NA MWANDISHI WETU, SENGEREMA

MRADI wa uanzishwaji wa Kituo kitakachosaidia kuondoa changamoto zinazoikabili jamii nchini hususan maeneo ya vijijini, umetambulishwa kwa wananchi wilayani Sengerema mkoani Mwanza na Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe. Erick Shigongo.

Mradi huo utakaokuwa chini ya Taasisi ya “Kijiji” utatekelezwa   katika Kijiji cha Kasisa jimbo la Buchosa, Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, umebuniwa na Familia ya Aliyekuwa Mbunge wa Kwanza wa Kuchaguliwa jimbo la Sengerema kati ya mwaka 1965-1985, marehemu Alphonce Rulegura, ili kuenzi nia yake njema ya kuwawezesha wananchi wa jimbo hilo kuondokana  na umasikini.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taasisi hiyo mjini Sengerema, Mbunge wa jimbo la Buchosa ambalo liko wilayani humo, Mhe. Erick Shigongo alisema, mradi huo utaleta faida kubwa sio tu kwa wanakijiji wa Kasisa na maeneo jirani lakini pia nje ya jimbo la Buchosa.

“ Kilichofanyika hapa leo hii ni baraka kubwa sana na nina uhakika marehemu Rulegura huko aliko mbinguni ana furaha kubwa sana kwani jambo hili linaendeleza mema aliyokuwa akiyafanya kwa watu wa Sengerema,” alisema Mhe. Shigongo

Alimpongeza Muasisi na Rais wa Taasisi hiyo ya “Kijiji”, Bi. Clara Luregura Ford, ambaye ni binti wa marehemu Rulegura kwa kuona umuhimu wa kuendeleza ndoto za marehemu baba yake licha ya kwamba kwa sasa binti huyo anaishi na kufanya kazi nchini Marekani.

“Ninachokishuhudia hapa leo ni fundisho kuwa watoto tunao wajibu wa kuziishi na kutimiza ndoto za wazazi wetu na kuhakikisha majina yao hayapotei kwa sisi kutenda mambo mema katika jamii tunazoishi.” Alisema Mhe. Shigongo.

Akielezea malengo ya Taasisi ya “Kijiji”, mjumbe wa Bodi,  Bw. Martin Rulegura alisema ni kuchagiza swala la maendeleo endelevu katika Tanzania kupitia elimu, uwezeshaji wa jamii, wanawake na vijana.

Alisema wazo la kuanzishwa taasisi ya Kijiji lilianza mwaka 2018 wakati Muasisi na Rais wa Taasisi hiyo, Bi. Clara Rulegura Ford akiongozana na familia yake alitembelea kijiji cha Kasisa, mahala alikozaliwa baba yake na kwamba alipokelewa kwa furaha na wana kijiji ambao walimueleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.

“Mlinipatia risala ya mahitaji na nikaahidi ninavyoweza kusaidia na ilinichukua miaka mitatu baada ya kufanya utafiti kufikia uamuzi huu, lengo langu halikuwa kutoa fedha tu, na sasa tumefika mahala ambapo tunaweza kuanza kushughulikia changamoto zetu.” Alisema Bw. Martin akinukuu hotuba ya Muasisi na Rais wa Taasisi ya Kijiji Bi. Clara Rulegura Ford.

Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi na watu werevu na kama alivyosema baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, kwamba Watu Tunao na Ardhi tunayo hakuna sababu ya maana wananachi washindwe kuishi maisha yao kwenye uhuru wa Kiuchumi.

Hivyo ili kutatua tatizo la umasikini ni lazima kujua asili yake ili kuung’oa umasikini kutoka kwenye mizizi yake, Alisema Bi. Clara kwenye hotuba hiyo.

“Ndio maana hiki Kituo kitajikita katika miradi 9 ambayo ni kutoa elimu ya mafunzo ya ufundi stadi,  Nyumba endelevu na imara,  Ufanisi wa Nishati,  Nishati Mbadala, kujenga miundombinu wezeshi ya Upatikanaji wa maji safi na salama, Usanifu wa vyoo na mifumo ya majitaka, elimu ya Afya, Kilimo endelevu na cha  Umwagiliaji, Udhibiti wa taka na uchakataji.” Alifafanua Bw. Martin.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, ambaye aliwakilishwa na Afisa Tarafa wa Wilaya hiyo Bw. Fadhili Abel alisema kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Sengerema wanaipongeza Taasisi ya Kijiji kwa kuja na mradi huo kwani utaharakisha nia ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.

“ Safari ya kuwaletea maendeleo wananchi ambayo serikali ingechukua miaka 50, lakini tukiungana na Taasisi zisizo za Kiserikali kama hii ya Kijiji tunaweza kuchukua miaka 10 tu kuwafikisha wananchi wetu katika maisha ambayo wanastahili kuishi.” Alibainisha Bw. Fadhili.

