Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesisitiza kwamba itaendelea kufanya jitahada mbali mbali katika kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika nyanja zote za uchumi na kutoa wito kwa wadau kutoa mchango wao katika kuwawezesha watu wenye ulemavu hususan watoto wadogo ili waweze kupata elimu na malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao na hatimaye kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Watu Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, alipokuwa akikabidhi vifaa mbali mbali vya msaada katika shule za watu wenye ulemavu ambavyo vimetolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amesema watoto wenye ulemavu wana uwezo mkubwa ambao hautofautiani na watu wasiokuwa na ulemavu hivyo endapo watalelewa vizuri na kupata elimu stahiki wanaweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

“Niwashukuru OSHA kwakushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kufanya ziara katika shule tatu za watoto wenye ulemavu. OSHA imekuwa ni taasisi ya faraja sana kwa watu wenye ulemavu kwani katika kile kidogo wanachokipata wameona ni vema wakashirikiana nami na Ofisi nzima ya Waziri Mkuu kuja kuwatembelea hawa watoto. Hivyo, binafsi nimefarijika sana,” amesema Naibu Waziri huyo wa Nchi anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu na kuongeza;

“Natamani kuona watu wenye ulemavu wanajumuishwa ipasavyo katika sekta zote na ndio maana nimekuwa nikipita katika maeneo mbali mbali ikiwemo ajira, elimu, afya, uchumi ili kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata nafasi katika kila fursa inayotokea na katika mipango mbali mbali ya serikali.”

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema serikali itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo zikiwemo Taasisi, Asasi zisizo za kiserikali, makampuni na watu binafsi katika kuwawezesha watu wenye ulemavu ili nao waweze kutoa machango wao katika kuijenga nchi yao.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, ambao ndio wameandaa vifaa hivyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, amesema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taasisi yake wa kusaidia jamii kwenye sekta za elimu, afya, majanga na uboreshaji wa mazingira ya kazi.

“Sisi tumekuja katika shule hizi za watu wenye ulemavu kwa ajili ya kutoa faraja kwa wanafunzi na watumishi wenzetu ambao wanafanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi na vihatarishi vingi vikiwemo vihatarishi vya kisaikolojia hivyo wanahitaji kutiwa moyo ili waendelee kuifanya kazi hii ambayo kimsingi ni kazi kubwa na muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Aidha, wanafunzi na viongozi wa baadhi ya shule zilizopatiwa msaada wa vifaa hivyo, wameishukuru Taasisi ya OSHA kwa msaada uliotolewa na kuwaomba wadau wengine kuendelea kusaidia kutatua changamoto mbali mbali zinazozikumba shule za watoto wenye ulemavu.

“Binafsi nimefarijika sana kwasababu sikujua kuwa OSHA watakuja kwani walinipigia tu simu wakiniuliza changamoto tulizonazo hivyo namshukuru sana Naibu Waziri Ummy ambaye kwakushirikiana na OSHA wameona waje watutembelee na kutuletea zawadi. Kiukweli mahitaji waliyotuletee ni ya muhimu sana kwetu na hatujawahi kuwa nayo tangu shule hii ilipoanzishwa kwa mfano wametuletea vifaa vya kuzimia moto na kompyuta ambayo itatusaidia sana katika kuandaa mitihani ya wanafunzi,” alisema Kajika Gallan, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazinyungu.

Msaada huo wenye thamani ya takribani milioni 15 ambao ulihusisha ukaguzi wa usalama na afya hususan katika mabweni ya wanafunzi, umetolewa katika shule za za msingi za watoto wenye ulemavu za Uhuru Mchanganyiko ya Ilala-Dar es Salaam, Mazinyungu ya Kilosa-Morogoro na Buigiri ya Chamwino-Dodoma. Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na; kompyuta, vifaa vya kuzimia moto, taulo za kike, vifaa kinga, vifaa vya usafi, karatasi na vibao maalum ya kuandikia watu wenye ulemavu.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda (mwenye kiremba chekundu) akishiriki zoezi la kugawa chakula kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri Wasioona, ambacho kiliandaliwa sambamba na msaada wa vifaa mbali mbali vilivyokabidhiwa katika shule hiyo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga. Viongozi hao walishiriki chakula hicho pamoja na wanafunzi, walimu na watumishi wengine wa shule hiyo.

Mkaguzi wa Usalama wa Umeme wa OSHA, Mhandisi Maria Ndaskoy, akifanya ukaguzi wa mifumo ya umeme katika bweni la shule ya Uhuru Mchanganyiko iliyoko Wilayani Ilala Mkoani Dar es Salaam wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga na Mtendaj Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda kwa lengo la kutoa vifaa wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga akishiriki chakula cha mchana pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri Wasioona ambacho kiliandaliwa sambamba na msaada wa vifaa mbali mbali vilivyokabidhiwa katika shule hiyo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga. Viongozi hao walishiriki chakula hicho pamoja na wanafunzi, walimu na watumishi wengine wa shule hiyo.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga (watatu kushoto) na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (wapili kushoto) wakikabidhi vifaa mbalimbali vya msaada kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazinyungu ya Kilosa, Morogro, Kajika Gallan, wakati wa ziara ya kukabidhi msaada wa vifaa wezeshi kwa watoto wenye mahitaji maalum katika shule tatu za Msingi zilizopo Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...