Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye  atembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR kipande cha Dar Es Salaam – Morogoro  kwa kutumia treni ya uhandisi kutoka stesheni ya SGR Pugu hadi Kwala mkoani Pwani  hivi karibuni 23 Oktoba, 2021.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Burundi  Mhe. Evariste Ndayishimiye  yupo nchini Tanzania katika ziara ya kikazi yenye lengo la kuimarisha uhusiano baina ya nchi ya Tanzania na Burundi.

Rais Ndayishimiye alipata taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa reli ya Kisasa - SGR kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa na kushuhudia ujenzi ulivyokamilika kwa asilimia 94 huku akitembea kwa treni ya uhandisi kutoka stesheni ya pugu mpaka Kwala, mkoani Pwani ambapo alitembelea eneo la hekta 10 ambalo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipatia Serikali ya Jamhuri ya Burundi ili kurahisisha shughuli za usafirishaji.

Mara baada ya kufika eneo la bandari kavu Kwala mkoani Pwani, Rais Ndayishimiye alitoa shukurani za dhati kwa niaba ya wananchi wa Burundi kwa zawadi kubwa ya ujenzi wa reli ya kisasa - SGR pamoja na Serikali ya Tanzania kutoa eneo la bandari kavu kwa ajili ya nchi ya Burundi, ambapo amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo  itasaidia kujenga uhusiano mzuri  wa sekta ya biashara, uchumi na viwanda kati ya Burundi  na Tanzania.

‘’Warundi wamepata zawadi kubwa  mbili kwanza ni hii reli ya kisasa – SGR, Burundi tulikuwa tunasumbuka sana wafanyabiashara wakitaka kusafirisha bidhaa zao kuleta Buurndi kutoka Dar es Salaam wamekuwa wakitumia muda mwingi pamoja hivyo reli hii ni zawadi kubwa sana kwetu na tutaimarisha uhusiano wa biashara kupitia reli hii. Nimeambiwa kuwa reli ya kisasa itafika kwa siku 1, hivyo bei ya malighafi kwa nchi ya Burundi itapungua’’ alisema Mhe. Rais.

Hata hivyo Rais Ndayishimiye aliweka wazi namna reli ya kisasa itakavyochagiza maendeleo kwa kuokoa muda pamoja na umbali,  ‘’Reli itatusaidia kusafirisha bidhaa mbalimbali kwa haraka, salama na bei nafuu. Hapo mwanzo tulikuwa tunatumia gharama kubwa za usafirishaji lakini kwa sasa tutalipa gharama kidogo na hizo pesa tutakuwa tumeziokoa na kwenda kuwekeza kwenye miradi mingine’’ aliongeza Mhe. Rais.

Naye, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi  Prof. Makame Mbarawa  ameeleza namna Serikali ya Tanzania inavyotekeleza diplomasia ya uchumi kwa kushirikiana kibiashara na nchi jirani za Afrika katika  usafirishaji wa mizigo ambao utakuwa ni tija katika ukuaji wa uchumi nchini Tanzania na barani Afrika.

‘’Kwa upande wa reli bandari hii kavu ya Kwala itaunganishwa kwa reli za aina mbili, kwanza ni reli zamani – MGR, pili reli ya kisasa – SGR. Na kwa sasa tumeanza kujenga jumla ya Kilomita 1.3 zimekwisha kujengwa na zimegharimu milioni 434’’ alisema Waziri Mbalawa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa alibainisha kuwa lengo la mradi huu wa SGR ni kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na nje ya nchi kwa wingi na kwa muda mfupi ili kukuza uchumi wa Tanzania kwa kuziunganisha bandari na nchi jirani ambazo hazina bahari.















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...