKOINE alikuwa mchamungu na alichukia maovu kwa dhati ya moyo wake na hakushiriki hata kidogo kwenye vitendo viovu.

46. Tafakuri Jadidi

46.1 Je, ni viongozi wangapi leo wanaweza kujitolea sehemu ya mshahara wao kusaidia wengine kama alivyokuwa akifanya SOKOINE?

46.2 Je, wewe kama Kiongozi ( iwe Kiranja darasani, kiongozi wa Kata  Serikalini na kwingine) unamuenzi na kumuishi marehemu SOKOINE kama alivyoasa hayati Dr. JPM?

46.3 Kwakuwa maneno ya mwisho ya SOKOINE bungeni Idodomia alionya vikali na kusema "Jambo hili la kutumia fedha bila ya idhini ya Bunge lazima tulikomeshe", je Taifa linamuenzi kivitendo marehemu SOKOINE kwa kutofanya jambo hilo?

Na Mzee wa Atikali ✍️✍️✍️

atikaligbm@yahoo.com

0754744557

Atikali Hii Inalindwa na Hatimiliki

April 12, 2021.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...