UTAFITI uliofanywa na serikali mwaka 2014 umeonyesha kuwa asilimia 29 ya watoto wa miaka 5-17 sawa na watoto millioni 4.2  wanatumikishwa katika sekta mbalimbali nchini huku sababu zinazochangia ni  umasikini.

Aidha, imeelezwa kuwa unyanyasaji wafanyakazi wa ndani bado ni changamoto kubwa hivyo kuanzia sasa serikali itaanza kuangazia upande huo ili kuhakikisha wanapata haki zao.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Patrobas Katambi jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga utumikishwaji watoto kwenye shughuli hatarishi yaliyoshirikisha wadau mbalimbali wa mashirika 40.

Katambi alisema kuwa kati ya watoto hao wanaume ni asilimia 29.3 na wasichana ni asilimia 28.4 ambao hutumikishwa katika sekta mbalimbali ikiwemo Mashambani, migodini, viwandani licha ya sheria kukataza watoto wa umri huo kutumikishwa.

Alibainisha sababu zinazopelekea kuwepo kwa suala hilo nchini kuwa ni umasikini, Vifo vya wazazi na walezi, mifarakano katika familia, mila na desturi kandamizi kwa watoto zenye mazingira ya kuonewa.

Alifafanua kuwa madhara yanayotokea kutokana na hali hiyo ni kuongezeka kwa umasikini, kuwa na taifa lenye watu wasiojua kusoma na kuandika, kuendea kwa magonjwa mbalimbali kama ukimwi.

“Unakuta huko watoto wanaingiliwa kimwili bila ridhaa yao na wanafanya mapenzi kabla ya wakati..mazingira ni magumu kama hatua hazitachukuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,

Pia, madhara mengine ni watoto kufariki katika umri mdogo hivyo kuwataka wadau kuweka nguvu kwenye suala la utumikishwaji watoto katika mazingira hatarishi,”alisema.

Kuhusu kunyanyasika kwa wafanyakazi wa ndani, Katambi alisema kumekuwa na changamoto hiyo hasa wenye umri chini ya miaka 18, huku wengi wao hawalipwi kiasi kinachotakiwa na serikali.

“Kwa sasa serikali itaangaza eneo hili maana wengi wanafanya kazi chini ya masaa ya kawaida unakuta hana muda wa kupumzika wakati mwingine anafanya mpaka majukumu ya mama mwenye nyumba na hali hii hupelekea wengine kubakwa na wababa wenye familia.

Tutakutana na mashirika haya ili kufanya tathimini ya Walibi huku lies hatua maana wapo ambao wakipewa ujauzito wanafukuzwa na waajiri wao kumbe ni ya baba mwenye nyumba hivyo huo ni unyanyasaji,”alisema.

Alifafanua kuanzia mwaka ujao wizara za kisekta zitakaa kwa pamoja kuangalia namna suala hilo linavyoenda ili hatua zichukuliwe kwenye maeneo husika maana kutakuwa na tathimini ya mashauri ya watoto maana ni aibu kuwepo halafu hayafanyiwi kazi.

Aidha, alisema ili kukabiliana na suala hilo serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kuhusu athari za utumikishwaji na kuwataka wahanga kutoa taarifa kwenye madawati ya jinsia yaliyopo kwenye vituo vya polisi nchini.

Kwa upande wake, Mratibu wa kitaifa kutoka mtandao wa kupinga utumikishwaji watoto nchini, Scholastica Pembe alisema watoto wengi wanatafuta ajira ili kujisaidia wenyewe na kukabiliana na changamoto ya umasikini.

Alibainisha mtandao huo kwa sasa una wanachama 40 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar huku lengo likiwa ni kuleta wadau karibu ili kufanya kazi kwa pamoja.

Alitoa wito kuwa mikataba ya kitaifa iliyoingiwa ya kutokomeza utumikishwaji watoto nchini ili kujipima nini kimefanyika, tulipokwama na nini kirekebishwe.

Pia, sheria zinahitaji maboresho wapi ili ziendelee kung’ata wanaofanya utumikishaji  kwa watoto ili kutokomeza ajira hizo nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...