WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama, ikiwemo mifumo mbalimbali na majengo umesaidia kuchochea utoaji wa haki kwa wananchi kwa wakati ambapo ameshuhudia ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, utunzaji mzuri wa kumbukumbu na nyaraka na pia utoaji wa huduma kwa njia za kidijitali.

Ameyasema hayo  leo Mei 23, 2022 mara baada ya kumtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kufanya naye mazungumzo mafupi ambapo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji mkubwa wa utoaji huduma za haki kwa wananchi. 

Amesema kuwa yule anayeijua Mahakama jinsi ilivyokuwa kabla ya uboreshaji huo atagundua kuna hatua kubwa imefanyika. Walioanzisha uboreshaji huo wanastahili pongezi. 

"Labda niwakumbushe kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa sasa, Balozi Hussein Katanga ndiye aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa kwanza wa Mahakama na ndiye aliyeanzisha uboreshaji huu. Amefanya kazi kubwa ambayo imeendelezwa na wale waliomfuatia. Kusema kweli, Mahakama inastahili pongezi.” Amesema.

Dkt. Ndumbaro amebainisha pia kwa sehemu ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama unaenda sambamba na kuhakikisha mashauri yaliyopo mahakamani yanasikilizwa ndani ya muda mfupi iwezekenavyo. “Kama ambavyo wanasema, haki iliyocheleweshwa ni haki iliyodhurumika. Kwa hiyo, tusicheleweshe haki na Mahakama imeshafanya hivyo na inaendelea kufanya,” amesema.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kwa sasa shauri katika Mahakama ya Mwanzo linatakiwa kuisha ndani ya miezi sita, katika Mahakama ya Wilaya na Hakimu Mkazi shauri lazima liishe ndani ya miezi 12 na katika Mahakama Kuu isizidi miaka miwili, hivyo amesema hata kama mashauri hayo yakiisha ndani ya siku moja hicho ndicho kinachotakiwa.

“Ile habari ya kesi kukaa mahakamani miaka 10 imeisha sasa kwa sababu mtu ambaye anakwenda mahakamani anadai haki, tunapomchelewesha tunachelewesha haki yake. Kwa hiyo, niwaombe wananchi tusilalamike kwamba usikilizaji wa kesi unakwenda haraka sana, tuiunge mkono Mahakama kwa hili ili anayedai haki aipate ndani ya muda mfupi kadri inavyowezekana,” amesema.

Akizungumzia kilichojiri kwenye mazungumzo yao, Mhe. Dkt. Ndumbaro amefurahi kupata fursa ya kuitembelea rasmi Mahakama ya Tanzania akiwa Waziri wa Katiba na Sheria na kukutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, ambaye amemweleza jinsi gani Mahakama imefanya kwenye uboreshaji katika utoaji haki, katika kuwafikia wananchi na katika kupata mrejesho kutoka kwa wananchi.

“Amenithibitishia kwamba kasi ya uboreshaji wa huduma za utoaji haki inaendelea kwa kasi kubwa ili kuhakikisha sio tu haki inatendeka lakini pia ionekane inatendeka. Amenihakikishia kuwa Mahakama kama Mhimili ambao upo huru kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utaendelea kutoa ushirikiano katika mambo ya kisera kwa Wizara ya Katiba na Sheria,” amesema.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akisaini kitabu cha wageni mara Baada ya kutembelea Mahakama  leo Mei 23, 2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...