Na Mwandishi Maalum - Dar es Salaam

WAUGUZI wanaofanya kazi katika wodi za wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) pamoja na wodi zingine wametakiwa kutokutumia simu muda mwingi wawapo kazini kwani mazingira yao ya kazi yanawataka kuwa karibu na wagonjwa wanaowahudumia kutokana na maisha yao kuwa hatarini.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua mafunzo  ya wiki 27 ya  jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi (Critical Care Emergence) yanayotolewa na Taasisi hiyo kwa wauguzi kutoka Hospitali mbalimbali nchini.

Prof. Janabi alisema katika watumishi wa afya wauguzi ndiyo wanaokaa na wagonjwa muda mrefu wodini na vifo vingi vya wagonjwa vinatokea huko,  hivyo basi watumie muda wa kazi vizuri  kwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa kwa kufanya kila kinachotakiwa ili kuokoa maisha yao na iwe ni bahati mbaya mgonjwa amefariki.

“Unapokuwa kazini tumia muda mwingi kutoa huduma kwa mgonjwa na siyo kutumia simu, haikatazwi kuongea na simu pale utakapopigiwa  simu ya umuhimu pokea au kutumiwa ujumbe wa umuhimu ujibu,  kama ni kutumia simu kwa mawasiliano ya kawaida utayafanya  baada ya muda wa kazi”,.

“Ukisikia mashine ya cardiac monitor ambayo inafanya uangalizi wa karibu kwa wagonjwa mahututi inalia usipuuze fahamu kuwa kuna kitu hakiko sawa nyanyuka mahali ulipo nenda kamuangalie mgonjwa kama yuko salama,  ukikuta yuko salama angalia mashine ina shida gani”, alisistiza Prof. Janabi.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo  alisema Taasisi hiyo kutokana na huduma inazozitoa ikiwemo ya upasuaji wa moyo iliona kuna uhitaji wa kuwa na wataalamu wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi na kuamua kuwasomesha wataalamu wake kozi hiyo  nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uuguzi ambao ndiyo waandaaji wa kozi hiyo Robert Mallya alisema wazo la kufundisha mafunzo hayo  lilikuja baada ya Serikali kuzihamishia hospitali zote za mikoa katika  wizara ya Afya na kuhakikisha hospitali hizo zinakuwa na ICU ambazo zitatoa huduma ya kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi. Kutokana na uhitaji uliopo wakaona kuna haja ya kuanzisha kozi hiyo ili wabadilishane ujuzi  walionao nao na wauguzi wengine nchini.

Mallya alisema kozi hiyo inatolewa kwa mara ya kwanza katika Taasisi hiyo baada ya  kumalizika kwa kozi hiyo watatangaza nyingine ili wale wanaotaka kusoma nao wapate nafasi ya kusoma na kuwataka washiriki wa kozi hiyo pindi watakapomaliza na kurudi  katika maeneo yao ya kazi walete mabadiliko ya utoaji wa huduma katika Hospitali walizotoka.

“Uhitaji wa utaalamu huu ni mkubwa sisi tunawaandaa ili muweze kutoa huduma hii kwa wagonjwa wa ICU tumieni miezi sita kujifunza ili mtakapomaliza mkatoe huduma kwa wagonjwa, kuwafundisha wenzenu na kuwa mabalozi wazuri.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake wa kozi hiyo Afisa Uuguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando Archileus Dominick alisema watautumia muda vizuri katika kujifunza na anaamini watajifunza mambo mengi ambayo yatawasaidia katika kazi zao za kila siku za kuwahudumia wagonjwa.

Washiriki wa kozi hiyo ambao wako 12 watajifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa aliyepo katika mashine ya kumsaidia kumpumua (Ventilator)na jinsi ya kutumia mashine hiyo. Jinsi ya kutumia mashine ya Cardiac Monitor ambayo inafanya uangalizi wa karibu kwa wagonjwa mahututi, kuustua moyo ulioacha kufanya kazi (Defibrillation).

Pia watajifunza matumizi ya mashine inayosafisha damu ya mgonjwa wa figo na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa anayehitaji huduma ya dharula,  jinsi ya kutoa tiba maalum za wagonjwa wa figo, kutoa dawa za wagonjwa wa moyo na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa ambaye moyo wake haufanyi kazi vizuri (Basic Life Support – BLS, Advanced Cardiac Life Support – ACLS).
















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...