Rais wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu,  (TAPIE), Mahmod Mringo akimlisha keki Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Albert Katagira mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika jana Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Rais mpya wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu,  (TAPIE), Mahmod Mringo akikata keki mwishoni mwa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika jana. Kulia ni Mweka Hazina wa chama hicho, Shani Khalfan Swai (CPA)

Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu (TAPIE), kimemchagua Mkurugenzi wa shule za Paradigms Mahmoud Mringo kuongoza chama hicho kwa muda wa miaka mitano.

Mringo na Kamati ya Utendaji wote wamepita bila kupingwa kwenye uchaguzi uliofanyika kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika leo Oktoba 28,2021 jijini Dar es Salaam.

Wengine waliochaguliwa bila kupingwa ni Makamu wa Rais wa chama hicho, Chacha Wambura ambaye ni Mkurugenzi wa shule zaa WAJA, Katibu Mkuu Dk. Albert Katagira ambaye ni Mkurugenzi wa shule za Tusiime na Mweka Hazina ni Shani Khalfan Swai (CPA), Mkurugenzi wa shule ya Baobab Mapinga Bagamoyo.

Akizungumza mara baada ya kupitishwa, Mringo amesema atafanya mabadiliko makubwa kuiwezesha taasisi hiyo kuwa imara na kuwa mtetezi wa wamiliki wa shule ambao amesema wanabakiliwa na changamoto mbalimbali.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid amewataka wamiliki wa shule binafsi zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali kuziwasilisha serikalini ili zipatiwe ufumbuzi.

“Semeni nini mnataka serikali iwafanyie sisi tuko tayari kupokea changamoto zenu na kuzifanyia kazi na mengine makubwa tutayapeleka sehemu husika kwaajili ya kupatiwa ufumbuzi,” Amesema

Pia amewataka wamiliki wa shule hizo kuziendesha kwa kufuata sheria za nchi kwa kuhakikisha zimesajiliwa na kupata vibali vyote vinavyohitajika kwa ajili ya usajili.

Amesema serikali inawajali na kuwathamini sana wamiliki wa shule binafsi kwani wamekuwa wakipata changamoto kama ambazo maofisa wa elimu wamekuwa wakizipata hivyo wanachotakiwa kufanya ni kushirikiana kwaajili ya kuzitatua.

“Nyinyi mnapata changamoto kama sisi tunavyopata changamoto sasa naomba niwaambie changamoto zangu kwenu nanyinyi mtaniambia za kwenu cha muhimu endesheni shule zenu kwa kufuata sheria,” alisema.

Afisa Elimu huyo amesema, changamoto nyingine ni tabia ya baadhi ya shule ambazo zimekuwa zikitumia mbinu mbalimbali kuiba mitihani kwa lengo la kufaulisha wanafunzi wengi .

Aidha amewataka wamiliki wa shule hizo kukomesha tabia hiyo na kusimamia vizuri walimu wao waweze kufundisha kwa viwango ili waweze kufaulu bila kutumia njia haramu za wizi wa mitihani ambayo itawasababishia matatizo.

Amesema mkoani Dar es Salaam kuna baadhi ya shule binafsi ambazo zimekuwa zikisua sua kutokana na uhaba wa fedha na kuwataka kwenda kukopa CRDB kama ambavyo wameahidiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo.

Amewataka wamiliki hao kuzitangaza shule zao zinapopata matokeo mazuri au huduma bora zinazopatikana lakini wasitumie mbinu chafu ambazo zinasababisha maumivu kwa watu wengine.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...