SERIKALI imezitaka taasisi za elimu ya juu kutathmini ni kiasi gani zimekuwa chachu ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuleta maendeleo ya nchi.

Aidha, imezitaka kuendelea kufanya tafiti zinazojikita kutatua changamoto za jamii na kuwezesha kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika pato la taifa.

Hayo yamesemwa leo Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Zena Ahmed Said wakati akifungua maonesho 16 ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Zena amesema taasisi za elimu ya juu na za utafiti zishirikiane na sekta binafsi hususan viwanda ili kuendeleza teknolojia na kuhamasisha matumizi yake  ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pia amezitaka taasisi hizo kushiriki kwenye mjadala wa kuboresha Mtaala wa elimu ili uendane na soko kwa kutoa wahitimu bora wenye kukidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa." Nimeambiwa katika maonesho haya kuna zaidi ya taasisi 100 hii ni ishara kwamba  maonesho haya huwapa manufaa ya ufahamu na ujuzi kuhusu kazi za utafiti zinazofanywa na vyuo vya elimu ya juu," amesema Said.

Kauli mbiu ya maonesho hayo ni kuendelea kukuza uchumi kupitia elimu ya juu sayansi na teknolojia inaakisi muelekeo wa serikali katika kujenga Tanzania ya Viwanda.

Amesema katika miaka mitano iliyopita uchumi wa nchi umeendelea kukua kwa asilimia 6.9 kutokana na utekelezaji mzuri wa Mpango wa II wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2016/17 -2021..

Pato la wastani la kila mtu ni kutoka Sh Milioni 1.6 sawa na Dola 992/2015 kwa mwaka hadi Sh bilioni 2.6 sawa na Dola 1,200.

Amesema uchumi umechochewa na Sekta ya Ujenzi kwa asilimia 25.6, kilimo 19.4 viwanda 9.8 mawasiliano na uchukuzi 8.8. sekta hizo zimechangiwa na sekta ya elimu ambayo hutoa rasilimali watu wanaochangia kuleta tafiti zenye matokeo ya kiuchumi na kiuchumi.


Hata hivyo, amesema sekta  hiyo ya elimu ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kutoa ushauri na utafiti wa kitaalamu kuhusu dira na muelekeo wa jamii na taifa kwa ujumla ili kupata maendeleo endelevu.

Katibu Mkuu huyo amesema mkakati wa kukuza maarifa wa miaka 10 inabidi kuwe na sera maalum ya kukuza ujuzi itakayosimamia malengo na masuala ya kushirikisha sekta binafsi katika kukuza ujuzi na maarifa.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu(TCU), Profesa Charles Kihampa amesema, lengo kuu la maonesho hayo ni pamoja na kutoa fursa kwa taasisi zinazoshiriki kujitangaza kwa kuonesha huduma na kazi mbali mbali wanazozifanya na mchango wao katika kuendeleza jitihada za serikali za kukuza na kudumisha uchumi wa kati kupitia elimu ya juu sayansi na teknolojia.

Amesema kupitia maonesho hayo wananchi na wadau mbali mbali wa elimu wanapata fursa za  kuona shughuli zinazofanywa na taasisi na vyuo vya elimu ya juu na kuwawezesha kuweza kufanya makubaliano ya namna ya kupata huduma za ushauri wa kujiunga na elimu ya juu  kwa kufanya chaguzi sahihi wanapofanya udahili.

"Mwaka huu jumla ya taasisi 73 zimeshiriki kwenye maonesho haya ikilinganishwa na taasisi 67 zilizoshiriki maonesho ya 15 yaliyofanyika 2020, ikiwa ni ongezeko la taasisi sita." Amesema Kihampa.

Aidha, Kihampa amesema,  taasisi zinazoshiriki maonesho ya mwaka huu zinajumlisha taasisi 54 zinazotoa mafunzo ya ngazi ya elimu ya juu, mabaraza ya udhibiti ubora mawili, wakala na taasisi zingine za Serikali  tano, bodi za usajili wa wataalamu tatu, Taasisi za Sayansi Teknolojia na utafiti moja na taasisi za vyama vya kifedha moja na taasisi za wakala wa vyuo vya nje nane.

Naye, Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya vyuo vikuu (TCU), Charles Mgone amesema, tume itabaki kuwa taasisi imara na thabiti hapa nchini  Kikanda na kimataifa,  pia itaendelea kufanya majukumu yake  kwa misingi bora ambayo imeishatayarishwa.

"Tunaahidi kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti ubora wa elimu ya juu na kufanya taasisi zetu za elimu kuwa chachu ya maendeleo ya taifa letu na kuzalisha wahitimu mahiri, wabunifu na wenye uwezo wa kustahimili ushindani wa soko la ajira na changamoto za kijamii na kiuchumi, tume itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuwatumikia watanzania katika sekta hii", Amesema  

Pia, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa amesema, maonesho ya vyuo vikuu yamekuwa msaada mkubwa kwa vijana wanaomaliza masomo kidato cha sita kupata maelezo na namna nzuri ya kutumia vyuo vikuu vilivyopo nchini na mifumo mbali mbali iliyopo ili kujiunga na vyuo hivyo.

"Uwepo wa vyuo vikuu na maonesho haya ni fursa nzuri ya kuonesha kazi ambazo zinafanyika kwenye vyuo hivi na kuwawezesha wanafunzi kujifunza zaidi juu ya elimu ya juu na hata kupata uwezo wa kupata elimu kutoka nje ya nchi kwani navyo vipo hapa na vinatoa huduma". Amesema 

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Katibu Mkuu wa Baraza la Wawakilishi Zanziber Mhandisi Zenna Said akihutubia wakati akifungua rasmi Maonesho hayo leo Julai 27,2021 katika viwanja vya Mnazi mmoja Dar es Salaa.
Makamu mMwenyekiti wa TCU na Makamu Mkuu wa Chuo cha kumbukumbu ya Hurbert Kairuki Prrof. Charles Mgone akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwenye Viwanja vya Mnazimmoja Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Charles Kihampa akitoa hotuba yake ya utangulizi kwenye halfa fupi ya ufunguzi wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na TCU Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Charles Kihampa (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo mbele ya Mgeni rasmi Mhandisi Zenna Said (wa pili kushoto mwenye koti nekundu) alipotembelea Banda la TCU kupata maelezo ya namna Tume hiyo inavyotekeleza Majukumu yake. (kulia) ni Afisa Mwandamizi wa Udhibiti Ubora TCU>
Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa  TCU Hilda Kawiche (kushoto) akimueleza Mgeni rasmi Mhandisi Zenna Said namna ambavyo Tume hiyo inatekeleza Majukumu yake ya kudhibiti ubora wa Viwango vya Elimu inayotolewa na Vyuo Vikuu mbalimbali hapa nchini.
Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa  TCU Hilda Kawiche (kushoto) akimueleza Mgeni rasmi Mhandisi Zenna Said namna ambavyo Tume hiyo inatekeleza Majukumu yake ya kudhibiti ubora wa Viwango vya Elimu inayotolewa na Vyuo Vikuu mbalimbali hapa nchini.
Picha ya Pamoja ya Watumishi wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) wakiwa kwenye Banda lao katika siku maalum ya ufunguzi wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofunguliwa rasmi leo Julai 27,2021 Jijini Dar es Salaam.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...