Na Said Mwishehe, Michuzi Blog

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako ametoa pongezi kwa uongozi na watumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kutokana na namna ambavyo wamejipanga na kutoa huduma bora kwa wanachama wa Mfuko huo.

Pia Profesa Ndalichako ametoa maelekezo kwa mfuko huo kuhakikisha wanaendelea kuwakumbusha waajiri ambao hawajajiunga na mfuko kuhakikisha wote wanajiunga na kutoa michango ya wanachama wao na kwa sasa Rais Samia Suluhu Hassan amepunguza kiwango cha fedha cha uchangiaji pamoja na ulipaji  faini,lengo kumpunguzia mzigo mwajiri.

Akizungumza leo na viongozi na wafanyakazi wa Mfuko huo akiwa katika ziara yake ya kikazi na  kuangalia shughuli za Mfuko Profesa Ndalichako aliyekuwa ameambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Patrobas Katambi amesema ameridhishwa na utendaji kazi wa mfuko huo.

"Niwapongeze wafanyakazi kazi ,nimeridhishwa kwa namna ambavyo mmejipanga kuwahudumia wafanyakazi ambao ni wanachama wa mfuko huu hasa wale wanaopata matatizo wakiwa kazini kama ugonjwa au ulemavu ukiwemo wa viungo wakiwa kazini.

"Mfuko huu ni muhimu kwasababu wenyewe unaanza kumsaidia mfanyakazi tangu akiwa kazini pindi anapopatwa na changamoto, mfuko unaonesha ambavyo mtumishi anathaminiwa hata akiwa kazini , hivyo Serikali inaendelea kutekeleza sheria ya mfuko wa fidia kwa Wafanyakazi.WCF imefikisha miaka sita lakini kwa namna wanavyotoa huduma utadhani wana miaka mingi sana"amesema Waziri Ndalichako.

Wakati akiendelea kuzungumza na menejimenti na wafanyakazi wa WCF ,Waziri Ndalichako ametoa rai kwa mfuko kuendelea kuhamasisha wafanyakazi kujiunga na mfuko na kwamba waajiri 28,153 wamejisajili na waajiri 2000 bado hawajajisajili na mfuko ,hivyo ni vema wakaendelea kuwafuatilia,lengo ni kuhakikisha waajiriwa ambao wako kazini wakipatwa na changamoto wawe na uwezo wa kuendelea kuhudumiwa.

Waziri Ndalichako amezungumzia Mifumo ya TEHAMA katika mfuko huo ambavyo iko vizuri na imetengenezwa na vijana walioko ndani ya mfuko huo na kwamba asilimia 95 ya shughuli za mfuko zinafanyika kwa mfumo wa TEHAMA.

"Nitoe mwito kwa Wafanyakazi wanapopatwa na matatizo wazingatie sheria ya mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ili kupata huduma za matibabu, ushauri nasaha ambao utamsaidia mtumishi angalau kupewa tumaini baada ya kupata ulemavu ukiwa kazini.Wakati anapata matibabu pia kuna kiasi cha fedha ambacho mhusika atakuwa anakipata wakati akiwa na changamoto.

"Niahidi nitasimamia kuhakikisha haki za watumishi ambao wamepata changamoto kazi wanapata huduma kwa haraka na nitoe rai pale anapotokea mtumishi amepata matatizo basi nyaraka zake ziwasilishwe haraka kwa ajili ya kupata huduma zinazostahili,"amesema.

Kuhusu uwekezaji ambao umefanya na WCF,amesema  wote una tija, uwekezaji uliofanywa na mfuko umekuwa wa faifa ,lakini amesisitiza wajibu wa mfuko kulinda uwekezaji huo kwani unatokana na michango ya wanachama.

"Mfuko uko vizuri na katika kipindi cha miaka sita wanapata hati safi, katika mahesabu wako vizuri,niwaombe tuendelee kufanya kazi.Mfuko huu ni mzuri mpaka unanitoa jasho na vijana walioko kwenye mfuko huu wanafanya kazi.Vijana mko na mama nitawalea vizuri,tutangeneza fursa kwa vijana ,lakini pia na watu wenye ulemavu nao watapewa kipaumbele kwani wengine ulemavu wao wameipata wakiwa kazini.

"Nimefurahishwa sana na mfuko huu na pale kwenye changamoto tutashirikiana kutatua, kikubwa taarifa ziwe zinaandaliwa vizuri,na wawe wanaweka na vifungu vya sheria kwa kile wanachokihitaji, sitaki kuuziwa mbuzi kwenye gunia,kukiwa kuna jambo la mfanyakazi tuwe tayari kukesha kwa ajili ya kumhudumia,"amesisitiza.

Awali Naibu Waziri wa Wizara hiyo Patrobas Katambi amesema kwa ufahamu wake mfuko hup ni moja ya mfuko bora barani Afrika, mfuko una umri wa miaka sita lakini utendaji wao ni kama wana uzoefu wa karne, hiyo  inathibitisha kuwa tunao Watanzania wenye ujuzi mkubwa wa kutumia taifa lao

Pia amewapongeza mfuko huo katika eneo la Uwekezaji kwani kabla ya kuwekeza wanafanya tathimini kwa lengo la kulinda mfuko huo.Aidha amesema Wafanyakazi wanapopata madhila ya ulemavu wanaendelea kuwepo katika mfuko ,hivyo ni vema wakajiunga na mfuko huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia wa Wafanyakazi Dk.John Mduma amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Ndalichako huku akieleza mfuko huo utaendelea kutoa huduma kwa ufanisi."Tukuhakikishie Waziri tutaendelea kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa na kwa kutumia mifumo ya Tehama tuliyonayo tunaamini tutaendelea kuwa bora.Pia tutaendelea kutoa elimu kwa waajiri na waajiriwa kuhusu mfuko huu ili waone umuhimu wake."

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalicho( katikati waliokaa) akiwa na viongozi wengine wa Wizara hiyo , menejimenti na wafanyakazi wa WCF baada ya kufanya ziara ya kikazi katika mfuko huo jijini Dar es Salaam
Baadhi ya watumishi wa mfuko wa WCF wakiwa kwenye kikao kazi kati yao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalicho( hayupo pichani)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalicho akizungumza na wafanyakazi,Mejimenti na wajumbe wa bodi ya WCF wakati alipofanya ziara yake ya kikazi katika mfuko huo.
Patrobas Katambi ambaye ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu akizungumza wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ya Waziri wa Wizara hiyo Profesa Joyce Ndalicho na watumishi wa mfuko wa WCF
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalicho (wa tatu kulia)akimsikiliza mmoja ya wanachama wa mfuko wa WCF ambaye alifika katika Ofisi za mfuko huo kufuatilia fidia baada ya kupata changamoto akiwa kazini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...