Na Beda Msimbe
TAMTHILIA ya Jua kali juzi katika Tuzo za kwanza
za taifa za filamu ilizoa tuzo nane ikiwamo tuzo ya muigizaji bora wa
kike iliyotwaliwa na Godliver Godian, darekta bora wa kike Leah
Mwandamseke, muigizaji bora wa kiume na kike wa kwa chaguo la
watazamaji.
Tuzo za chaguo la watazamaji liliwafikia waigizaji
watamthilia hiyo ambayo pia ilipata tuzo ya tamthilia bora ni Iddy
Kapalata na Maria George. Tuzo nyingine za Jua Kali ni Tuzo za muziki
bora wa filamu, Tuzo bora ya mfumo wa uzalishaji na muigizaji msaidizi
bora wa kike iliyokwenda kwa Hellen Herman.
Aidha filamu bora
ilienda kwa sinema ya Obambo ambayo pia ilitwaa tuzo ya muigizaji bora
iliyokwenda kwa Isarito Mwakalindile, sinematografia bora na athari
maalumu iliyokwenda kwa Ochu na RamarKing na kuwafanya wawe na tuzo
nne.
Aidha katika uitoaji huo wa tuzo Waziri wa Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Innocent Bashungwa alipokea Tuzo ya Heshima kwa Niaba ya
Rais wa Tanzania,Samia Suluhu kwa kutambua mchango wake wa kuiendeleza
Tasnia ya Filamu nchini ikiwemo "Royal Tour".
Akizungumza wakati
wa utoaji wa tuzo hizo juzi usiku Bashungwa ametoa wito kwa mikoa yote
nchini kuiga Mkoa wa Mbeya katika kushirikiana na Wizara yake kuandaa
Tuzo za Filamu katika miaka ijayo ili kukuza vipaji na kutoa ajira kwa
wasanii wengi zaidi walio kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini.
Katika tuzo hizo zilizoratibiwa na Bodi ya Filamu chini ya usimamizi wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Waziri Bashungwa
alisema
Serikali imeshatenga kiasi cha Sh bilioni 1.5 kwenye mfuko wa Maendeleo
ya Sanaa na Utamaduni kwa ajili kukuza na kuendeleza shughuli za
Utamaduni na Sanaa ikiwa ni pamoja na Filamu.
“Ninawajulisha kuwa
tuzo hizi ni endelevu, hivyo ninawakaribisha wadau wote wenye nia ya
kushirikiana na Serikali kwa mwaka 2022.”
Akizungumzia mchakato
wa sinema hizo Waziri alisifia sana mchakato ulivyokwenda na kusifia
jinsi Tuzo zilivyoweza kuinua vipaji.
Alisema serikali imeanza mwaka huu kwa kutambua nafasi ya tasnia hii kuitambulisha nchi yetu.
Kwa
kutambua Mchango wao Mkubwa kwenye Sekta ya Filamu Nchini,Picha za
Wasanii Wa Filamu waliotangulia mbele za haki King Majuto,Sharo
Milionea,Sajuki na Steven Kanumba ziliwekwa ndani ya Ukumbi wa Tughimbe
zilizokofanyika tuzo.
Akizungumza katika mahojiano baada ya tuzo
hizo, Mwenyekiti wa Jopo la Majaji 7 waliohakiki sinema hizo, Profesa
Martin Mhando alisema kama majaji waliipa filamu ya Janga tuzo kwa
kuwa ni filamu inayoonesha mwelekeo chanya wa tasnia.
Alisema sinema hiyo ya Ben Royal inabidi itazamwe kwa jicho la kipekee kutokana na uhamasishaji wake.
Janga ni filamu iliyoandikwa na John Kokolo ambaye ndiye pia aliyeigiza mhusika Mkuu, ni hadithi inayozungumzia suala la Maji.
"Dhamira
hii ni nzito. Ni filamu ambayo kote duniani inaweza kutazamwa kwa hamu
na kuzungumza kwa jinsi inavyolizungumzia Janga la kukosekana kwa maji.
Uigizaji wake, mazingira, mandhari na hisia zinazooneshwa zinamkamata
mtazamaji kikwelikweli.
Lakini muhimu zaidi ni kuwa filamu inatumia
mfumo (genre) ya kusisimua (action) ambayo ndiyo inayouza zaidi duniani
lakini sisi Tanzania hatujaweza, au tukiifanya inakuwa kama tunanakili
hadithi za wenzetu"alisema Profesa Mhando.
Anasema kwamba jopo
imeangalia na kuona kwamba Janga ni hadithi inayoakisi mazingira ya
Kiafrika ingawa ni dunia aliyoibuni mwandishi.
"Tuna matamanio
makubwa ya kuona filamu za kibunifu kama hizizikishamiri nchini. "
anasema profesa huyo ambaye alisema amefurahi jinsi wasanii walivyopokea
matukio hayo.
Akizungumzia tathmini yake kama mtaalamu wa
masuala ya filamu alisema filamu nyingi bado zina matatizo ya kutamba na
hadithi nyepesi na kusema zile zilizojaribu kumzungumzia masuala mazito
zimeonesha upana wa mawazo na uwezo kitaaluma.
"Filamu
iliyoshinda kama filamu Bora- inayotwa Obambo ni filamu inayoonesha
umahiri kitaaluma kwa kutumia mfumo (genre) ya kitaaluma ya filamu za
kutisha. Hapa tumeona ufahamu mkubwa wa dhamira nzito, uwezo wa uigizaji
lakini zaidi Dairekta aneonesha ufundi wa hali ya juu ya kutamba na
hadithi ya filamu." anasema Profesa Mhando katika mahojiano.
