Kampuni ya SGA Security imeahidi kuendelea kuunganisha wakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia michezo huku ikidhamini safari maalumu ya baiskeli ijulikanayo kama ‘the Great African Cycling safari’ itakayoshirikisha nchi tano za Afrika Mashariki.  

Safari hiyo ilianzia Jijini Dar es Salaam mapema wiki hii na kuzinduliwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mh. Mbarouk Nasser Mbarouk ambaye aliongozana na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mh. Dan Kazungu na wadau wengine.

Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Security, Eric Sambu alisema ni heshima kubwa kwa kampuni yake kudhamini tukio kubwa kama hilo ambalo litadumu kwa siku 55 na wataendesha urefu wa kilometa 6000 katika nchi hizo tano.
Alisema waendesha baiskeli hao watavuka kuingia nchini Kenya kupitia Tanga, kisha kuelekea Mombasa, Nairobi, Kampala, Kigali, Bujumbura, Dodoma na hatimaye kumalizikia Arusha ambayo ndio makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema kampuni ya SGA pia itasindikiza msafara huo na kutoa huduma za ulinzi huku ikilenga kuunganisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na pia kuangalia namna ya kuimarisha biashara kati ya nchi hizi bila vikwazo.
 “Ni jambo zuri kuona waendesha baiskeli kutoka nchi hizi wakisafiri pamoja huku kukiwa na shughuli mbalimbali zimeandaliwa katika maeneo mbalimbali watakayopita,” alisema na kuongeza kuwa wananchi wa Afrika Mashariki wanalo jukumu la kulinda amani na utulivu na kwamba uendeshaji wa baiskeli utasaidia katika kuhakikisha afya njema na kupunguza maradhi. 
 
Alisema timu ya SGA katika kila nchi itapokea msafara huo katika mipaka husika na kuongozana nao hadi mpaka unaofuata kama njia ya kuonesha umoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema tukio hilo pia litatumika katika utunzaji wa mazingira kwani waandaaji wameandaa shughuli mbalimbali za upandaji miti katika maeneo mbalimbali watakayosimama.

Kwa mujibu wa Bw. Sambu kampuni yake inaifahamu vizuri Afrika Mashariki kuliko kampuni nyingine yoyote kwani wana magari zaidi ya 800 katika ukanda huu.  
“Tunasafiri zaidi ya km 12,000 kila siku kuimarisha biashara katika ukanda huu. Katika kila shilingi inayoguswa Afrika Mashariki angalau senti 80 huwa imesafirishwa na SGA,” alisema na kuongeza kuwa SGA imeajiri zaidi ya wafanyakazi 19,000 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki hivi kuifanya kampuni kubwa zaidi ya ulinzi.

SGA Security inatoa huduma mbalimbali ikiwemo za ulinzi, alarm, huduma za fedha, ulinzi wa kielektroniki, huduma ya kusafirisha mizigona huduma nyinginezo na  ndio kampuni pekee ya ulinzi yenye cheti cha ISO 18788 – Security Operations Management System.

Mwaka huu kampuni hiyo ilipokea tuzo baada ya kutangazwa mshindi wa jumla kama kampuni yenye rasilimali za kutosha na ya kuaminika  (Most Equipped and Reliable Security Company of the Year, 2020) katika tuzo za chaguo la wateja (Consumer Choice Award).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...