Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akizungumza na wajumbe wa kamati yake na watendaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili ya kamati hiyo mjini Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA.Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akielezea ushirikiano wa MKURABITA na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuwezesha urasimishaji wa biashara za wanyonge kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili ya kamati hiyo mjini Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA.Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dkt. Seraphia Mgembe akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili ya kamati hiyo mjini Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITAKiongozi wa Kikundi cha Umoja Group, kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za sabuni, shampoo na mafuta ya kupaka, Bi. Lucy Ngulai akimueleza Mjumbe wa Kamati ya USEMI Mhe. Margaret Sitta (Mb) namna MKURABITA ilivyompatia mafunzo ya ujasiriamali yaliyowawezesha kurasimisha biashara zao.Katibu wa Kikundi cha Tungi Youth Initiatives kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za viatu, Bw. Raban Anselmo akiushukuru Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali yaliyowawezesha kurasimisha biashara zao.

…………………….

Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro

Wajasiriamali mkoani Morogoro wameishukuru Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kuwapatia elimu iliyowawezesha kurasimisha biashara zao ambazo zimeboresha maisha yao.

Wajasiriamali hao wametoa pongezi hizo kwa MKURABITA mjini Morogoro walipotembelewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa katika banda la MKURABITA wakati wa Maonesho ya Tano ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyohitimishwa jana.

Kiongozi wa Kikundi cha Umoja Group, kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za sabuni, shampoo na mafuta ya kupaka, Bi. Lucy Ngulai amesema kabla ya kupatiwa mafunzo na MKURABITA walikuwa wakiuza bidhaa wanazozalisha kwa kutembeza mitaani lakini baada ya kupatiwa elimu ya ujasiriamali wameweza kupata leseni ya biashara na kurasimisha rasmi biashara yao.

“Elimu hiyo ya ujasiriamali tuliyopewa na MKURABITA imetuwezesha kupata fursa ya kunufaika na mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na manispaa ya Morogoro hivyo tumeweza kukuza mtaji wetu,” Bi. Ngulai ameeleza.

Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Tungi Youth Initiatives kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za viatu, Bw. Raban Anselmo amesema kikundi chake kimenufaika na MKURABITA kwa kurasimisha biashara yao baada ya kupatiwa mafunzo.

Bw. Anselmo amesema kuwa, licha ya MKURABITA kuwapatia mafunzo inawasaidia pia katika kuwatafutia masoko ya bidhaa wanazozalisha ikiwa ni pamoja na kuwaongezea ufanisi kiutendaji.

Naye, mjasiriamali aliyenufaika na MKURABITA ambaye anafanya uzalishaji wa gundi, Bi. Loyce Ntandu amesema awali alikuwa ni mmachinga ambaye anachukua bidhaa dukani na kwenda kuwauzia wateja wake mitaani lakini baada ya kuwezeshwa na MKURABITA amekuwa na ofisi zake ambazo anazitumia kuwahudumia wateja wake.

Bi. Ntandu ameongeza kuwa, MKURABITA imempatia elimu ya namna ya kutunza mahesabu yake ikiwa ni pamoja na kupanga kazi zake kibiashara, hivyo ameishurukuru MKURABITA kwa kumpatia elimu bora iliyomuwezesha kurasimisha biashara yake.

Akizungumzia utendaji kazi wa MKURABITA, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amewaeleza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuwa MKURABITA wanafanya kazi kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuwezesha urasimishaji wa biashara za wanyonge.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, licha ya kufanya kazi na Mamlaka za Serikali za Mitaa, MKURABITA pia inafanya kazi na taasisi za kifedha ili kuwawezesha wananchi wanaopatiwa Hati za Haki Miliki za Kimila kupata fursa ya kukopa mikopo kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo, biashara na ujasiriamali ambazo zitaboresha kipato na maisha yao.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wako kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Morogoro yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA, ambapo wamefanikiwa kutembelea Kituo Jumuishi cha Huduma cha Manispaa ya Morogoro na kuwatembelea wajasiriamali walionufaika na MKURABITA katika Maonesho ya Tano ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyoanza tarehe 08 hadi 14 Mei,2022 katika Viwanja vya Jamhuri Morogoro.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...