NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA

MKAZI wa Buhongwa,Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza,Bakari Mrisho ameibua malalamiko ya kudhulumiwa nyumba ya marehemu baba yake,Mrisho Bakari na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan kumsaidia arejeshewe nyumba hiyo. 

Amesema kuwa kwa miaka 18 amehangaika kutafuta haki yake bila mafanikio ikizingatiwa nyumba hiyo iliuzwa kwa nyaraka batili na yeye kama mrithi halali hakuwahi kuagiza iuzwe,lakini kwa mfumo na mazingira yaliyokuwepo kwa wakati huo kwenye vyombo vya sheria ameshindwa kupata haki.

Nyumba hiyo iliyopo katika Mtaa wa Mlimani A Kirumba,kwenye Kiwanja Na.10, Kitalu A III, Manispaa ya Ilemela kwa sasa, mwaka 1986 na Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Nyamagana kwa kutumia nyaraka za kughushi.

Akizungumza na Michuzi Blog  jana Mrisho alilalamika kuwa,Mambosasa akiwa Katibu wa Bakwata Wilaya ya Nyamagana,(wakati huo) aliuza nyumba ya marehemu baba yake (Mrisho Bakari) kwa nyaraka ban dia akishirikiana na Saad Ali (sasa marehemu).

Alisema nyumba hiyo aliuziwa Suleiman Mbaraka Salum, wakati huo yeye Bakari Mrisho akiwa Mombasa, Kenya ikidaiwa kuwa alishafariki lakini kwenye hati ya mauziano inaonyesha alipewa mgawo wa sh.100,000 ambao hakuwahi kuupokea.

Mrisho alisema,alibaini kuuzwa kwa nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Mlimani A Kirumba baada ya kurudi nchini kutoka Kenya ambapo Oktoba Mosi, 1986 Idara ya Ardhi Jiji la Mwanza kabla ya kugawanywa na Ilemela ilibadilisha jina la mmiliki kutoka kwa Mrisho Bakari kwenda kwa Suleiman Mbaraka Salum kwa hati Na.033062/135.

Alisema kuwa aliamua kufungua kesi ya mirathi kwenye Mahakama ya Mwanzo Ilemela na kushinda ambapo mahakama hiyo ilimtambua kama mrithi halali na kuiagiza Manispaa ya Ilemela kufuta mirathi 40/85 iliyotumika kuuza nyumba ya baba yake lakini hadi leo hakuna kilichofanyika.

“Nikiwa mrithi pekee wa marehemu baba yangu,nimeporwa na kudhulumiwa nyumba na kumilikishwa mtu mwingine sababu ya fedha,leo miaka 18 nimehangaika mahakamani bila mafanikio licha ya kutambua ni mrithi halali kwa kuwa mirathi namba 40/85 iliyotumika kuuza nyumba ni batili,”alisema Mrisho.

Hata hivyo,aligundua kunyofolewa kwa nyaraka za ushahidi mbalimbali kwenye jalada la ardhi, kiwanja namba 10 katika Manispaa ya Ilemela ili kumnyima haki huku majalada ya mashauri aliyofungua kwenye mahakama tofauti yakipotezwa mara tatu kuanzia la kesi ya jinai(kughushi nyaraka na kuuza nyumba),jalada la kesi iliyofunguliwa Baraza la Ardhi Nyamagana nalo lilipotea.

Alieleza kuwa amezunguka kwa miaka 18 mahakamani na kwenye ofisi za vyombo mbalimbali za umma akitafuta haki yake bila mafanikio likiwemo Baraza la Ardhi Nyamagana baada ya kumpa ushindi mdaiwa,hata alipoomba nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi ya jinai na fomu ya kusudio la kukata rufaa alinyimwa na kuambiwa kompyuta ziliibwa.

Mhanga huyo alisema anamwomba Rais Samia Suluhu Hassan, kumsaidia kupata haki yake kwani anapata shida ya kupanga nyumba ya makazi ya kuishi ilhali nyumba ya urithi aliyoachiwa na marehemu baba yake akiitumia mtu mwingine.

Alidai haki yake imeporwa na watu wenye fedha wakiwemo watumishi wa idara za Ardhi na Mipango Miji za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela na kumwomba Rais aingilie kati ili haki itendeke na ikibidi azifumue idara hizo ambazo zimetumika kuwapora wanyonge ardhi zao.

Akizungumza kwa simu jana, Mambosasa alisema kuwa ndiye alikuwa msimamizi wa mirathi ya Mrisho Bakari, ambapo mwanaye Bakari Mrisho alimshitaki Mambosasa mahakamani na kushindwa kesi.

“Hilo lilikwisha baada ya kumshinda mahakamani na shauri hilo halikuendeshwa kienyeji,alimshitaki pia wakili wangu Nasimire kwenye jopo la mawakili naye akamshinda,”alisema.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan, akiwasilisha mwelekeo wa serikali yake kwenye eneo la ardhi alisema “ Nataka Niseme, nimekuta ma-file (majalada) mengi pale ya uhaulishaji.Nataka niseme, umiliki halali wa ardhi.Watu wameporwa sana ardhi zao na walio facilitate uporaji huu ni maofisa ardhi.”

“Hao ndio wamesaidia wale watu wengine kuwa na documents fake (nyaraka bandia),nataka mkasimamie umiliki halali wa ardhi kwa wananchi na taasisi.Kuna migogoro kibao! Nimekuta kwenye mafaili ardhi hii kapewa huyu na kapewa huyu.” Aliongeza; “Naomba mkasimamie yaondoke haya, hata maeneo ya umma yanachukuliwa lakini Wizara ya Ardhi tupo lakini mkaangalie namna ya kudhibiti na kuwadhibiti maofisa ardhi mkoani na wilayani.Kule ndiko wanakocheza ngoma wanayoitaka wenyewe, dhuluma kubwa iko huko chini, kwa hiyo mkawasimamie maofisa ardhi mikoa na wilaya.”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...