Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo amelazimika kufanya mabadiliko ya hotuba yake wakati wa utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri sana katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT).

Profesa Mkumbo ameamua kubadilisha hotuba yake baada ya kushuhudia mambo makubwa yaliyofanywa na wanafunzi wa DIT ambao kwa kupitia elimu waliyoipata katika taasisi hiyo wamebuni na kutengeneza mitambo na vifaa  ambavyo vinakwenda kujibu changamoto zinazoikabili jamii ya Watanzania .

Miongoni mwa vifaa ambavyo ameshudia Profesa Mkumbo ni pamoja na baiskeli maalum inayomuwezesha mtu mwenye ulemavu wa miguu  kukitumia na akaendelea na majukumu yake.

Pia ameshudia mashine inayotumika  kupima mapigo ya moyo na kisha kutunzwa kwa kumbukumbu kwa muda wote ambao mgonjwa atakuwa akipatiwa matibabu.Mbali na mashine hiyo ameshuhudia mashine ya kupima ulevi mwilini na kutoa taarifa kupitia mtandao wa simu ya mkononi .Aidha mashine inayotumika kuchuja maji yenye chumvi ili yatumika kwa kunywa huku wanafunzi wakionesha kifaa cha kuzalisha umeme unaotokana na jua ambacho kifaa hicho kinauwezo wa kufuata muelekeo wa jua.

Akizungumza kabla ya kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri sana ,Profesa Mkumbo amesema hivi" Nilikuwa nimeandaa hotuba yangu lakini kwa mambo makubwa niliyoshuhudia hapa nimeamua kubadilisha hotuba yangu, vijana wameonesha kwa vitendo jinsi ambavyo wamepikwa katika ubunifu na ujuzi.

"Nilichokiona wakati natembelea maonesho kuona ubunifu uliofanywa na wanafunzi wa DIT ndio hayo ambayo tunahitaji kwa ajili ya kujibu changamoto zilizoko katika jamii,kuna baiskeli imetengenezwa na mmoja ya wanafunzi ambayo inaweza kumsaidia mwalimu mwenye ulemavu kufundishana kuandika ubaoni.

"Nimevutiwa sana na ubunifu, niombe DIT ninyi mbakie katika sayansi na teknolojia,msihangaike na mambo mengine,hayo waachieni wengine waendelee nayo, tunawategemea katika eneo hili la teknolojia.

"Niwaahidi tutaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana katika kukuza ujuzi na ubunifu huu,Wizara ya Viwanda na Biashara tunahitaji sana kuona watalaamu wakiendelea kuzalishwa na DIT,"amesema Profesa Mkumbo.

Kuhusu tuzo na zawadi ambazo zimeandaliwa na DIT na kukabidhiwa kwa wanafunzi waliofanya vizuri sana,Profesa Mkumbo amewapongeza kwa kuwatambua wanafunzi hao kwani hiyo inatia hamasa na heshima kwa wahusika ,hivyo kuendelea kufanya makubwa zaidi 

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kuanzia mwaka 2022, Wizara ya Viwanda na Biashara  itaanza kutoa tuzo  kwa mwanafunzi aliyebuni mfumo, nyenzo au kifaa kitakachotatua changamoto ya kijamii au binadamu.

Kuhusu ushauri wake kwa wanafunzi amewaomba kuwa wavumilivu katika kutafuta mafanikio kwani hayaji mara moja na hata wakipata ajira wajitahidi kukaa eneo moja kwa muda mrefu kwani wengi wao hawakai sehemu moja na hiyo ni changamoto ambayo waajiri wanailalamikia.

 "Wenzetu mkipata kazi hamtulii na wenye viwanda wanalalamika, wanawapeleka mafunzo nje, mkirudi mnataka kuondoka, msitake maisha ya haraka .Wengine tumefika tulikofika kwasababu ya kutulia na kuvumilia, tulianza kazi na mshahara mdogo,hatukukimbia,"amesema Profesa Mkumbo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...