Na Seif Mangwangi, Arusha 

ULAJI wa hovyo wa vyakula bila kuzingatia vyakula lishe umeelezwa kuwa chanzo cha ugumba kwa wanaume na wanawake pamoja na maradhi yasiyoambukiza kwa vijana wadogo walio katika umri wa balahe.

Ili kudhibiti hali hiyo, wazazi na walezi nchini wametakiwa kuzingatia chakula chenye lishe kwa vijana wenye umri wa kwenda shule na vijana balehe ili kuwajenga kiakili na mwili na kuwaepusha na maradhi yasiyoambukiza.

Akizungumza wakati wa kufunga mdahalo wa watoto wenye umri wa kwenda shule na vijana balehe kuhusu mifumo ya chakula, ulioandaliwa na taasisi ya serikali ya Chakula na Lishe Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dk.Silvia Mamkwe amesema hali ya afya kwa watoto hivi sasa ni ya hatari sana.

Amesema  wazazi wengi hujisahau na kuwapa watoto wao vyakula visivyokuwa na tija na kuwasababishia udumavu na upungufu wa damu kwa baadhi yao.

Dkt.Mamkwe amesema katika utafiti uliofanywa nchini kati ya watoto 100 watoto 34 wanaugua tatizo la upungufu wa damu huku kati ya watoto100 watoto 25 wanakabiliwa na tatizo la udumavu na kuwasababishia kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kuhimili masomo.

"Utafiti unaonyesha kuna hali ya hatari sana ya kiafya kwa watoto wetu, kati  ya kila  watoto 100 shuleni, watoto 34 wanakabiliwa na upungufu wa damu,kila kwenye watoto 100 watoto 25 wanakabiliwa na udumavu na  kila kwenye idadi ya watoto 100 watano wanauzito uliozidi,"amesema.

Amesema hali hiyo inachangiwa na changamoto mbalimbali za mfumo wa uzalishaji,uhifadhi na usindikaji wa chakula,masuala ya masoko,upatikanaji wa chakula na ulaji usiofaa.

Dk.Silvia  amesema  hali si nzuri kwa maeneo ya vijijini hivyo kuna haja ya kuhamasishana na kusabambaza elimu ya lishe kwenye jamii ili wazazi na walevi wabadilike.

"Wengi tunafurahi kumpa mtoto chips ni kumpenda kijana au mtoto kumbe tunamuharibu na matokeo yake anapokuwa kijana anakosa nguvu  za kuzaa  na  tunaishia kununulia dawa za kuongeza nguvu wakati ukimpa chakula lishe anajengeka kiafaya,akili na mwili,"amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Chakula na Lishe nchini,Dk.Germana Leyna  amesema tatizo la utapiamlo uliozidi upo baadhi ya mikoa na Arusha inaongoza katika eneo hilo kutokana na sababu ya ukosefu wa chakula chenye lishe.

Amesema kutokana na kuona ongezeko la udumavu na upungufu wa damu kwa watoto wenye umri wa kwenda shule na vijana balehe, wameamua kuendesha mdahalo huo na kukusanya baadhi ya vijana pamoja na wazazi wao,toka mikoa  mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani ili kutoa elimu ya masuala ya lishe.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dk.Silvia Mamkwe akizungumza na wanafunzi wenye umri wa kwenda shule na vijana balehe pamoja na walezi waliofika kwenye mdahalo kuhusu mifumo ya chakula ulioandaliwa na taasisi ya chakula na lishe.

Wanafunzi wenye umri wa kwenda shule na vijana balehe kutoka katika shule mbalimbali nchini wakisikiliza hotuba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakati wa kufunga mdahalo wa majadiliano kuhusu lishe bora kwa afya ya binaadam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...