Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Kigoma Mathius Mwenda kuhakikisha mradi wa maji wa Kifura Wilayani Kibondo unakamilika ifikapo Februali mwakani. Mhe. Majaliwa ametoa agizo hilo jana Septemba 17, 2021 alipotembelea na kukagua mradi huo ambao unatarajia kuwanufaisha wananchi wapatao 12,095 wa kijiji cha Kifura.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan analenga kuhakikisha kila mtanzania anafikiwa na huduma ya majisafi na salama, hivyo watendaji wa serikali wanapaswa kusimamia hilo.

“Mama Samia amedhamiria kupeleka Maji kwa kila Mtanzania. Anafaham jinsi akinamama, vijana na watanzania wote wanavyohangaika kutembea kwa miguu, bodaboda na baiskeli wakiwa na madumu ya maji. Kwa hiyo anafanya kila njia kuhakikisha huduma hii inamfikia kila Mtanzania” Amesema Mhe. Majaliwa

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Kigoma Mathius Mwenda amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi M/s NANGAI Engineering and Contractors Co. Ltd kwa Gharama ya EUR 880,256.54 sawa na shilingi Bilioni 2,405,741,123.83 za Kitanzania.

Amesema fedha yote ya utekelezaji wa mradi ipo, hivyo hana mashaka kwamba mradi huo utakamilika kwa wakati.

Amewataka wananchi wanaohitaji kuunganishwa maji majumbani mwao wajitokeze. Aidha, amesema mradi huo una vituo vya kuchotea maji 50 ambavyo vitasaidia kuondoa kabisa changamoto ya Maji katika kijiji hicho.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amempongeza Rais Samia kwa kuimarisha mahusiano na nchi za nje. Amesema mahusiano hayo mema ndio yamewezesha Serikali ya Ubelgiji kusaidia utekelezaji wa mradi huo. Amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati.

Mradi wa maji Kifura ni moja ya miradi ambayo inatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ubelgiji mkoani Kigoma.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...