Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

CHAMA  Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka kimesema kwamba kinaridhishwa na juhudi za kisera zitokanazo na  ufanisi, upeo na maarifa alionayo Mwenyekiti wa CCM na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika medani za  Kimataifa katika Utekelezaji wa Sera ya Nje na kuimarisha Sera ya Diplomasia ya Kiuchumi

Hayo yamesemwa na Chama hicho baada ya Rais Samia kufanya ziara nchini Kenya na kisha kupata fursa ya kuhutubia mabunge mawili ya nchi hiyo.

 Akizungumza jijini Dodoma, Shaka amesema,  Rais Samia licha ya kuonesha upeo, maarifa na ufahamu  mpana wa masuala ya Kidiplomasia, ameweka bayana msimamo wa  nchi yake akionesha dhamira njema ya kutaka uendelezwa ushirikiano  wa Kanda ya Afrika Mashariki.

Ameongeza CCM haikukosea kumteua  kuwa Mwenyekiti wa Chama, kwani Chama chake  hakikuwa na  hofu katika kushika nafasi hiyo nyeti na ya juu kabisa kutokana na uzoefu na umahiri wake wa Uongozi. 

" Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ni kuendeleza diplomasia ya kiuchumi baada ya  kupata mafanikio makubwa ya kujitangaza, kuweka bayana misimamo yake hatimaye kufahamika kimataifa kutokea awamu ya kwanza hadi ya sita.Rais Samia amekuwa ni Rais wa awamu ya sita.

"Amekuta  wakuu wenzake wa nchi  wakiwa madarakani hivyo hana budi kuwatembelea, kujitambusha, kujadiliana na kuendeleza na kuboresha mambo yote mazuri yaliofanywa na mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Magufuli.

"Rais hatazuiwa  kwenda mahali popote kwakuwa zipo sababu maalum kwa maendeleo ya nchi na watu wake. Hatasita kushiriki kwenye meza za majadiliano ya kisiasa au ya kiuchumi,. Atashiriki mazugumzo ya kibiashara, uwekezaji na mijadala ya kilimo afya, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi . " amesisitiza Shaka.

Ameongeza  Rais Samia katika hotuba yake  ameweka bayana haja ya kuvutia wawekezaji, Kama ilivyoahidiwa na CCM  katika Ilani ya Uchaguzi 2020 – 2025 Fungu la 22 (a) “Chama kitazielekeza serikasli zake mbili, Kuimarisha Utekelezaji wa Mpangpo wa kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini ili kuendelea kuvutia Sekta Binafsi kushiriki katika uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuiweka nchi katika nafasi nzuri katika mizania ya kimataifa ya wepesi wa kufanya biashara.”

Shaka amefafanua kuwa, ziara hiyo ya Mhe. Rais ni utekelezaji wa Ilani ya CCM katika masuala ya Kidipomasia na kusisitiza kuwa, katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025  Fungu la 132 (a ) inaeleza,

“Chama kitaielekeza Serikali, kuboresha utekelezaji wa mipango ya kuimarisha diplomasia ya siasa ya kimkakati kwa ajili ya kulinda amani, uhuru, maslahi ya Taifa na kuimarisha ujirani mwema pamoja na kushiriki kikamilifu katika kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kukuza mahusiano ya kiuchumi na Mataifa, Jumuiya za Kikanda na taasisi nyingine za Kimataifa.”

Aidha, Chama kimempongeza Rais Samia, kwa kuendeleza msisitizo kwa kuyapa msukumo masuala ya ulinzi na usalama, mapambano dhidi covid 19 pia ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama wa kikanda na katika kukabiliana na uhalifu. .


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...