Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Hussein Blood Drive (Khoja Shia) itawazawadia jezi mashabiki wa soka 200 watakaojitolea damu, ambazo watazivaa kwenda kushuhudia pambano la watani wa jadi nchini Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Mashabiki hao wa mkoani Kigoma watazawadiwa jezi za mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Simba na washindi wa pili, Yanga ambao watacheza fainali ya Kombe la Azam Sports Federation, Jumapili hii mjini Kigoma.

Kwa mujibu wa Mratibu wa taasisi hiyo,  Azim Dewji, mashabiki hao 200 kila timu itatoa mashabiki 100 watakaozawadiwa jezi hizo za Simba au Yanga.

"Mbali ya kutoa zawadi za jezi hizo mia mbili, pia kutakuwa na fursa ya mashabiki hamsini, ishirini na tano kwa kila upande kupiga picha na wachezaji wao nyota.

"Katika hili la kupiga picha, shabiki atakayependa kupiga picha hiyo na mchezaji wake anayempenda atachangia shilingi laki mbili. Fedha zitakazopatikana zitakwenda kununua jezi zaidi kwa ajili ya kugharimia zoezi kama hili mikoa mingine," alisema Azim.

Azim ambaye alikuwa mfadhili mkuu wa Simba ilipofika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, alisema kazi ya utoaji damu itafanyika katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni siku ya Jumamosi.

Aidha, alisema mahali kwa ajili ya mashabiki kwenda kupiga picha na wachezaji patatangazwa kabla ya Jumamosi.

Taasisi ya Hussein Blood Drive (Khoja Shia) imekuwa na utaratibu wa kuchangisha damu kwa ajili ya kuweka akiba na kuwapatia wahitaji kutokana na sababu mbalimbali.

Mwaka juzi na mwaka jana walifanikisha kupatikana kwa chupa 500 wakati wa mechi za watani hao wa jadi wa soka la Tanzania kwa mechi za Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, kuchangia damu kwa hiari ni muhimu sana kwa taifa la watu wenye afya njema.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaelekeza kila nchi mwanachama kukusanya damu asilimia moja ya wakazi wa nchi yake au chupa 10 kwa kila wananchi 1,000 ili kujitosheleza na mahitaji ya damu salama wakati wote.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...