Aidha
alisema tamthilia zilizooneshwa zimeonesha ubora katika ufundi
(techniques) lakini hadithi zinazotamba ni za kawaida mno kiasi cha
kutoweza kuvuka mipaka ya nchi japo ikafika Afrika Mashariki.
"Lazima
tutumie ufundi wa waigizaji wetu kutamba hadithi zinazoweza kukamata
watazamaji wa kimataifa. Hilo ni suala la kuangalia na tasnia nzima
ikiwa ni pamoja na stesheni za TV kama Azam ambao wakiweza kuwahamasisha
kwa kuinua upana wa hadithi na kuwaongezea fedha na muda wa kutengeneza
hizo tamthilia. " alisema.
Anasema bila kufanya hivyo tamthilia
zetu zitaduma na mwisho wenzetu wa Kenya watakuja kutupiku maana suala
kubwa hapa ni tasnia kuifikia hadhira pana ya watazamaji wa tamthilia za
Kiswahili.
Wakati huo huo Zaizbar imepanga kumpokea kwa kishindo
msanii pekee aliyeshinda tuzo ya filamu ya Taifa kupitia filamu ya
Urithi wa Mila, Mudi Sule.
Wananchi wameombwa leo kuhakikisha
kwamba wanakusanyika katika viwanja vya Binti Hamran saa nne kwa ajili
ya kumpokea shujaa wao huyo na wasanii wote ambao walikwenda Mbeya
kushiriki tuzo hizo.
Ifuatayo ni orodha kamili ya washindi
1. Filamu Fupi Bora (BEST SHORT FILM)
MWANDISHI
2. Filamu bora ya kikaragosi (BEST ANIMATION FILM)
NIVUSHE
3. Filamu Bora ya Dokumentari (BEST DOCUMENTARIES)
URITHI WA MILA
4. Filamu bora ya Ucheshi (BEST COMEDY)
SALUNI YA MAMA KIMBO
5. Tamthilia bora ya Ucheshi (COMEDY SERIES (ONLINE/TV)
KITIM TIM
6. Mcheshi Bora (BEST COMEDIAN)
MCHUZI JUU (JOTI) - LUCAS LAZARO MHUVILE
7. Tamthilia Bora (BEST SERIES)
JUA KALI
8. Filamu Bora Ndefu (BEST FEATURE FILM)
OBAMBO
9. Sinematografia Bora (BEST CINEMATOGRAPHY)
OBAMBO – FREDDY FERUZI
10. Uhariri Bora (BEST EDITING)
JANGA - BERNARD EDSON (BEN ROYAL)
11. Mfumo bora wa sauti (BEST SOUND DESIGN)
MGENI – VINONDO RECORDS
12. Muziki bora wa Sinema (BEST MUSIC SCORE)
JUA KALI – SELEMANI MASENGA & SWITCH MUSIC GROUP
13. Ubunifu Bora wa maleba (BEST COSTUME DESIGN)
JANGA – BERNARD EDSON (BEN ROYAL)
14. Mfumo bora wa Uzalishaji (BEST PRODUTION DESIGN)
JUA KALI – FLORANCE G. MKINGA
15. Muonekano Bora wa Eeneo (BEST SET DESIGN)
NYARA – ELIUD DOMINIC & KIFUA COMPOUND
16. Ubunifu bora wa Grafiki (BEST GRAPHICS DESIGN)
NYARA – ELIAS KINOGO (Destro)
17. Athari bora maalumu (BEST SPECIAL EFFECTS MAKEUP)
OBAMBO – OCHU KIOTA & RAMAR KING
18. Uchezaji skrini Bora (BEST SCREEN PLAY)
JANGA - BERNARD EDSON (BEN ROYAL)
19. Darekta bora wa Kike (BEST FEMALE DIRECTOR)
JUA KALI - LEAH MWENDAMSEKE
20. Darekta Bora wa Kiume (BEST MALE DIRECTOR)
JANGA – BEN ROYAL
21. Muigizaji Bora wa Kiume (BEST ACTOR)
OBAMBO – ISARITO MWAKALINDILIE
22. Muigizaji bora wa Kike (BEST ACTRESS)
JUA KALI – GODLIVER GODIAN
23. Muigizaji Bora Msaidizi wa Kike (BEST SUPPORTING ACTRESS)
JUA KALI – HELLEN HERMAN
24. Muigizaji Bora Msaidizi wa Kiume (BEST SUPPORTING ACTOR)
HAIKUFUMA – HUSSEN LUGENDO
25. Muigizaji Bora anayechipukia wa kike (BEST UPCOMING ACTRESS)
BANTU – BRENDA MALEMBEKA
26. Muigizaji Bora anayechipukia wa kiume (BEST UPCOMING ACTOR)
HAIKUFUMA – SADAM NAWANDA
27. Muigizaji Bora wa Kiume chaguo la watazamaji (BEST ACTOR AUDIENCE CHOICE)
JUA KALI – (IDDY KAPALATA) MOHAMEDY KINGARA
28. Muigizaji Bora wa Kike chaguo la Watanzamaji (BEST ACTRESS AUDIENCE CHOICE)
JUA KALI – (MARIA GEORGE) MARIANNE MDEE
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...