Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizindua rasmi mradi wa nyumba 644 za makazi Magomeni Kota zilizojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA.)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa nyumba 644 zilizojengwa na  Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) katika eneo la Magomeni Kota leo jijini Dar es Salaam.



RAIS Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la wakazi wa Magomeni Kota la kununua nyumba zilizojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) katika eneo hilo kwa kutoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuruhusu wakazi hao kununua nyumba hizo kwa utaratibu wa Mpangaji-Mnunuzi kwa kurejesha fedha ya ujenzi pekee bila gharama ya ardhi.


Rais Samia ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua nyumba 644 zilizopo katika eneo la Magomeni Kota na kueleza kuwa kama ilivyoahidiwa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Joseph Magufuli  wakazi hao wataishi miaka mitano bure na kwa miezi mitatu ya awali hawatachangangia gharama za huduma jumuishi.

''Nimeridha kuwa baada ya miaka mitano wananchi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba hizi kwa utaratibu wa  Mpangajii-Mnunuzi na kurejesha gharama za ujenzi pekee, hatutawatoza gharama ya ardhi kwa sababu tukifanya hivyo mtashindwa kuzinunua.'' Amesema.

Aidha amesema, kwa wakazi ambao wapo tayari kulipa gharama za ununuzi wa nyumba hizo wanaruhusiwa kulipa kidogo kidogo bila riba huku wakiendelea kuishi katika makazi hayo.

Kuhusiana na utunzaji wa mradi huo Rais Samia amewataka wakazi hao kuzingatia usafi na kudumisha upendo na mshikamano;

''Ninawaomba mtunze mradi huu kwa kuzingatia usafi wa nyumba hizi ambao ni dhamana yenu kwa sasa, nyumba kama hizi tunategemea mpikie gesi hatutegemei mpikie kuni katika maghorofa haya.'' Amesema.

Rais Samia ameitaka wakala hiyo kushirikiana na  Shirika la Nyumba la Taifa (NHC,) na Watumishi Housing kukutana na sekta binafsi na kuona sehemu wanazoweza kuwekeza kwa kuwa hadi sasa wapo tayari kushirikiana na TBA  katika kujenga maeneo yote ambayo yapo tayari kujengwa ili kuleta maendeleo ya haraka zaidi.

Pia, amempongeza  Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro kwa hekima na ubunifu uliotumika katika kupambana na changamoto hadi kukamilisha ujenzi huo kwa kutekeleza sera ya matumizi bora ya ardhi ya kujenga nyumba za kutosha kwenye maeneo ya Umma ili wananchi wengi waweze kunufaika na miradi ya namna hiyo.

''Nawaomba TBA kumalizia kujenga eneo lililobaki lakini nawapongeza kwa kupata wazo la kuweka Machinga Complex, SuperMarket pamoja na sehemu ya maegesho ya magari ambayo ninataka mjenge maegesho ya kisasa ambayo yataweka magari mengi.'' Amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema wizara inaendelea kuratibu upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga majengo katika maeneo mengine yaliyorejeshwa Serikali Kuu kutoka TEMESA na katika kuhakikisha mradi huo unatunzwa Wizara kwa kushirikiana na TBA wameandaa mwongozo ambao umezingatia mambo muhimu ambayo utazifanya nyumba hizo zidumu kwa muda mrefu.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amesema Kazi za ubunifu, usanifu, ujenzi na usimamizi zimetekelezwa na TBA kwa kushirikiana na TEMESA kwa kutumia Wataalam wao wenyewe, na kazi hizo zilizingatia mabadiliko chanya ya ukuaji wa sekta muhimu pamoja na kanuni na viwango bora vya ujenzi vya Serikali.

Arch. Kondoro amesema ujenzi huo ulianza mwezi Oktoba, 2016 ambapo eneo lililojengwa hivi sasa lina ukubwa wa ekari 9, na umegharimu jumla ya shilingi bilioni 52.19 na kukamilika kwa asilimia 100.

Amesema katika kuunga  juhudi za Rais  Samia Suluhu Hassan na kwa kuzingatia ukubwa wa eneo hilo TBA iliamua kuanzisha miradi mingine kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani kwa kujenga majengo ya kibishara yanayotoa huduma kwa wakazi wa eneo hilo.

Amesema mradi huo umeweza kutoa ajira kwa Wataalam 60 wa fani mbalimbali, ajira kwa mafundi na vibarua 350 wa kila siku,  kuwajengea uwezo Wataalam wa fani mbalimbali pamoja na nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo Vikuu na vya Kati na wakati wa utekelezaji wa mradi huo TBA ilikarabati Kituo cha Afya cha Magomeni.

Pia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema uzinduzi wa nyumba 644 za Magomeni Kota ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais Samia ya kuhakikisha anaendeleza miradi yote iliyoachwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, na hapo amethibitisha kwa vitendo kwa kutoa shilingi bilioni 52 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.

Amesema ujio wake katika uzinduzi huo umemaliza mambo mawili ikiwemo kufuta fitina zote zilizokuwa zikijengwa juu ya wakazi hao wa Magomeni Kota, pamoja na matapeli waliokuwa wakija kuwaonesha watu nyumba hizo na kuwaambia zinapangishwa.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Magomeni Kota, Bw. George Abel amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewafanyia mambo makubwa kwa kuwa wakazi wengi wa eneo hilo ni Wazee, Wajane na Wastaafu ambao kipato chao ni cha chini, lakini Rais Samia amewawezesha kuwatoa katika kipato cha chini na kuwapeleka katika kipato cha kati, na wataishi hapo miezi mitatu bure bila kulipa gharama za huduma pia watakaa miaka mitano bure kama walivyoahidiwa. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akikagua mradi wa nyumba 644 zilizojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) katika eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akikabidhi mfano wa ufunguo kwa Bibi. Mwajuma Sama na Mzee Henry Ngwemba kama ishara ya kuwakabidhi nyumba hizo rasmi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro wakati akitoa maelezo juu ya utekelezaji wa mradi huo wa nyumba 644 za makazi Magomeni Kota.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kuzindua mradi wa nyumba 644 za makazi zilizojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA.)

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...