Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kufufua Kamati za UKIMWI ngazi ya Vijiji, Mitaa na Kata na utendaji wa Kamati hizo pamoja na kutenga Bajeti kwa ajili ya Utekelezaji wa jukumu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kundi hilo linahudumiwa vizuri.

Mhe. Senyamule amesema hayo leo Disemba 01, 2021 wakati alizungumza na wananchi kwenye viwanja vya Uyovu Wilayani Bukombe wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani Mkoa wa Geita. 

Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka Viongozi na wanachama wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (KONGA) kuendelea kuhamasisha WAVIU wajiunge na KONGA na kuwa wafuasi wa dawa za kufubaza makali ya VVU na kufuata maelekezo yanayotolewa na watoa huduma za afya majumbani na wataalamu wa afya ikiwemo kuzingatia elimu ya lishe bora.

Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi dhidi ya janga la Ugonjwa wa Uviko 19.

"Napenda kuwahamasisha kutafakari kwa kina na kuhihiari kupokea chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19 na kutumia njia zote za kujikinga zinazotolewa na wataalamu wetu wa Afya," amesema.

Akisoma taarifa ya Mkoa ya hali ya Utekelezaji wa shughuli za napambano dhidi ya  Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Ndugu Erikana Haruni amesema jumla ya watu 175,206 (Wanawake 107,382 sawa na asilimia 61 na Wanaume 67,824 sawa na asilimia 39) walichukuliwa sampuli ya damu katika vituo na mikusanyiko mbalimbali kwa ajili ya kupimwa maambukizi ya VVU. Kati ya hao, watu 10,823 (sawa na 6% ya wote waliopimwa) walibainika kuwa na maambukizi ya VVU. Kati ya hao Wanawake walikuwa 6,284 (sawa na 58%)  na Wanaume walikuwa 4,539 (sawa na 42%).

"Kwa mama wajawazito, jumla ya wajawazito 107,961 walipatiwa huduma ya ushauri nasaha na kupimwa VVU katika hudhurio la kwanza Kliniki. Kati ya hao, akina mama wajawazito 739 (sawa na asilimia 0.7%) waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU na kuanzishiwa dawa za  kufubaza makali ya VVU (ARVs)." Amesema Haruni.

Aidha, amesema Mkoa wa Geita kama ilivyo kwa Taifa na dunia umeendelea kuwa sehemu ya ufanikishaji wa lengo la dunia la kuhakikisha ifikapo 2030 tunatokomeza kabisa maambukizi mapya ya VVU, unyanyapaa na ubaguzi na vifo vitokanavyo na UKIMWI. Shughuli ambazo zimekuwa zikifanyika ni pamoja na kuelimisha jamii kujikinga na maambukizi ya VVU, kuepuka imani potofu kuhusu VVU/UKIMWI, kuepukana na unyanyapaa, kuingia kwenye matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI ili kuimarisha afya, kubaini na kuhamasisha wadau waliomo kuchangia rasilimali fedha na vifaa tiba dhidi ya VVU/UKIMWI. 

Aidha, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa Ndugu Leonidas Felix ameitaka jamii kuacha kujihusisha na rushwa ya ngono anbayo ni kisababishi kikubwa cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwenye jamii. 

Akisoma Risala, Ndugu Mashauri Charles amesema ulevi kupita kiasi, unyanyapaa, shughuli za machimboni na tabia hatarishi za uasherati zimekua chanzo kikubwa cha kuenea kwa maradhi ya Ukimwi na kusababisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...