Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo amekabidhi rasmi Ofisi ya Wilaya ya Kisarawe kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Nickson John Simon ambaye ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo baada ya kukamilisha mchakato wa kuteua wakuu wa wilaya nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Juni 24,2021 na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Idara za Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakiongozwa na Mkurugenzi wao Mussa Gama pamoja na viongozi wa taasisi zilizopo ndani ya Wilaya hiyo.

Akizungumza wakati akikabidhi ofisi hiyo Jokate ambaye amehamishiwa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam amesema anaondoka Kisarawe kiutendaji na kiutumishi lakini moyo wake umeja upendo mkubwa wa wana Kisarawe ambao walimpokea , kumleta na kumfunda hadi kuendelea kuaminiwa tena na Rais Samia, hivyo kwake watabaki kuwa watu muhimu kwenye historia ya maisha yake.

"Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ndugu yangu Nickson wewe ulishaonesha mahaba makubwa na Wilaya yetu na huenda Rais wetu ameona hilo ameamua kukuleta Kisarawe.Wananchi wa Kisarawe wana upendo mkubwa, Kisarawe mambo yote ya maendeleo yanawezekana.Niwaombe ndugu zangu wana Kisarawe tumpe ushirikiano zaidi ule mliyokuwa mnanipatia mimi.

"Najua kuna muda lazima uwe mkali kwa maslahi mapana ya Kisarawe, kwa maslahi mapana ya Mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla.Ndugu yangu Nickson wewe ndio usukani wa Wilaya ya Kisarawe, njoo na maono yako,njoo na ubunifu wako, sio lazima ufanye kama nilivyofanya mimi, kikubwa unatakiwa kuwa na mipango yako ilimradi Kisarawe iende mbele.

Unaye Mbunge mzuri Selemani Jafo, hana tatizo lolote, ameniwezesha kufanya ninachokiona kinafaa,ametuachia uhuru na ukweli namshukuru, nawe Nickson mshike mbunge wetu atakusaidia.Binafsi niseme nawapenda sana Kisarawe mmenilea,mmenikuza na kunifanya niendelee kuaminika,"amesema Jokate.

Amefafanua Kisarawe ndio Wilaya yake ya kwanza kujifunza uongoza na hata alipokuwa anapita kwenye wakat mgumu kwa baadhi ya nyakati lakini wana Kisarawe waliendelea kumshika mkono na kumtia moyo.Nawashukuru sana Kisarawe."Kubwa zaidi naomba nikabidhi ofisi kwako, na viongozi na wananchi mumpe ushirikiano".

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Kisarawe Nickson Simon akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo, amesema amewaambia viongozi wa Wilaya hiyo na wananchi jambo kubwa ni kuendelea kushirikiana kwa lengo moja tu la kuleta maendeleo.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ambaye sasa amehamishiwa Wilaya ya Temeke, Nickson amesema kikubwa ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM, lakini kubwa zaidi wote kwa umoja wso watasonga mbele.

"Tukishirikiana kwa kila kidogo ambacho kila mmoja wetu anacho tukiunganisha tutakwenda mbali sana.Niseme tu Mkuu wetu wa Wilaya Jokate amefanya mambo makubwa na ameacha alama.Nami niahidi nitafanya zaidi ya alipofanya yeye maana amenionesha njia, nina mahali pakuzia pale alipoishia yeye.Mimi nimekuja na mambo matatu ambayo nitayasimamia kwa nguvu zangu zote ni ujuzi, sayansi na kuinua vijana kiuchumi kupitia biashara ndogo ndogo.

Hivyo amesisitiza maono yake kwa Kisarawe ni Ujuzi, Sayansi na kuinua wananchi kiuchumi na vyote hivyo vikifanyika watafanikiwa na kuvunja mzunguko wa umasikini kutoka kizazi kimoja kwenda kingine."Haya maono haya niliyonayo yatafanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja.

Ndoto yangu siku moja ni kuiacha Kisarawe ikiwa na ujuzi, yenye kuifahamu sayansi na uchumi wa wananchi hasa vijana uimarike.Kisarawe ni Wilaya kongwe,ni Wilaya ya wajanja na ndio maana ilikuwa ya kwanza kuwa Wilaya." 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Zuberi Kizwezwe amesema anamkaribisha Nickson na kumuomba awatawale wananchi kwenye mioyo yao na sio awatawale kwenye viwiliviwili huku akifafanua Jokate anaishi kwenye mioyo ya wana Kisarawe kwasababu aliwatawala katika mioyo yao.

Kizwezwe amesema matumaini yake ni kuona Kisarawe inakwenda mbele zaidi ya ilivyokuwa sasa na hilo linawezekana kwa ushirikiano wa viongozi na wananchi wote.

."Nitoe ombi kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke endelea kumshauri mkuu wetu wa Wilaya, umekaa muda mrefu Kisarawe unaijua vizuri,usisite kumshauri, ukiona simu yake pokea,ipe umuhimu, ulivyokuwa Kisarawe Nicskon alikukimbilia hivyo nawe mkimbilie."


Wakati huo huo Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Mussa Gama amempongeza Nickson na Jokate kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku akitumia nafasi hiyo kuwapongeza kwa kuamua kufanya makabidhiano hayo kwa kushirikisha viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo.