“ Jukumu mnalolitekeleza linarahisisha utendaji kazi wa Serikali, changamoto zitakazoenda kutatuliwa na hii Taasisi ya Kijiji, kwa namna moja au nyingine itarahisisha maendeleo ya watu wetu huko katika kijiji cha Kasisa na sio Kasisa pekee lakini pia maeneo mengine nje ya kijiji.” Alifafanua na kuongeza…..Pale ambapo viongozi wa Taasisi wanapohitaji msaada wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya iko wazi kusaidia.

Kwa upande wao, wanakijiji wa Kasisa ambako ndiko kutajengwa Kituo hicho wameeleza furaha yao na kutaja vipaumbele vyao kuwa wangependa Taasisi ya Kijiji ianze kutatua shida ya upatikanaji wa Maji Safi na Salama ikifuatiwa na eneo la Elimu kwa na Afya.

“ Tunaomba mradi uanze na maji, tunasumbuka na maji, maji yetu sio salama, tunapata maji kutoka ziwani na kisimani, ziwani ni mbali na haya ya kisimani ni machafu na tunatumia kwa kupikia na kunywa.” Alisema Bi. Sabina Paulo, ambaye ni anatoka kitongoji cha Kigongo.

Alisema maji ya kutumia kwa kunywa na kupikia wanayapata kutoka ziwani na visimani.

Hata hivyo ili upate maji ya ziwani unatembea umbali mrefu wakati yale ya kisimani hayana ubora unaotakiwa na hivyo amesisitiza kuwa mradi uanze na kutatua changamoto ya Maji na mingine itaendelea kufanyiwa kazi.

“Mimi ninafurahia mradi huu, mimi ni fundi wa kuchana mbao kwa kutumia mikono na msumeno, nimeshazeeka, watoto wangu wakipata elimu ya ufundi kutumia mashine za kisasa itasaidia katika kazi zetu.” Alisema mwanakijiji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Makoye Shilole Shigemelo.

Katika uzunduzi huo Familia ya Marehemu Rulegura iliongozwa na Mkewe, Bi. Margaret  Rulegura na watoto wake Coleta Mnyamani na Martin Rulegura.

Mbunge wa jimbo la Buchosa ambalo liko wilayani Sengerema, Mhe. Erick Shigongo (kulia), akilakiwa na Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya KIJIJI, Bw. Martin Rulegura, wakati akiwasili ukumbini tayari kuzindua Taasisi hiyo mjini Sengerema Julai 20, 2021.

Mbunge wa jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza, Mhe. Erick Shigongo (kulia) akisalimiana na Bi. Margaret Rulegura, Mjane wa aliyekuwa Mbunge wa kwanza wa jimbo la Sengerema kuanzia 1965-1985, Marehemu Alphonce Rulegura huku Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Kijiji, Bw. Martin Rulegura (katikati) akishuhudia, wakati Bw. Shigongo alipofika kuzindua taasisi hiyo mjni Sengerema juzi. Taasisi hiyo itajenga Kituo cha kutoa elimu ili kuchagiza swala la maendeleo endelevu katika Tanzania kupitia elimu, uwezeshaji wa jamii, wanawake na vijana.

Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Sengerema na wengine kutoka Kijiji cha Kasisa wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi huo.
Mbunge wa jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza, Mhe. Erick Shigongo, akitoa hotuba yake.
Bibi Margaret Rulegura, Mjane wa Marehemu Alphonce Rulegura, akizunhgumza katika hafla hiyo ambapo alijielekeza katika kuelezea kiu ya mumewe katika kipindi cha uhai wake ambapo alikuwa karibu sana na watu na alitamani kuona jamii yake inastawi kiuchumi kwa kuwawezesha katika nyanja mbalimbali hususan za kibiashara.

Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya KIJIJI, Bw. Martin Rulegura, akitoa hotuba kwa niaba ya Muasisi na Rais wa Taasisi hiyo, Bi. Clara Rulegura Ford.

Bi. Margaret (kushoto), akiwa na wageni mbalimbali kutoka Kijiji cha Kasisa ambao walihudhuria hafla hiyo.
Bi. Margaret Rulegura, akiwa kwenye hafla hiyo.
Bi. Coleta Mnyamani, mmoja wa mabinti wa marehemu Alphonce Rulegura
Mmoja wa vijana waliosanifu mchoro wa kituo (Centre) itakayojengwa chini ya mradi wa Taasisi ya KIJIJI, akitoa maelezo kuhusu mchoro huo.





Padri Thomas K. Bilingi (kushoto) akiwakabidhi zawadi Familia ya marehemu Alphonce Rulegula wakiongozwa na mjane wa marehemu, Bi. Margaret Rulegura (katikati).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...