Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro akizungumza na Wananchi wa wilaya hiyo katika moja ya mikutano yake iliyofanyika hivi karibuni.



Na Thobias Mwanakatwe, Ikungi


WAKULIMA wa kata saba zinazolima viazi vitamu wilayani Ikungi mkoani Singida wamelalamikia kukithiri kwa vitendo vya wafanyabiashara na madalali kununua mazao yao kwa kutumia vipimo vya lumbesa visivyokubalika kisheria.

Malalamiko hayo yalitolewa juzi na viongozi wa kata ya Puma wakati Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro, alipofanya mkutano na madiwani, wenyeviti wa vijiji, vitongoji, watendaji na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili wananchi kwenye maeneo yao.

Kata zinazolima viazi katika Wilaya ya Ikungi ni Puma, Kituntu, Ihanja, Isyeke,Makiungo, Dung'unyi na Ikungi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ( UVCCM) kata ya Puma, Hangida Ramadhani, alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakienda katika maeneo ya vijiji vya kata hizo na kutaka kuuziwa viazi kwenye magunia yaliyojazwa kupita uzito wa kawaida wa kilo 100.

Ramadhani alisema kwa ujazo wa lumbesa wakulima wamekuwa wakiuza viazi kwa bei ya Sh.55,000 kwa ujazo wa zaidi ya kilo 200 badala ya kilo 100 unaokubalika kisheria.

Alisema kuwa ni vyema Serikali ikaingilia kati tatizo hilo ili wafanyabiashara hao wasiendelee kuwanyonya wakulima wakati wanaponunua mazao na hivyo kuendelea kuwa masikini.

Alisema ununuzi wa mazao hayo kwa kutumia vipimo hivyo hauwanufaishi wakulima ambao wamekuwa wakitumia nguvu kubwa na muda mrefu katika kuzalisha, badala yake huwapa faida wafanyabiashara.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro, akijibu malalamiko hayo alisema serikali itashughulikia tatizo hilo na kwamba imeshaanza kwa zao la alizeti ambalo nalo kulikuwa na ulaghai kama huo kwa wakulima.

Muro alisema changamoto kubwa iliyopo ni kwa wakulima wenyewe ambao baadhi yao wamekuwa wakikubaliana na kuwauzia wafanyabiashara mazao yao kwa bei ya chini yakiwa bado yapo shambani kwa vipimo vya lumbesa ambavyo kimsingi havikubaliki.

"Njaa haina adabu ukiendekeza njaa utakufa maskini, hivi sasa tumekubaliana alizeti iuzwe kwa njia ya mnada lakini wapo baadhi ya wakulima wanakwamisha na hivyo kutoa fursa kwa dalali ambaye anapiga hela nyingi kuliko mkulima wakati hana shamba wala hajui bei ya mbolea," alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...