"Wameona umuhimu wa kukabidhiana ofisi, lakini kwetu sisi Kisarawe hatuamini katika kuagana maana utumishi wa umma ni kuzunguka leo unaweza kuondoka na kesho au keshokutwa ukarudi Kisarawe."

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Kisarawe Khalfan Sika amewaomba watumishi wote wa Chama na Serikali kumpa ushirikiano Nickson na ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kuitazama Kisarawe kwa jicho la pekee, ametoa kijana ameingiza kijana.

Aidha ameomba viongozi na watumishi wasimpelee majungu kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, amesema anaimani na Nickson John atafanya vizuri na hamu yake ni kuona baada ya Kisarawe akawe mkuu wa mkoa na hiyo ndivyo anavyoamini.

Amemuhakikishia watu wa Kisarawe wanafanya kazi na wala sio watu wa kupenda ngoma kama watu wanavyosema."Kisarawe tunachapa kazi sana, wanapenda kujituma,ni jukumu la viongozi kuonesha njia".

Amesema Kisarawe hakuna magomvi ndani ya Wilaya hiyo ingawa changamoto kubwa ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, ameongeza ni imani yake atafanya vema na bahati nzuri naye ni Kihindi kideke."Tushirikiane, tunaamini DC wetu anaweza, narudia tena wale wapeleka majungu wasipeleke majungu kwa DC.

Kwa Jokate ameona ni kama amepanda, amekwenda kwenye wilaya kubwa kimapato na wanaamini atafika mbali zaidi.Amemuomba Jokate aende kuwatumikia wananchi wa Temeke, kama alivyofanya Kisarawe, ameacha alama na sasa Rais amemuamini kwa kumpa Wilaya kubwa,.Kisarawe unayoiacha leo utaikuta zaidi ya unavyoiacha."

Awali kwa niaba ya Wazee wa Wilaya ya Kisarawe Juma Kilumbi Mpapasingo amesema "Nimesikia tu kwenye vyombo vya habari, sijaona ila nimesikia, hivyo baada ya kuondoka Kisarawe na kwenda Temeke nimeona nami nije hapa kusikiliza anavyoagwa.

Mimi sioni ila nasikia,Mama Jokate tumekaa naye wana Kisarawe wote, ni mwanamke mpambanaji, Mama huyu kabuni tokomeza Zero,kabuni Ushoroba, amejenga shule.Tunampenda sana na ukweli hakuna tofauti na mtoto ambaye unampenda halafu anaolewa,unachukua mahali lakini siku akiondoka unaumia.

"Kwa Nickson Kisarawe hatumpendi mtu,hatumchukii mtu, ukituchukia tutakupenda, ukituudhi tutakufurahia.Tunaamini utafanya makubwa kama alivyofanya Jokate, uongozi ni ubunifu na sio tu kufanya yale Ilani, tunategemea ubunifu wako.

Nakuomba upokee simu zangu, maana shida ya viongozi ni kutopokea simu, naomba simu zangu uwe unapokea.Jokate nenda Temeke ,kawatumie wananchi, Nickson karibu Kisarawe tutakupa ushirikiano.Niombe wewe unayekwenda Temeke kaongoze vizuri na wewe unayekuja Kisarawe utuongoze."

 

Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo( kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe( wa pili kulia) wakiwa wameshika nyaraka za kiofisi baada ya kufanyika kwa makabidhiano ya ofisi ya Wilaya ya Kisarawe.Makabidhiano hayo yamefanyika leo Juni 24,2021 . na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo
Mkuu wa Wilaya Kisarawe Nickson Simon (kushoto) na Katibu Tawala wa wilaya hiyo Mwanana Msumi(kulia) wakimsikiliza Jokate Mwegelo ambaye leo Juni 24,2021 amekabidhi ofisi rasmi baada ya kuhamishiwa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Simon akiwa akisalimiana na viongozi wa wilaya hiyo kabla ya kuingia ukumbini kwa ajili ya kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo ambaye amehamishiwa Wilaya ya Temeke
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo ( kulia) na Mkuu wa Wilaya Kisarawe Nickson Simon ( kulia) wakielekea ukumbini wakati wa tukio la makabidhiano rasmi ya ofisi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Mussa Gama akiwa makini kufutilia maelezo ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo ambaye amekabidhi ofisi rasmi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Simon leo Juni 24,2021
baadhi ya wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakiwa wameshiriki tukio la aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo kukabidhi rasmi ofisi kwa mkuu wa wilaya hiyo Nickson Simon
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo (kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Simon wakati wa tukio la makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika leo wilayani humo
Katibu Tawala Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Mwanana Msumi akizungumza wakati wa tukio hilo
viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakiwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo(wa nne kushoto) wakati wa tukio la makabidhiano ya ofisi
sehemu ya watumishi na viongozi wa Chama na Serikali wa Wilaya ya Kisarawe wakiomba dua wakati wa ufungzuzi wa kikao cha makabidhiano ambapo Jokate Mwegelo alikuwa anakabidhi ofisi kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Nickson Simon leo Juni 24,2021
 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...